Na Mroki Mroki, JamhuriMedia
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Septemba 19,2023 kuwa ni siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mbarali na Kata sita (6) za Tanzania Bara.
Tume ilitangaza uchaguzi huo baada ya kuketi katika kikao chake cha Agosti 5, mwaka huu na siku hiyohiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima, akatoa taarifa kwa umma juu ya uwepo wa uchaguzi huo mdogo.
Tayari mchakato wa Uchaguzi huo umeshaanza ambapo Agosti 13 hadi 19, 2023 wagombea walichukua fomu za uteuzi, uteuzi ulifanyika tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi ambazo zilianza tarehe 20 Agosti, 2023 zinaendelea hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
Wagombea 14 kutoka vyama vya siasa 14 vyenye usajili wa kamili walichukua fomu za uteuzi na kati yao wagombea 13 wameteuliwa kuwania kiti hicho cha ubunge Jimbo la Mbarali. Mgombea wa Chama cha NRA hakurejesha fomu, hivyo alikosa sifa za kuteuliwa.
Wagombea walioteuliwa kuwania Ubunge Jimbo la Mbarali na vyama vyao kwenye mabano ni Halima Magambo (AAFP), Osward Mndeva (DP), Zavely Seleka (UDP), Exavery Mwataga (CCK), Mary Daudi (UPDP), Modestus Kilufi (ACT-WAZALENDO), Morris Nkongolo (TLP), Hashim Mdemu (ADC), Fatuma Ligania (NLD), Mwajuma Milambo (UMD), Bahati Ndingo (CCM), Husseni Lusewa (ADA-TADEA) Bariki Mwanyalu (DEMOKRASIA MAKINI). Mgombea wa Chama cha NRA, Makuke Makuke hakurejesha fomu za uteuzi.
Aidha vyama vya siasa 17 vilijitokeza kuchukua fomu kwaajili ya kuwania nafasi za Udiwani katika Kata sita za Tanzania Bara ambapo jumla ya wagombea 45 waliteuliwa kuwania nafasi hizo.
Kata zinazofanya uchaguzi mdogo ni Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Jumla ya wagombea 58 wameaminiwa na vyama vyao vya siasa na kupewa ridhaa kuwania nafasi zilizowazi, kwa kufanya hivyo, vyama hivyo vya siasa vimewatendea haki wanachama wao na wananchi kwa ujumla kwa kuwa wamepata haki ya kikatiba ya kugombea lakini pia wanachama na wananchi, watapata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.
Wagombea hawa 58 walioteuliwa na Tume ni wale waliopendekezwa na vyama vyao vya siasa kugombea kiti cha Ubunge na Udiwani ambapo pia walijazana kuwasilisha fomu za uteuzi katika Ofisi za Uchguzi katika Jimbo na Kata husika.
Aidha, wagombea Ubunge waliwasilisha fomu za uteuzi katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo na wagombea Udiwani kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata. Fomu za uteuzi za wagombea wote ziliwasilishwa siku ya uteuzi kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni.
Wagombea hawa wote siku ya uteuzi walijaza na kusaini mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi fomu ya maadili ya uchaguzi.
Wagombea hawa walijaza fomu hizo kukiri kuheshimu na kuyazingatia maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na viongozi wa vyama vyao mwaka 2020 wakati wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa Tanzania Bara.
Uwepo wa maadili ya Uchaguzi unalenga hasa kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi na wa kuaminika. Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria , kanuni na taratibu za uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.
Vyama vya Siasa, Serikali na Tume walikubaliana kuwajibika kuyatekeleza Maadili hayo yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343. Viongozi hao kwa pamoja walisema “Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha Maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea pamoja na wanachama wote wa vyama vya siasa”.
Sheria, Kanuni na miongozo yote iliyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 bado inatumika na kufuatwa na vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchagzi na Serikali katika chaguzi hizi ndogo za udiwani.
Tayari Kampeni za uchaguzi zimeanza tangu siku moja baada ya uteuzi na zitaendelea hadi siku moja kabla ya siku ya kupiga kura.
Wakati wote wa kampeni wagombea wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni za uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni.
Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni utasaidia katika kuweka uwanja huru na waamani wa ufanyaji wa uchguzi.
Vyama vya Siasa na wagombea pamoja na wafuasi wao wanapaswa kuepuka kufnya siasa za fujo na za vitisho dhidi ya upande mwingine.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi au asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.
Tume itatoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote ambayo yanafanya uchaguzi mdogo. Lakini pia zipo asasi tatu ambazo zimepewa kibali na Tume kutoa elimu hiyo kwa baadhi ya maeneo.
Elimu hiyo inayotolewa ni ile ya kumuwezesha Mpiga Kura kutambua sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwa ni pamoja na utaratibu mzima wa kufunguliwa na kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.
Lakini pia elimu hiyo itasaidia kutoa hamasa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.
Asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na maeneo watakayotoa elimu hiyo ni Alpha and Omega Reconciliation and Peace Building (AREPEB), itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika Jimbo la Mbarali, Umbrella of Women and Disabled Organisation (UWODO) itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika Kata ya Mtyangimbole na Bright Child Development Tanzania (BRIGHT CHILD), Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Kata ya Mwaniko.
Ni muhimu wananchi katika maeneo yote yanayofanya uchaguzi mdogo wakajitokeza kwa wingi kusikiliza sera za vyama na wagombea kisha kwa utashi wao wachague viongozi wanaowafaa kujaza nafasi zilizowazi.
Mwandishi wa Makala haya ni Afisa Habari Msaidizi Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.