Kwa muda mrefu nimekuwa na tabia ya kutazama luninga na kujisomea magazeti ya Kenya, si tu kwamba nijiongezee ufahamu wangu kama mwandishi wa habari, bali pia ni kutokana na ukweli wa kuwahi kufanya kazi na kampuni moja kubwa ya habari ya nchi hiyo na Afrika ya Mashariki kwa ujumla. 

Mambo haya mawili yamekuwa sababu ya kuwa nikifuatilia masuala mengi yanayoendelea nchini Kenya – yawe mazuri ama mabaya.

Agosti 27, 2016 nilikuwa nikitazama moja ya vituo vya luninga nchini Kenya ikionesha moja kwa moja ufungaji wa tamasha kubwa la utamaduni wa watu wa Turkana nchini Kenya. Kwa mujibu wa Gavana wa Turkana, Josephat Nanok, tamasha hilo lilileta watu wengi kwa maelfu kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Pamoja na mambo mengine, lengo kubwa ambalo lilijificha kwenye tamasha lilikuwa kutangaza utalii wa utamaduni wa eneo hilo na Kenya kwa ujumla. Nchi kadhaa zilialikwa katika tamasha hili zikiwamo Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia.

Sijui kama Tanzania ilialikwa au la, lakini sikusikia ikitajwa katika tamasha hilo. Kama haikualikwa, siyo suala la kuhoji maana huo ulikuwa uamuzi na ukarimu wa mwandaaji wa tamasha, ingawa pia kwa walio katika sekta ya utalii wanaweza kujua kwa nini Tanzania haikualikwa.

Madhumuni makubwa ya makala hii ni kuzungumza na wenzangu katika tasnia ya habari, sekta ya utalii, watendaji serikalini na wananchi wengine kwa ujumla juu ya kile kilichozungumzwa baadaye katika tamasha la Turkana na tufanye nini katika mazingira kama haya.

Gavana Nanok anasema Turkana, ambayo ni kame sana mbali na kugunduliwa kwa mafuta na maji mengi chini ya ardhi, sasa inatambulika ndiyo eneo ambalo mwanadamu wa kwanza aliishi na kuwafahamisha wageni kwamba hapo walipo, Turkana, Kenya ndipo mahali alipoishi mwanadamu wa kwanza duniani.

Najua kwamba tafiti mbalimbali kujua asili ya mwanadamu zinaendelea duniani na hasa katika maeneo ya Bonde la Ufa, Tanzania, Kenya, Afrika Kusini na Chad. Matokeo ya ugunduzi yamekuwa yakichanganya na mara nyingine yamekuwa kila mwamba ngoma ngozi huvutia kwake, na hasa hasa kwa kutumia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi husika.

Bonde la Olduvai nchini Tanzania lilitajwa katika kongamano moja la kimataifa la vijana wapatao 1,000 jijini New York , Marekani, mtoa mada Mkenya aliitangazia dunia kuwa bonde hilo lipo nchini Kenya. Vyombo husika nchini Tanzania vilikanusha taarifa hiyo, ingawa sijui ni kwa kiwango na wepesi gani.

Kwa hiyo taratibu, mbali na kuamini kwamba huenda mwanadamu wa kwanza duniani aliishi katika bonde hilo, umaarufu wa bonde letu hili unaweza kuanza kupungua kutokana na kampeni za aina ya matamko kama ya Turkana.

Suala hili halikuanzia Turkana, maana mwaka 2013, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu katika serikali ya sasa nchini humo, alitoa kauli kama hiyo pamoja na kwamba amewahi kutembelea Ngorongoro na Bonde la Olduvai.  

Wenzetu hawa wanasema na kutangaza hasa katika vyombo vya nje na katika vipeperushi kwamba Mlima Kilimanjaro upo Kenya, Nyanda za Serengeti, Kreta ya Ngorongoro na hata madini ya tanzanite vipo Kenya.

Wanaposhtukiwa kuhusu Mlima Kilimanjaro, hugeuza kwa kuwaambia watalii kwamba wanakaribishwa nchini Kenya kujionea Mlima Kilimanjaro “upande wa Kenya.” Huu ni mlima unaotumika sana katika Kenya hasa hasa kwenye matangazo ya biashara na majina ya bidhaa.

Huenda ikawa vigumu hata kwangu tukiacha historia tuliyosoma wote kwamba Bonde la Olduvai ndilo linalodaiwa kuwa binadamu wa kwanza aliishi.

Tafiti zimekuwa zikiendelea na huenda kuna mabadiliko, ama taarifa hizi za kila siku zinaweza kubadilika kutegemea zinatolewa wapi, mdhamini na hatimaye tukageuka eneo la watu kuja kufanyia utafiti wa kujipatia uprofesa. Bila shaka wahusika watajibu.

Ninachosema hapa ni kwamba mambo haya hayafanyiki kwa bahati mbaya, mengi ni kwa makusudi na yanalenga sekta ya utalii ambayo Tanzania ni mshindani mkubwa wa Kenya ingawa sasa Ethiopia inakuja juu na imeipiku Kenya kwa mbali.

Kwa vile Kenya haiwezi kushindana na Ethiopia kwa sasa, nguvu kubwa za Kenya katika utalii imezielekeza kwa inayedhani ni mnyonge wake, Tanzania, ambaye kimsingi bado yupo nyuma katika kujitangaza na hajawa mtundu katika fitina halali za kibiashara.

Vyombo vyao vya habari vinajipambanua katika kuweka ajenda ya kuitetea na kuipamba Kenya. Sawa kabisa na hakuna kosa kwa kufanya hivyo. Hili ndilo eneo ambalo viongozi wa sekta husika Tanzania wanaweza kutia mkono wao kwa kuwatumia wanahabari waliopo katika kurekebisha hali hii.

Wanapaswa kujua, taarifa hizi za upotoshaji zinaiumiza sana sekta yetu ya utalii ingawa kuna ukweli pia kwamba yapo yanayosemwa Kenya kutokana na kutoijua historia na jiografia ya Tanzania.

Mfano mmoja ni wakati nikiwa Mhariri Mkazi wa moja ya majarida makubwa ya ukanda huu mwaka 2005. Habari niliyotuma Nairobi haikutumika kwa vile ilisema kuna sehemu inaitwa Malindi nchini Tanzania.

Mhariri alipoiona Malindi, aliiweka pembeni akidai Tanzania hakuna sehemu inayoitwa Malindi, ila ipo Kenya pekee! Ufafanuzi niliuotoa baadaye ndiyo uliyofanya habari hiyo ichapishwe tena baada ya wiki moja kupita.

Kwa hiyo, kwa wanahabari, jukumu la kuweka mambo sawa ni lenu. Vaeni uzalendo kama uliooneshwa na baadhi yenu wakati wa sakata la bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanga.

Hawa jamaa wana mambo mengi ambayo kimsingi yanatuumiza kama nchi. Kwa muda mrefu tunahangaika na suala la Loliondo, haitashangaza nikisema kwa miaka ya hivi karibuni Loliondo imegeuka makao makuu ya mashirika yasiyo ya kiserikali {NGO} ya Kenya.

NGO hizo za Kenya zimejipanga kukwamisha miradi yetu ya miundombinu tunayoipanga kupitia Serengeti. Wameishtaki Tanzania kwenye Mahakama ya Afrika ya Mashariki ama vyombo vingine vya kimataifa utadhani wao ndiyo viranja wa sehemu hii ya dunia.

Wamekwamisha nia ya Tanzania katika matumizi ya pembe za ndovu nchini kwa kukampeni usiku na mchana dhidi ya Tanzania duniani kote – Tanzania ikitaka pembe ziuzwe fedha itumike kuhifadhi wanyama, Kenya ikitaka zichomwe moto. Ni vyema tukajua tunaye jirani wa aina gani – hatugombani kwa sababu tu jirani mmoja ameamua kunyamaza.

Sasa kuna mtihani mwingine. Wameruhusu makazi katika hekta 17,000 kwenye msitu wa Mau huku miradi ya mabwawa huko Ewaso Ngiro imepamba moto. Bonde la Enapuiyapui ni roho ya mfumo wa ekolojia ya mto Mara na Serengeti lakini wenzetu wanafanya mambo ambayo yapo kinyume na mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maji katika mto Mara yanapungua kwa kasi, hali ambayo italiathiri Ziwa Viktoria na Serengeti. Mto huu una urefu wa kilometa 395 asilimia kama 70 ikiwa unapita Kenya. Kupungua kwa maji mto Mara kumesababishwa na shughuli na miradi inayoendelea Kenya.  

Hali hii imeathiri wanyama ndani ya Serengeti, na kwa kuona hili, TANAPA imeomba serikalini kupanua eneo la mbuga kuelekea Ghuba ya Speke, wilayani Bunda ili wanyama waweze kupata maji ya kutosha. Lakini upande wetu Tanzania tupo kimya na hatujapiga kelele.

Kwa upande wa wahusika katika sekta ya utalii na nyingine,  huu si wakati wa kudai tupo kwenye mchakato, tupo mbioni, mipango inafanywa, tunawasiliana na wadau kama Rais John Magufuli alivyowahi kusema, bali ni wakati wa kuchukua hatua.

Ushindani unaokuja Afrika Mashariki ni mkubwa sana, kwa vile nchi hizi zinashindanisha bidhaa mpya ya mafuta na gesi katika masoko ya kimataifa, huku utalii ukionekana kuwa moja ya nguzo za uchumi wa nchi hizi. Tujipange kwa ajili ya hili pambano kuu.

Kwa kutumia vyombo vyetu vya habari, dunia itajua kipi kinaendelea Tanzania na kwa usahihi. Taarifa za upotoshaji zinahitaji majibu sahihi wakati huohuo maana katika upashanaji habari suala la muda ni muhimu mno ingawa yapo tunayojibu, lakini tunachelewa.

Lakini mengine ni uzembe wetu wenyewe. Kulalamika kwamba Kenya inatangaza Mlima Kilimanjaro upo Kenya ni unyonge uliopitiliza. Sisi kwa upande wetu Tanzania nani alitukataza kutangaza kwamba Mlima Kilimanjaro upo Tanzania? Wenzetu Kenya wanasema, wanaandika, wanatangaza, wanahamasisha, basi na sisi tufanye vivyo hivyo na kwa kasi kubwa.

 

Mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa siku nyingi nchini na msomaji mkubwa wa JAMHURI.  Sasa ni mwandishi wa kujitegemea. Anapatikana kwa: [email protected] au 0753 700821.