Wanafunzi watatu na dereva mmoja wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha magari mawili likiwemo gari aina ya ‘Coaster’ na gari la mizigo aina ya Scania kugongana uso kwa uso alfajiri ya leo katika kijiji cha Gajal kilichopo wilayani Babati mkoani Manyara.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori kutokuwa makini barabarani na kuigonga ‘Coaster’ hiyo iliyokuwa imebeba wanafunzi 33 wa Shule ya Sekondari Endasaki waliokuwa wakielekea mkoani Arusha kwa ajili ya likizo baada ya kufunga Shule.
“Ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo katika eneo la Gajal Babati mkoani Manyara ambapo Coaster ilikuwa imebeba wanafunzi kutoka Hanang kuelekea mkoani Arusha na baada ya Kufika eneo hilo iligongana uso kwa uso na Scania,”Alisema Makarani.
Kufuatia ajali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ametoa pole kwa wanafunzi, walimu, wazazi na wananchi wote kufuatia ajali hiyo.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape nafuu na uponyaji wa haraka majeruhi wote,”Alisema Sendiga.