Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akisaidiana na mafundi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kutandaza mabomba ya maji.

Ule usemi wa baada ya dhiki ni faraja, umeanza kudhihirika kwa wakazi wa Salasala, Wazo na Madale jijini Dar es Salaam baada ya baadhi ya maeneo hayo kuanza kupata huduma ya maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA).

Maeneo hayo ni makazi mapya, hivyo hayakuwa na miundombinu ya maji, lakini katika kipindi cha miezi mitano tayari wameanza kuyaona matunda ya Dawasa mpya, huku wananchi wakifurahia kupunguza gharama za kununua maji.

Modesta Faustine, ni mkazi wa Salasala katika Kitongoji cha Kilimahewa, anasema ameishi katika eneo hilo kwa miongo miwili sasa lakini hakuwahi kupata maji ya bomba, isipokuwa yale ya kununua kwenye ‘maboza’.

“Unajua maji ni uhai, kwetu sisi wanawake maji ni kila kitu, ndiyo maana utakuta mama ndiye anahangaika kuhusu maji na si baba…tumeishi hapa kwa zaidi ya miaka 20 sasa, hatukuwahi kupata huduma ya maji kutoka iliyokuwa Nuwa, City Water wala Dawasco, ila sasa hii Dawasa mpya…

“Nakumbuka mwaka jana alitembelea hapa Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, akawaagiza Dawasa watuletee maji, anasema hataki kuona tukiendelea kupata shida ya maji. Kweli leo hapa kwangu unaona nina maji ndani ya fensi yangu…” anasema Modesta.

Modesta anasema ameanza kuyaona maisha mapya baada ya Dawasa kufikisha maji katika eneo la Salasala, Kilimahewa. Anasema alikuwa anatumia wastani wa Sh 100,000 kununua maji kwenye ‘maboza’.

Anasema kwa kupata maji ya Dawasa anaamini kutampunguzia matumizi, maana kwa utaratibu atawajibika kulipia unit ambazo ametumia kwa mwezi, ikilinganishwa na maji ya ‘boza’. Unit moja ya maji ni sawa na lita 1,000, na Dawasa wanauza unit moja kwa Sh 1,663.

Ramadhani Maliganya, mkazi wa Salasala Kilimahewa Juu, anasema anaipongeza serikali pamoja na Dawasa, kwa kuwapelekea huduma ya maji, huku akisema sasa anapata huduma hiyo muda wote.

“Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali, maana kwetu sisi kupata maji imekuwa ni ndoto iliyogeuka kweli. Maji ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu, lakini pia katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu, sasa tunasubiri huduma ya majitaka,” anasema Maliganya.

Wakati wakazi wa Salasala wakiendelea kufaidi namna ilani inavyotekelezwa, Dawasa imeanza kuwasambazia maji wananchi wa Kata ya Wazo na vitongoji vyake ikiwa ni utekelezaji wa ahadi.

Dawasa imewekeza na imejenga tanki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni sita zitakazofanya wakazi hao kupata maji kwa kipindi chote bila mgawo.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kumaliza kazi na kuwapatia wananchi maji, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa, amewaomba wasimamizi wa vizimba (maduka ya kuuzia maji) kuuza maji kwa Sh 50 kwa ndoo na si Sh 100 kama ilivyokuwa awali.

“Leo mnafurahi kufunguliwa maji ila naomba muuze maji kwa Sh 50 kwa ndoo, sitaki kuona wananchi wanalalamika eti bei ni kubwa, mimi ndiyo msimamizi, naomba mtekeleze, mkumbuke na kulipa ankara zenu za maji ili Dawasa waweze kuwahudumia vema,” anasema Prof. Mbarawa.

Akizungumza mbele ya wananchi hao na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema kuwa kulikuwa na changamoto kidogo ila kwa sasa wananchi wote waliokuwa kwenye mtandao wa maji wa zamani wataanza kupata maji kuanzia saa 2 usiku.
Luhemeja alisema mradi huo una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni sita kwa sasa tofauti na ule wa zamani uliokuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita elfu sitini na kusababisha mgawo wa maji kwenye maeneo mengi.
“Kuanzia sasa hivi hakutakuwa na mgawo wa maji kwenye maeneo yote yaliyo na mtandao wa maji, mradi huu una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni sita, hivyo tatizo la maji kwa Kata ya Wazo, Madale na maeneo mengine limekwisha,” alisema Luhemeja.
Akielezea maeneo ambayo haujafika mradi kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa maji, Mhandisi Luhemeja amesema kuna fedha takriban Sh bilioni 115 zimeshapatikana kwa ajili ya kusambaza mabomba yenye urefu wa Kilometa zaidi ya 1,000 katika maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kuna fedha Sh bilioni 115 zimetengwa tayari kwa ajili ya mchakato wa ununuzi, pia tunakaribia kusaini mkataba na mkandarasi ambaye tumeshampata na nitawakaribisha wenyeviti wote wa mitaa kuja kushuhudia ikiwemo na wakuu wa wilaya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Februari 28, mwaka huu, nitawaita watendaji wote wa mitaa mkoani Dar es Salaam, wadau na viongozi na tutakutana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee ili kujadili utekelezaji wa mkakati huu mkubwa wa maji.

“Fedha tumepata na mkandarasi amepatikana, hivyo tutaanza ujenzi wa mradi huu mkubwa wa maji,” alisema Mhandisi Luhemeja.

Alisema maeneo mengi ya Dar es Salaam ambayo hayapati maji sasa yataanza kupata kwa wingi na kuwahakikishia wananchi ambao maeneo yao hayajapatiwa mabomba ya maji kuwa yatapitishwa miundombinu hiyo ili kila mwananchi anufaike na huduma hiyo.

Akizungumzia changamoto ya maji katika Kata ya Wazo, Mhandisi Luhemeja, alisema ilitokana na ongezeko kubwa la wananchi kwani pampu iliyokuwa katika eneo hilo ilikuwa na uwezo wa kusukuma lita 60,000 za maji.

“Wito wangu kwa wananchi ni kwamba, kwa kuwa maji hayakutoka muda mrefu huenda miundombinu ikawa imeharibika sasa, kama mtaona maji yanavuja toeni taarifa haraka,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo,  alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli, miradi mingi imekuwa ikitekelezwa na wananchi wawe na subira na wameahidiwa maji kuanza kutoka kwenye mabomba.
Chongolo alisema anaamini kuwa Mtendaji Mkuu wa Dawasa si mwanasiasa, hawezi kudanganya, kazi imefanyika na inaonekana ya kutoka uzalishaji wa maji lita elfu sita hadi milioni sita kwa sasa.
Amesema atafuatilia ili kujionea kama maji yameanza kutoka, Dawasa wamedhamiria kufika asilimia 95 ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.