Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Songea
WAKAZI wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuona umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa Barabara ya Mtwara Corrido (Songea by Pass) ambayo itasaidia kuondoa msongamano wa maroli katikati ya mji ,yanayosafirisha makaa ya mawe kutoka Mbinga kwenda mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuacha kuchafua mazingira kwa kumwaga makaa ya mawe hovyo barabarani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti tofauti Festo Mlelwa ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Seedfarm amesema kuwa ,hali ni mbaya kutokana na ongezeko la maroli hayo kupita katikati ya mji kunasababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo jambo ambalo linaweza kusababisha ajali ,ambapo ameitaka mamlaka husika kuharakisha ujenzi wa barabara ya mchepuko ya Mtwara Cordo ili kuondoa kero hiyo.
“Tunaiomba Serikali iharakishe mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara Cordo ambao utasaidia kuondoa msongamano wa maroli kwenye barabara kuu itokayo Mbinga-Songea -Njombe ili kuondoa usumbufu wa msongamano wa maroli ambayo yamekuwa mengi zaidi na kuturahisishia wafanyabiashara shuguli zetu za kila siku kama zamani,” amesema Mlelwa.
Naye John Haule (56), Mkazi wa Namanditi songea amesema, maroli hayo yamekuwa yakipita kwa mwendokasi hata kwenye maeneo yenye makazi ya watu bila kujali watumiaji wengine wa barabara na kusababisha ajali ambazo zingeweza kuzuilika kama kungekuwa na barabara ya mchepuko.
Hata hivyo ameiomba Serikali kusaidia kudhibiti uchafuzi unaofanywa na baadhi ya madereva wa makaa ya mawe kwa kudondosha makaa hovyo barabarani hali ambayo imechangia mji kuwa na sura tofauti ya uchafuzi.
“Kuna magari yanadondosha makaa ya mawe na hayo hivyo kumechangia kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira na pia msongamano mkubwa wa malori mjini tunaiomba Serikali iharakishe ujenzi huo ili kutuondolea kero hiyo,” amesema.
Akizungumzia malalamiko hayo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma , Mhandisi Ephatar Mlavi amekiri kuwepo kwa msongamano huo hata hivyo kuna juhudi zinafanyika ili kuwapunguzia kero wananchi.
Amesema,tayari uthamini umeshafanyika na kwa sasa mradi upo kwenye hatua ya manunuzi ambayo yanafanywa na makao makuu hivyo wanasubiri hatua inayofata ili kuanza kutekeleza mradi huo ambao unatarajiwa kuanza Novemba 2022.
Amefafanua kuwa,kutokana na ongezeko la maroli wanataka barabara ya Mtwara Cordo ipite kuanzia Namanditi kupita changarawe barabara ya Tunduru- Masasi, ili kupunguza msongamano huo kwenye makazi ya watu hasa maeneo ya mjini.
Aidha, ameongeza kuwa maradi huo unajengwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo amewataka wananchi kuendelea kutunza miundombinu kwani mradi huo ni wao pia pia ni vyema sasa kwa wasafirishaji makaa ya mawe kushirikiana katika utunzaji mazingira , pamoja na utunzaji miundombinu ya barabara na kuchafua kumwaga ovyo makaa ya mawe barabarani.
Alipohojiwa kuhusu kiwango cha ubora wa barabara hiyo kama kinaweza kuhimili upitaji wa malori hayo amesema barabara ina ubora wa kupita maroli yenye tani kuanzia 50 na kwamba haina tatizo ipo vizuri.