Ndugu Rais, walituambia kukaa kimya ni kukubali yote; bali kukemea yasiyofaa ndiyo busara na hekima ya kiongozi bora. Watu wako baba wanakupenda kama walivyowapenda marais wengine waliokutangulia. Sasa huu wasiwasi unatokea wapi?
Watu wamejaa wasiwasi mwingi katika macho yao. Wasiwasi ni tunda la moyo baada ya mtu kijiridhisha kuwa ametenda uovu mwingi na sasa anachelea kisasi. Hapo wasiwasi huidhoofisha nafsi yake na kumjaza mtu huyo hofu kwa kila akionacho.
Wameibuka waduduwatu wanaodai ni watetezi wa baba yetu. Baba wanakupenda hawa jamaa kuliko wanavyowapenda wazazi wao. Ukiwaona kama waliopoteza fahamu! Njaa na tamaa ukiviabudu unaweza kuvua nguo mbele za watu na usijali. Anapoongea utadhani amevuta bangi kwanza. Ufundi wake ni kutukana watu hadharani kama vile serikali yote imo mfukoni mwake. Timamu anaweka mtetezi anapojua kuwa mwenyewe ni dhaifu. Baba una udhaifu gani mpaka huyu adai ni mtetezi wako? Nani aliwahi kushinda kesi kwa matusi? Nchi inaonekana kama ina pango la wahuni.
Wananchi wanaulizana hakuna wa kumkemea? Wenye mamlaka wanashindwa vipi kumkemea? Au ndiyo wamemtuma? Tusingoje mpaka wananchi watuone na sisi ni wale wale.
Baba naungama mbele yako, mimi ni mkristu. Namwomba Muumba wangu anisamehe ninaposema alitokea mwana aliyelaaniwa akasema mambo anayoyafanya Rais ni miujiza mikubwa kuliko aliyofanya Yesu Kristu kwa wana wa Israel. Hana hata mfano mmoja wa kuonyesha. Kama reli ndiyo tunajenga. Kama bwawa la umeme ndiyo tunachimba. Hakuna ambacho tayafri tumekifanikisha. Huyu ni mpuuzi. Na kwa upuuzi wake hawezi kuishia hapo. Kesho atasema Rais wetu amefanya mambo makubwa kuliko hata ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; Muhamad (S.A.W). Naomba niwe mkweli. Ninajilazimisha tu kuamini kuwa baba yetu huenda bado hajamsikia kwa hili! Kukaa kimya kwa ufedhuli huu tutawakumbusha Watanzania wosia wa majonzi wa hayati Mhashamu Baba Askofu Evarist Marc Chengula. Alisema, “Ujumbe uliokuwa umetolewa na Maaskofu ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristu, lakini hawana imani ya dini hiyo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema. Narudia, uliwalenga wanafiki wanaodai kuwa ni wakristu, lakini hawana imani ya Kristu.’’
Aliwataka Wakristu kwa kutumia jumuiya zao ndogo ndogo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kuchagua watu ambao hawatawafanya waishi kwa kuogopaogopa’.
Akaongeza, “Tuangalie, kulialia tu hakuna maana…Hakuna maana tufurahie watu fulani tumewachagua, lakini tunaishi katika hali ya wogawoga, sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho.’’ Alale pema peponi!
Zimepita awamu nne, lakini sifa za awamu ya tano ni tofauti na zote. Huku watetezi waliojitoa fahamu na kule watu wasiojulikana. Utadhani tunapigania tutawale maisha! Kwa hii sifa ya kumpiku Mungu, tukibaki kimya tujue kuwa Wakristu siyo wajinga sana. Wanaweza wakanyamaza, lakini mioyo yao haiwezi kuwa ‘clear’!
Viongozi wao hawajasikika, lakini hawawezi kukosa fundo katika vifua vyao! Wenye mamlaka wanaposhindwa kumkemea wanaonyesha jinsi walivyo pamoja naye! Kuepuka unafiki tuache mara moja kutumia maneno yao ya kiimani tusijefanana na kengele mbovu iliyopasuka, iliavyo!
Wenye mamlaka ya kuzuia uhalifu kukiri kuwa hawawajui watu wasiojulikana ni kukiri kuwa wao ni sehemu ya uhalifu huo. Wawasaidie basi wananchi kujua faida ya kuwa na viongozi ambao wenyewe wamethibitisha kuwa wameshindwa kulinda uhai wa wananchi wao.
Baba kila awamu ilikuwa na rais wake. Hakuna rais aliyechukiwa na Watanzania. Tuliwapenda na kuwaheshimu. Walipofanya vema tuliwaunga mkono. Ambapo hatukuridhika tuliwaambia ukweli. Walitumia busara kutusikiliza bila kutuita wachochezi. Katika vipindi vyao hakuna aliyewaonyesha Watanzania makali ya upanga! Wananchi waliopotea kwa miujiza, hawakuwapo na kama walikuwapo, basi wachache. Na waliokufa walikufa kwa amri ya Mungu! Imeandikwa kila nafsi itauonja umauti! Waliingia wakawakuta Watanzania wenye furaha na umoja kama awamu ya tano ilivyowakuta. Walipoondoka waliwaacha katika furaha, uhuru wa kutoa mawazo yao na kukutana na wengine bila vizuizi. Hawakuonyesha woga wao kwa vyama vya siasa mpaka kuonekana kama walikuwa na ndoto ya kuwa marais wa maisha.
Baba usome ushuhuda wa mwanao! Anaandika, “Mwalimu Mkuu naomba nikiri wazi kuwa ‘wewe kwangu mimi- Mzee Ernest Mashuda wa Nzega Tabora, ni zaidi ya nabii! Pia ni mzalendo asilimia 100, wa nchi hii. Mimi hununua Gazeti la JAMHURI ili nisome tu unabii wako. Huzuni yangu kuu, anapoonyesha hakuelewi kabisa! Yuko bize na kuinyosha Tanzania tu! Daah, unabii uliomo kwenye toleo na. 410 la tarehe 6-12/8/ 2019! Nilitarajia unabii huu utolewe na Kardinali, Maaskofu, Mufti au Masheikh- bali wako kimyaaa’’.
Utamaduni wa kiongozi mkuu kabisa kukutana na viongozi wa ngazi ya chini kabisa ulikuwa haujapata kuonekana katika nchi hii. Tatizo kubwa ni pale kiongozi mkuu anapolazimika kufanya kazi yeye mwenyewe na makatibu kata. Hapo, kweli kazi ya urais itakuwa ngumu. Kazi yoyote unayoifanya na unaiona ni ngumu kila siku, jua kuna mahali pa kurekebisha. Hakuna kazi ngumu duniani.
Rubani bora ni yule anayejua vitufe vya ndege yake ambavyo akivibonyeza ndege hufanya atakavyo. Hata dege lingekuwa kubwa kiasi gani, ujue linaongozwa kwa vidole tu. Litaruka na kutua wakati mwingine kwa kidole kimoja tu. Hapa ni kazi kwa teknolojia tu. Nani aliishamuona rubani anashuka kutoka kwenye ndege akiwa na shati lililolowa jasho mgongoni kutokana na kazi ngumu ya kuiendesha ndege?
Baba bonyeza tu vitufe, nchi itapaa yenyewe. Vitufe vya nchi yetu ndiyo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya na vyombo vilivyopo. Rubani kuteremka chini na kuingia uvunguni mwa ndege ili kuirusha kwa ‘nguvu’ yetu wenyewe, haahaahaa baba! Watatucheka watu! Kuongoza nchi hakuhitaji nguvu ya misuli ya mwili. Wanao bado tunakuhitaji.
Ila, kwa ule wingi wa makatibu kata walioonekana Ikulu siku hiyo, umezimisha kelele zote za wauza mchele waliokuwa wanalia kukosa soko. Baba watukutu hawakosekani. Watakuja watu kupiga hesabu ni rais gani alikula na wasaidizi wake wengi zaidi alipokuwa Ikulu.