Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mary Masanja amesema Serikali itawashirikisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri ya kukiondoa Kijiji cha Ngaresero katika Pori Tengefu la Ziwa Natron.

Naibu Waziri huyo ameeleza hayo Bungeni leo Mei 16,2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro,Emmanuel Lekishon Shangai, lililoulizwa na Zaytun Swai kuhusu lini Serikali itaondoa Kijiji cha Ngaresero kwenye eneo la Pori Tengefu la Pololet baada ya kujumuishwa kimakosa.

Amesema sababu ya kuwaondoa wananchi kwenye kijiji hicho ni kutokana na Pori hilo kuwa ni moja kati ya maeneo yaliyotolewa maelekezo na Baraza la Mawaziri kuwa lipandishwe hadhi.

Amefafanua kuwa kulingana na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2019, ardhi ya Pori Tengefu Ziwa Natron ipo kwenye kundi la ardhi ya Hifadhi.

Aidha,Masanja ameweka bayana kuwa Serikali itaenda kushughulikia mgogoro huo kwa kukutana na wananchi ili kufikia muafaka na hatimaye pori hilo liwe na hadhi iliyotarajiwa.