Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
WANANCHI 387 wameweza kutembelea katika Banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ili kuweza kupata msaada wa kisheria hususani katika maeneo ya migogoro ya ardhi na mirathi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, alipozungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo kwenye Viwanja vya maonesho hayo, Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.
Amefafanua kuwa hadi kufikia jana idadi ya waliotembela imefika 387 ambapo kati ya hao 195 ni wanawake na 192 ni wanaume.
“Na wengi waliojitokeza wamekuwa wakihitaji msaada katika maeneo ya migogoro ya Ardhi pamoja na masuala ya mirathi. Hata hivyo tunaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali na tunatarajia idadi hiyo itaongezeka,” amesema.
Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutumia jina lake kusaidia watanzania kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
“Mama Samia ametoa nafasi hii tutoe huduma ya msaada wa kisheria bila malipo kwa watanzania, huduma hii ni kubwa kwa sasa tunapaswa kuisambaza katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar,” ameeleza.
Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa tayari wameshazunguka mikoa saba ya awali huku akisema wana mpango wa kufika mikoa mingine 10 kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kutoa usaidizi wa watanzania wenye matatizo katika Sheria.