MTWARA
NA AZIZA NANGWA
Wananchi mkoani Mtwara wamesema kutokana na wimbi kubwa la ajali za barabarani hasa zinazotokana na pikipiki na magari, wanaona kuna umuhimu wa kuwa na huduma za madaktari bingwa wa mifupa kwenye maeneo ya vijijini, JAMHURI limeambiwa.
Kuwapo kwa huduma hizo kwenye maeneo ya vijijini kutaokoa maisha ya watu ambao watapata ajali na kuvunjika viungo vyao, hasa mikono na miguu, uchunguzi umebaini.
Takwimu zinaonyesha asilimia kubwa ya watumiaji wa usafiri wa pikipiki wapo maeneo ya vijijini na huko ndiko kuna kundi kubwa la waathirika wa kuvunjika mifupa kwa sasa.
Katika makala hii, JAMHURI limetembelea Mkoa wa Mtwara kuona hali halisi ya huduma zinazotolewa na madaktari bingwa wa mifupa kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) zinavyosaidia kutatua changamoto hii.
Katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya ST Benedict Ndanda, iliyopo wilayani Masasi, mkoani Mtwara, Josephat Ndukusi, anasema wao wameanzisha huduma za kibingwa hasa mifupa mwaka huu kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa kanda hiyo.
Ndukusi anasema hospitali hiyo ilianzishwa mwaka 1927 na tangu ilipofunguliwa kulikuwa na huduma zote, lakini huduma ya mifupa pekee ndiyo haikuwapo.
“Kwa kipindi chote hicho, wagonjwa wengi walipoletwa kutibiwa tulikuwa tukiwapa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI),” anasema Ndukusi.
Ndukusi anasema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya na wagonjwa wamekuwa wengi kutoka wilaya mbalimbali na mikoa jirani wakipelekwa katika hospitali yao, uongozi uliona haja ya kutafuta suluhisho kwa kuleta huduma za kibingwa katika tiba ya mifupa kwenye hospitali hiyo ili kuwasaidia wananchi.
“Unajua wananchi wengi huku wana hali ya chini, hivyo tulikuwa tukipata huruma, tulitaka kuwasaidia lakini tulikuwa hatuna jinsi,” anasema Ndukusi.
Anasema baada ya kuona haja ya kuwa na huduma hizo, uongozi uliamua wakubaliane na MOI kwa kuingia nao mkataba wa kuwapelekea madaktari bingwa wa mifupa ili watu wapate huduma hizo Ndanda.
“Lengo jingine pamoja na huduma hiyo pia madakari na manesi wetu waweze kujengewa uwezo na wajifunze huduma za mifupa zinavyotolewa kwa mtindo wa kutuletea wataalamu kila wiki mbili. Tunashukuru walikubali,” anasema Ndukusi.
Anasema baada ya kupeleka ombi la kutaka ushirikiano, Mkurugenzi wa MOI, Dk.
Respicious Boniface, alikubali bila pingamizi na kwa haraka. Katika makubaliano hayo, waliweka vipaumbele vya kushirikiana katika utoaji wa huduma za mifupa za kibingwa.
Ndukusi anasema baada ya kusainiwa mkataba, ST Benedict Ndanda imekuwa inatoa rufaa chache kwenda MOI, hasa zenye kuhitaji utaalamu maalumu kama huduma za ubongo na nyonga, lakini za miguu na mikono wamekuwa wakizifanya hapo hapo hospitalini.
Anasema kupelekwa kwa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo ya rufaa ni ukombozi mkubwa kwa watu wasiojiweza, kwani wengi wao ni wananchi wenye hali duni.
Ilipofika huduma ya madaktari bingwa kutoka MOI imewasaidia watu wenye uwezo mdogo kumdu gharama za matibabu, kwa sababu ni nafuu ikilinganishwa na awali ilipokuwa lazima mgonjwa apelekwe MOI.
“Kabla ya kuanza huduma ya upasuaji wa mifupa walikuja wataalamu kutoka MOI wakakagua vifaa vyetu iwapo vinakidhi viwango, wakagundua kwamba vipo vizuri na hata vyumba vya upasuaji vipo kwenye hali inayotakiwa kwa ajili ya upasuaji,” anasema na kuongeza: “Baada ya zoezi hilo, wakaturuhusu kushirikiana nao katika kutoa huduma kwa kushirikiana na madaktari wao,” anafafanua Ndukusi.
Anasema kuja kwa huduma ya tiba ya mifupa katika hospitali yao kumechochea hata mapato kuongezeka, kwani wamekuwa wakipokea wateja kutoka sehemu mbalimbali hadi nje ya nchi, ikiwamo Msumbiji.
Kwa sasa wamepunguza kutoa rufaa nyingi kila wiki za mifupa kwenda MOI kwa sababu huduma hizo zinapatikana katika hospitali hiyo na vifaa vipo vya kutosha.
Anataja chanzo kikubwa cha ajali kuwa ni pikipiki, kwani wananchi walio wengi wanapenda kutumia usafiri huo katika shughuli zao kutokana na unafuu wake.
Ndukusi anasema baada ya kuwapo kwa huduma za kibingwa hospitalini hapo, imekuwa chachu ya kuongeza wateja wa tiba ya mifupa kufikia kati ya wagonjwa 35 mpaka 40 kwa wiki mbili.
Ajali nyingi zinazotokea katika mkoa huo zinawahusu hasa vijana na watoto, kwani ndio wengi wanaoletwa hospitalini hapo wakiwa wamevunjika mifupa kwa kugongwa ama kugonga.
“Hospitali yetu kwa sasa tumebahatika kuwa na vyumba vinne vya upasuaji, ambapo vyumba vitatu ni kwa ajili ya upasuaji wa aina tofauti tofauti na kimoja ni upasuaji wa mifupa,” anasema Ndukusi.
Hospitali ina mikakati ya kutanua huduma zake na kuwa na vitengo vingine vingi kama huduma za ubongo, moyo, meno, macho na saratani ili kuwaondolea adha wananchi kwenda Dar es Salaam kupata huduma hizo kwa siku zijazo.
Ndukusi anasema kwa sasa wamekwisha kuanza maandalizi ya kuwaleta madaktari bingwa wa meno, macho, usingizi na huduma za dharura hivi karibuni.
Mikakati ni kuona tunakwenda mbali zaidi na kuwapata hata madaktari bingwa wa mionzi na ‘endoscopy’ kuchunguza viungo ndani ya mwili, kwani eneo hili wana wagonjwa wengi lakini hawana huduma ya kibobezi, japo wapo wanaoihitaji zaidi kwa sasa.
Ameongeza kuwa kuwapo kwa madaktari wa MOI kumewasaidia kuongeza ujuzi kwa madaktari na manesi wao kujua namna ya kumhudumia mgonjwa wa mifupa kitaalamu, tofauti na mwanzo.
Kuna uhitaji pia kwa madaktari na manesi kwa ajili ya Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), kwani kitengo hicho si kila nesi anaweza kutoa huduma kwenye wodi hiyo.
“Kabla ya kufanyiwa upasuji lazima mgonjwa afanyiwe maandalizi ya kutosha na manesi, hasa kwenye vipimo na vifaa, ili kuwarahisishia madaktari kujua hali ya mgonjwa kabla ya upasuaji kumsaidia kuwa salama,” anasema Ndukusi.
Mikakati mingine ni kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kipekee kwa Kanda ya Kusini itakayokuwa na huduma za kibingwa zote na madaktari wabobezi katika fani mbalimbali.
Kwa sasa wameanza kuwasomesha wataalamu wao ili waweze kuwatumia na kutoa huduma za kibingwa na kuondoa utegemezi kutoka katika hospitali nyingine siku za usoni.
Hospitali hiyo imefikia mafanikio makubwa kwa msaada wa wafadhili, ambapo wanazalisha hewa tiba ya oxygen kwa kutumia mtanbo wao (Production Plant) kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji hewa hiyo.
Wanaiomba serikali iwajali kwa kiasi kikubwa kutokana na kutoa huduma kubwa kwa jamii, kwani bila kufanya hivyo gharama za matibabu kwa wagonjwa zitakuwa kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Dk. Tumaini Minja, ambaye ni Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka MOI aliyepo Hospitali ya Rufaa ya ST Benedict Ndanda, anasema wameamua kutoa huduma hizo baada ya kuona kuna uhitaji mkubwa. Anasema MOI iliamua kufanya kazi Ndanda baada ya kuona kuna wagonjwa wengi wanaokwenda kutibiwa kwao.
Minja anasema wao kama wataalamu wapo hapo kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa, sanjali na kuwajengea uwezo madaktari na manesi wa Ndanda ili waweze kuwahudumia vizuri wagonjwa wa mifupa.
“Kwa kweli huduma imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaokoa watu katika ulemavu, kwa sababu wapo wagonjwa walikuwa wanashindwa kuja MOI kutokana na kukosa fedha, hivyo walikuwa wakiishi na maumivu ya muda mrefu, lakini kwa sasa hawapo kutokana na huduma za mifupa kusogea karibu yao,” anasema Minja.
Anasema kwa sasa wameweza kupunguza rufaa za kwenda MOI kwa ajili ya matibabu ya mifupa, labda wagonjwa waliovunjika migongo, nyonga na kichwa ambao nao si wengi.
Stanley Jeuza, msimamizi wa Jengo la Upasuaji, anasema kuwapo kwa madaktari hao kila siku kumeleta chachu ya utendaji mkubwa kwa madaktari na manesi.
Jeuza anasema yeye kazi yake ni kuhakikisha vyumba vya upasuaji na vifaa vipo sawa muda wote na wagonjwa wanapata huduma kwa vigezo vinavyotakiwa.
Anasema kuwapo kwa taasisi hiyo kumewajengea uwezo katika nyanja mbalimbali, ikiwamo matibabu na maandalizi ya wagonjwa wa mifupa ya kitaalamu.
“Mpango huu umetusaidia kupata wafadhili kutoka sehemu mbalimbali kuja kutusaidia vifaa vya kisasa vya upasuaji wa mifupa,” anasema Jeuza.
Jafari Ali ni mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo na anasema baada ya kuvunjika mfupa wa mguu kwa ajali ya pikipiki alikata tamaa kabisa.
Kutokana na hali yake duni kimaisha na alivunjika mguu mara sita, hakutegemea kama mguu wake ungerudi katika hali ya kawaida kutokana na ulivyokuwa.
“Nilikata tamaa kabisa ya kutibiwa na kupona, lakini madaktari wa MOI niliposikia wapo hapa walinisaidia sana kupona. Nashukuru sana na ninaomba huduma ziongezwe zaidi ili kutusaidia sisi watu wa hali ya chini kupata matibabu,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema hospitali hiyo iliona changamoto za watu wa Kanda ya Kusini ni kubwa kwenda kupata huduma MOI, hivyo ikasogeza huduma hizo kwenye Hospitali ya Rufaa ya ST Benedict Ndanda ili kuwasaidia wananchi.
Dk. Boniface anasema huduma za kibingwa zilikuwa zinahitajika katika kanda hiyo ili kupunguza rufaa za kuja MOI. Tangu huduma hizo zipelekwe Ndanda, imekuwa kinara na mkombozi katika utoaji huduma za kibingwa, hasa katika eneo la mifupa.
Anasema taasisi yake imekuwa ikitoa madaktari bingwa kila wiki wakibadilishana kwa ajili ya kwenda kuwajengea uwezo madaktari na manesi wa Ndanda ili waweze kutoa huduma hizo mbele ya safari bila kuwategemea madaktari wa MOI.
“Lengo la taasisi ni kupanua huduma za kibingwa za mifupa katika kanda ili madaktari waliopo katika maeneo hayo waweze kufanya tiba za kibingwa katika maeneo yao badala ya kuwapa wagonjwa rufaa. Tangu mpango huo uanze tumeweza kupunguza idadi ya rufaa kutoka mikoa ya kusini kuja kupata huduma za mifupa MOI. Hii haiusishi wanaokuja kutibiwa binafsi hapa MOI.
“Lengo jingine la mpango huu ni kuwaondolea gharama kubwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kibingwa katika hospitali hizo. Kama bodi, baada ya kuona idadi kubwa ya wagonjwa tuliridhia kutoa madaktari wetu kwenda kwenye hospitali za baadhi ya kanda kufanya tiba za kibingwa za mifupa ili kuwapunguzia gharama wananchi,” anasema Dk. Boniface.
Anasema MOI waliona umuhimu wa kuwapatia elimu ya kuwajengea uwezo na mafunzo ya kutosha madaktari wa kanda katika baadhi ya mikoa ili iwe rahisi kwa eneo hilo kukusanya wagonjwa na kuwatibu mifupa huko huko.
“Baada ya kuona umuhimu huo madaktari walikuwa tayari kufanya kazi hizo kwenye mikoa, japo mwanzoni walianza kuwafundisha madaktari wenzao katika mikoa na kuwawezesha baadhi ya vifaa ili kazi zao ziwe rahisi,” anasema.
Dk. Boniface anasema kwa sasa hospitali hiyo imepunguza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa MOI kutoka mikoa hiyo. “Programu ya kuwafundisha madaktari ilikuwa ya mwaka mmoja. Tulivyoona inakwenda vizuri tuliongeza mwaka mwingine ili kuwajengea uwezo madaktari wengi zaidi na kuondoa msongamano katika hospitali za kanda kama Ndanda na nyingine zote zilizopo mikoa ya kusini,” anasema Dk. Boniface.
“Lengo kubwa la kuanzisha programu hiyo ni kuhakikisha MOI inawakomboa watu wa kusini kwa kuwasogezea huduma ya matibabu haya karibu ili kuwasaidia wagonjwa wasipoteze gharama na hata kupoteza maisha kwa ajili ya kukosa huduma za kibingwa za mifupa,” anasema Dk. Boniface.
Wiki ijayo usikose kutufuatilia kwenye makala maalumu ya huduma za kibingwa za mifupa katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi.