Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imekamilisha ujenzi wa jengo la dharura (EMD) liliojengwa kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa Sh milioni 69 lengo kuwapa wananchi huduma ya dharura kwa ukaribu.
Hayo yalisemwa jana na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Princepius Mugishagwe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari walipotembelea majengo mawili ya Wodi ya Huduma ya Dharura na wodi ya kisasa maalum.
Mugishagwe alisema hospitali hiyo ilianza mwaka 2021 kukiwa na majengo ya wagonjwa wa nje (OPD),huduma za maabara na kliniki ya wajawazito na watoto na inawahudumia takribani wateja 200,000.
“Jengo la dharura limekamilika kwa kutumia Force Akaunti litasaidia wanaopata magonjwa ya Mlipuko,ajali za aina zote ikiwa vifaa vyote vipo zamani walilazimika kufuata huduma ya dharura mjini Geita kilomita 90”alisema Mugishagwe.
Fundi Mzawa, Jackson Clement alisema amepata zabuni ya ujenzi wa Wodi hizo amenufaika kuongeza kipato kwenye familia na kuajiri vijana 12 kwenye kazi ya ufundi.
Meneja wa umoja wa vijiji 14 vinavyozunguka Mgodi huo Joseph Lubega alisema kazi za ujenzi wa miradi mbalimbali zinafanywa na wananchi kwenye maeneo husika lazima waanze kutabuliwa kupitia ofisi hiyo na watu takribani zaidi ya 1000 wamepata ajira za muda mfupi.
Kaimu meneja mahusiano na Mazingira kutoka mgodi huo, Zuwena Senkondo alisema wameendelea kutekeleza miradi ya kimkakati wa kuangalia ujenzi wa ‘Private wodi’ ambayo itakuwa chanzo cha mapato kwenye hospitali na mgodi uko mbele kushirikiana na serikali na jamii.
‘Sisi tunavyopata uzalishaji ndiyo tunavyozidi kujenga miradi kwa kuwakwamua wananchi tumetoa Sh milioni 69 kwaajili ya ujenzi jengo la Dharura matumaini yetu watu wapate huduma karibu”alisema Senkondo.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Husna Toni alisema ufadhili wa fedha zinazotolewa kwaajili ya huduma ya jamii (CSR) wamefanikiwa ukamilishaji wa jengo la dharura ambayo itasaidia utoaji huduma nzuri na bora.