Takriban wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini wameuawa katika mapigano katika vita vya Ukraine tangu waingie kwenye mapigano upande wa Urusi mapema mwezi huu, mbunge wa Korea Kusini amesema.

Lee Sung-kwon, akizungumza na waandishi wa habari baada ya bunge kupewa taarifa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya nchi hiyo, alisema wengine 1,000 wamejeruhiwa.

Alisema waliopoteza maisha ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu, na inaweza kuelezewa na wanajeshi hao kutofahamu eneo hilo, na vita vya ndege zisizo na rubani.

Ripoti za kwanza za majeruhi wa Korea Kaskazini zilikuja mapema wiki hii. Iliibuka mwezi Oktoba kwamba Kaskazini ilikuwa imetuma wanajeshi 10,000 kusaidia juhudi za vita vya Urusi.

Siku ya Jumatatu msemaji wa Pentagon ya Marekani alisema Wakorea Kaskazini waliuawa, bila kutaja idadi, na siku moja baadaye afisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina alisema kuwa kulikuwa na “mia kadhaa” waliouawa au kujeruhiwa.

BBC haijathibitisha madai hayo kwa uhuru.

Wanajeshi wa Korea Kaskazini, ambao hakuna hata mmoja wao aliye na uzoefu, wanaaminika kuwa walitumia wiki zao za kwanza nchini Urusi katika mafunzo na kisha katika majukumu ya usaidizi.

Majeruhi hao wanadhaniwa kutokea katika eneo la Kursk nchini Urusi, ambako wanajeshi wa Ukraine wanalinda eneo dogo lililotekwa wakati wa uvamizi wa ghafla mwezi Agosti.

Jumamosi iliyopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeanza kutumia “idadi kubwa” ya Wakorea Kaskazini katika mashambulio yake huko Kursk.

Hawafikiriwi kuwa wametumwa nchini Ukraine kwenyewe, ambapo wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni.