VYUO vikuu vya umma nchini Malawi vimeamuru wanafunzi wote wanaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) waondoke au watafute njia mbadala za kulipia ada kama wangependa kuendelea na masomo.

Hatua hiyo baada ya kusitishwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani kwa siku 90 ambako kulitangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump muda mfupi baada ya kuapishwa Januari 20.

Serikali ya Malawi inajitahidi kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wanaendelea na masomo yao, lakini vyuo vimeonya kuwa haviwezi kumudu gharama yao bila usaidizi.

Advertisement

Serikali ya Marekani kupitia USAID kwa muda mrefu imekuwa ikifadhili masomo ya maelfu ya wanafunzi kwenye vyuo vya umma vya Malawi, na sasa hatua hiyo imeathiri vyuo vingi kikiwemo Chuo cha Kilimo na Mali Asilia cha Lilongwe, Chuo cha Afya na Sayansi cha Kamuzi pamoja na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Malawi, MUST.

Mmoja wa wanafunzi wanaofadhiliwa na USAID, Patience Yamikani Chakwama anayesoma chuo kikuu cha MUST, amesema kuwa kusitishwa kwa misaada hiyo ya kigeni kulitangazwa kabla ya wanafunzi kupokea fedha za matumizi ya kila siku.

Chakwama amesema kuwa kando la kulipiwa ada ya shule pamoja na makazi, USAID pia ilikuwa ikitoa fedha za chakula na huduma za internet kwenye simu zao.

Utawala wa Trump unasema kuwa ulichukua hatua ya kusitisha msaada huo kwa siku 90 ili kuhakikisha kuwa fedha za USAID zinatumika kulingana na sera na maslahi ya Marekani. Sitisho hilo litaendelea hadi Aprili 20.