Na Josephine Majura WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa itaanza kufanya malipo ya fidia kwa wananchi wa Kipunguni waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam ambao madai yao yamehakikiwa na hayana vikwazo vyovyote.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azan Zungu, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kipunguni waliopisha ujenzi wa Uwanja wa Ndenge wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Naibu Spika aliuliza swali hilo baada ya Naibu Waziri wa Uchukuzi , Mhe. David Kihenzile kujibu maswali mbalimbali ya wabunge kuhusu fidia za wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa Viwanja vya Ndege mbalimbali nchini.
Mhe. Dkt. Nchemba, alisema kuwa wananchi walishapewa mwongozo na Serikali kwa kuwa iligundulika kuna baadhi ya wananchi walipewa maeneo mbadala ambayo yalikuwa sehemu ya madai na kuna baadhi ambao walikuwa wanahitaji fidia zaidi.
Alisema Serikali imeshapeleka timu ya wataalamu kwenda kufanya uhakiki ili kuainisha madai na kupata madai sahihi kutokana na kuwepo kwa madai ya kuwa kuna baadhi ya wananchi wanadai fidia zaidi.
“Sasa, tunaendelea kutafuta fedha ndani ya mwaka huu wa fedha unaoendelea ili kuanza kufanya malipo”, alibainisha Mhe. Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa tathimini mpya ya ardhi na mali iliyofanyika kwa wakazi 1,184 inaonesha kuwa Serikali italipa zaidi ya shilingi bilioni 144, ikilinganishwa na tathimini ya awali iliyofanyika mwaka 2009 ambayo ilionesha kuwa wakazi hao walistahili kulipwa shilingi bilioni 15.5.