Nchi yetu kwa sasa imegeuka taifa la uchaguzi. Ukipita kwenye vijiwe vya kahawa, makao makuu ya vyama vya siasa, na hata hii Katiba mpya inayoandaliwa kila mtu analenga uchaguzi mwaka 2015. Tanzania ni nchi pekee kati ya nchi ninazozifahamu duniani, iliyojenga utamaduni wa kumaliza uchaguzi wanasiasa wakaanza harakati za uchaguzi unaofuata miaka mitano ijayo.
Nchi nyingi duniani zimekuwa na utaratibu wa kufanya kampeni za uchaguzi kwa muda usiozidi miezi mitatu, baada ya uchaguzi kufanyika kila kitu kinafungwa, wanachapa kazi. Nchi zilizoendelea wanaanza na mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama. Mchakato huu unachukua wastani wa miezi sita. Baada ya hapo wanaingia kwenye kampeni za kitaifa siku 90, kisha uchaguzi. Basi.
Sitaki kuweka mlolongo, niseme tu wanavyofanya Wamarekani na Waingereza. Kura zinapohesabiwa na kufikia asilimia 85 au 90 mgombea aliyeshindwa huwa anafahamu kuwa ameshindwa, anampigia simu aliyeshinda na kumpongeza. Baada ya hapo alfajiri siku inayofuata baada ya uchaguzi aliyeshinda anatoa hotuba kwa taifa na kueleza mwelekeo wake.
Sitanii, baada ya hotuba hiyo, lazima zipite siku kati ya 30 na 60 kabla ya kushika madaraka. Hapa wanakuwa wakikabidhiana madaraka. Rais Mteule anaanza kupewa siri za nchi na kuelezwa jinsi mifumo inavyofanya kazi na baada ya hapo na hata walioshindwa wanatumia muda huo kwenda mahakamani kama wanataka kufanya hivyo.
Kwa Marekani, Rais anaapishwa Januari 20 ya mwaka unaofuata, ilihali uchaguzi unafanyika Novemba 4 au 5 ya mwaka uliotangulia. Sasa hapa kwetu, tunashuhudia siasa miaka mitano. Ndani ya vyama anayeshindwa anaendelea kumfanyia fitina aliyeshinda ikibidi hata kura zake zipungue. Anayeshindwa anageuka kuwa adui. Wanafika hatua ya kutukanana hadharani.
Upinzani ndio usiseme. Ukishindwa ndio mwaka hadi mwaka unasusa kila jambo. Nakumbuka ni viongozi wawili tu, Freeman Mbowe aliyeshindwa na Jakaya Kikwete mwaka 2005, akahudhuria hafla ya kutangaza matokeo pale Karimjee. Mwingine ni Perofesa Ibrahim Lipumba, ambaye Mwaka 2010 naye alishindwa akahudhuri hafla kama hiyo mahala hapo.
Viongozi wengine wanasusa na kuzunguka nchi nzima wakieleza jinsi walivyoshindwa kwa fitina, na jinsi walivyoibiwa kura. Wanakaa wakieleza historia. Wanaeleza ufisadi, wanaeleza uzembe, lakini hawaelezi jinsi ya kutanzua tatizo. Ndani ya Chama tawala CCM na upinzani, kwa maana ya walioshindwa katika mchakato ndani ya chama, wote wanazunguka kueleza mabaya ya Serikali.
Kumbe kushindwa urais si mwisho wa uhunzi. Mwaka 2005 Chadema kilishindwa urais. Kiliposhindwa kikaamua kufanya kazi. Karatu nitaitumia kama mfano hai. Dk. Wilbrod Slaa aliposhinda ubunge, ingawa Chama chake hakikushinda urais akaamua kuwatumikia wana Karatu. Katika jimbo hili maji yalikuwa tabu kweli. Leo kwa Karatu tatizo la maji ni historia.
Jimbo la Moshi Mjini limekuwa chini ya Chadema. Pamoja na kwamba hawakushinda urais, Philemon Ndesamburo, wenyewe wanamwita Ndesa Pesa, amelisimamia jimbo hilo kwa ufasaha. Wanasomesha watoto, mjini umeendelea kuwa msafi na una maendeleo ya kweli.
Zitto Kabwe alishinda ubunge, ingawa chama chake hakikushinda urais, bado Kigoma ameifanyia mema mengi.
Amekuwa sauti ya Kigoma. Mara kadhaa ameeleza kero za Kigoma kuliko mtu yeyote. Kilichofuata ni nini? Leo ukienda Kigoma kuna barabara za lami usipime. Kuna kila dalili kuwa baada ya muda si mrefu barabara ya lami itakuwa imeunganisha Kigoma na Tabora, hivyo mtu ataweza kutoka kwa teksi Dar es Salaam hadi Kigoma.
Kwa bahati mbaya siasa hizi zinafanyika katika ngazi ya majimbo na mikoa na zinafanywa na viongozi wachache mno. Wengi wanasusa. Hawajihusishi na kazi zinazofanywa na Serikali au kuiambia Serikali ifanye nini. Hapo ndipo kosa lilipolala. Hapo ndipo nchi yetu inapopata hasara ya mwaka. Walioshindwa wanaendelea kuwinda urais katika muhula ujao.
Wiki iliyopita nilipata fursa ya kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya ukatili wa kijinsia. Mafunzo haya yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA). Tulikuwa tunafundisha waandishi wa habari jinsi ya kubaini viashiria vya ukatili wa kijinsia, aina za ukatili wa kijinsia, fumo dume, mila na desturi na imani potofu.
Mengine sitayazungumza, ila moja lililonigusa. Afya ya uzazi. Namheshimu kwa kiwango kikubwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi. Amefanya kazi nzuri. Dodoma ya sasa ina maghorofa utadhani uko Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dodoma kimebadili kabisa sura ya mji ule. Mji unapendeza.
Hata hivyo, tunapozungumza ukatili wa kijinsia ni pamoja na mambo ya msingi hasa yanayohusiana na afya. Dodoma ni Makao Makuu ya Tanzania. Katika Manispaa ya Dodoma kuna vijiji ndani yake. Kipo kijiji kinaitwa Mchemwa. Kijiji hiki wakazi wake wanaishi kwa mateso usipime.
Kina mama wanalazimika kutoka Mchemwa kwenda zahanati ya mbali ya Veyula. Kuna msitu kati ya Mchemwa na Veyula. Katikati ya pori hili, kuna vibaka walijipanga kuumiza wanawake. Wanawake wengi hulazimika kutumia baiskeli kama usafiri wa kutoka kijijini kwao kwenda Zahanati ya Veyula au Makutupola.
Kwa muda niliokaa Dodoma taarifa nilizopata kuna wastani wa matukio ya baiskeli nne kuibwa katika pori hili. Si hilo tu, wezi hawa wanapora baiskeli kutoka kwa kina mama wanaopeleka watoto kliniki. Kwa unyama na ukatili wanaofanyiwa kina mama wanaokwenda kupata huduma hii mbali, kama wanasiasa wangeingilia kati wakahubiri Mchemwa kujengewa zahanati, basi hali ingekuwa njema.
Ukiacha Mchemwa, kuna aibu ya kutisha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Pale kuna kituo cha kupokea kina mama wajawazito, ambao wanatoka katika wilaya za Bahi na Chamwino. Wajawazito hawa wanapewa hifadhi ya muda kabla ya kujifungua katika kituo kilichopo nje ya uzio wa hospitali hii.
Kina mama hawa wanakuwa ni wale ambao imethibitika kuwa mimba walizonazo zina matatizo ya aina moja au nyingine. Hawa wanakuwa wamepelekwa hospitalini pale kama sehemu ya rufaa. Kwa bahati mbaya, wajawazito hawa badala ya kusaidiwa wanazidi kuongezewa maumivu. Uchunguzi uliofanywa na wanahabari waliopata mafunzo yaliyoandaliwa na TAMWA, umebaini mambo ya kusikitisha.
Kwanza kituo hiki kina uwezo wa kulaza wajawazito 16. Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita kulikuwa kuna wajawazito wapatao 113. Ukiacha hilo la idadi kubwa ya wajawazito waliorundikana katika kituo hicho, vitanda wanavyotumia ni unyanyasaji. Kimsingi si vitanda, bali ni mazege tu sawa na makaro ya kuoshea vyombo.
Mazege haya ndiyo huwekewa magodoro kisha kulaliwa na kina mama. Kitaalam hairuhusiwi mwanamke mwenye mimba kulazwa katika sehemu yenye ubaridi kama sakafuni, ila kwa Dodoma katika kituo hiki wanafanya hivyo. Hii inawaathiri kwa kiwango kikubwa wanapofika saa ya kujifungua kwani uchungu hupotea.
Sitanii, si hilo tu, bali kituo hiki kina kunguni usipime. Uchunguzi umebaini kuwa Serikali haitoi huduma yoyote kwa kina mama hawa na hata wanapofikia muda wa kujifungua hulazimika kutembea umbali mrefu kuzunguka uzio, kupitia lango kuu kwenda kwenye wodi ya uzazi, baada ya mzunguko huo wanawake wengi wanajifungulia nje ya lango la hospitali.
Hali hii inasikitisha. Inawezekana wapo wasioumizwa na hali hii, ila TAMWA imeahidi kulivalia njuga. Waadishi wa Dodoma wamekwishaanza kulifanyia kazi, lakini kimsingi inauma kuliko maelezo. Kina mama hawa wanawaleta duniani malaika. Tungeweza kuwapunguzia adha kwa kuua kunguni, kuwawekea vitanda na kuepusha kulalia zege.
Si hayo tu, uzio wa kuingia hospitalini ungeweza kukatwa ukaruhusu kina mama kuingia moja kwa moja hospitalini wakitokea kwenye kituo hicho badala ya kuuzunguka. Tatizo ninalopata ni je, ni nani yuko tayari kuyasemea haya. Je, viongozi wetu wako tayari au wanakimbizana na uchaguzi mkuu wa 2015?
Napata shida kuamini iwapo Mkuu wa Mkoa wa Dk. Nchimbi anafahamu tatizo hili. Mama huyu ni mchapa kazi, mwenye huruma na upendo kwa binadamu wenzake. Huenda viongozi wasaidizi wake wakifika katika eneo hilo huwa wanamzungusha na kumwingiza katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma iliyokarabatiwa kwa kiwango kizuri.
Wanaishia kumwonesha maghorofa mazuri yaliyojengwa ya hospitali hiyo, lakini hawathubutu kumwambia kuwa kuna kina mama wenzake wanateseka mno. Ni imani yangu kuwa baada ya makala haya, TAMWA watafanya kila mbinu kuwasiliana na Dk. Nchimbi, kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuokoa maisha ya kina mama hawa. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Dodoma.