Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wanaendelea na unyanyasaji wao mashariki mwa jimbo la al-Jazirah, ambapo wanashambulia raia.

Katika Jimbo hili, unyanyasaji umeenea kwa kiwango kikubwa sana. Kwa mfano, katika mji wa Al-Hilaliya, kilomita 70 kutoka Wad Madani, wakazi wamezingirwa.

Mauaji, ubakaji, udhalilishaji wa pamoja, uhamisho wa kulazimishwa na uharibifu wa vijiji vimekuwa vitendo vya mara kwa mara vya wanamgambo wa RSF.

Wanajeshi hao walikusanya idadi ya watu misikitini na katika viwanja vya umma, wakiwazuia kuhama. Kulingana na mashahidi kadhaa, wakazi wa mji wa Al-Hilaliya wamefukuzwa kutoka kwa nyumba zao, lakini wamepigwa marufuku kutoka kwa mji wao uliozingirwa na RSF. Wale wanaotaka kuondoka eneo hilo lazima walipe ushuru kwa RSF.

Kulingana na mwanahabari Kamal al-Charif, familia yake iliyokuwa ikiishi mji wa Al-Hilaliya ilibidi kulipa kiasi cha euro 1,500 ili kuweza kuondoka kwa miguu. Wanajeshi hao walipora kila kitu, yakiwemo magari na mali nyinginezo.

Takriban wakaazi 70,000 bado wamekwama huko Al-Hilaliya wakiwa katika hali mbaya ya kibinadamu na kiafya.

Jiji hilo limezingirwa kwa muda wa wiki moja, wakazi wake hawana chakula na dawa na kwa sasa wanaugua kipindupindu. Kulingana na mashahidi wa ndani, RSF ilichoma maeneo ya umma na kuwabaka wanawake.

Wakati RSF inawashambulia raia kote nchini, wengi wanashangaa kwa nini jeshi la Sudani haliingilii kati na kwa nini ulimwengu unakaa kimya. Kulingana na vyanzo kadhaa, watu wasiopungua arobaini waliuawa au kufa kwa ugonjwa katika jiji hili lililozingirwa.