Na Ashrack Miraji, JamhiriMedia, Same

Watu saba wamefariki dunia na wengine 75 wamejeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea wilayani Same.

Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya Njoro na kuhusisha basi la Kampuni ya Osaka lililokuwa likielekea Dar es Salaam, ambapo ilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 52 walijeruhiwa.

Ajali ya pili ilihusisha basi aina ya Costa la Kampuni ya Mkokota majira ya saa 2 asubuhi ya leo, ambalo lilipinduka katika kona za milima ya Ilamba, na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi 23.

Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni wanakwaya waliokuwa wakisafiri kutoka Chome kuelekea Ndolwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema kuwa majeruhi wa ajali ya kwanza walipokelewa hospitalini majira ya saa nane usiku, huku majeruhi wengine 23 pamoja na miili ya marehemu sita ikifikishwa hospitalini mchana wa leo.

Baadhi ya majeruhi wa ajali iliyotokea usiku wameeleza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na mwendokasi, hali iliyomfanya dereva kushindwa kulimudu gari. Chanzo cha ajali ya pili chanzo chake kikielezwa kuwa ni kukatika kwa stering road.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, ameonesha masikitiko yake kutokana na vifo hivyo na kuwasihi madereva kuwa waangalifu wanapopita wilayani Same, hasa kutokana na hali ya hewa yenye upepo mkali.

Aidha, amewataka abiria kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wao wakiwa safarini ikiwemo mwendokasi.