Dodoma. Wanafunzi 70,904 waliohitimu kidato cha nne mwaka jana wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi na vya elimu ya kati kwa mwaka 2018, huku wengine 21,808 waliokuwa na sifa za kuchaguliwa wakiachwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 16,2018 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –Tamisemi, Selemani Jafo amesema kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 31,884 na wavulana 39,020.
Amesema wanafunzi waliochaguliwa ni kati ya 92,712 wa shule na taasisi ya elimu ya watu wazima waliokuwa na sifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi na vyuo elimu ya kati.
“Utaratibu uliozingatiwa wa kuwachagua wanafunzi hao ni kuangalia alama za ufaulu wa daraja, daraja la ufaulu, ufaulu katika masomo ya sayansi, jinsia na nafasi zilizopo kwenye kozi na vyuo husika,” amesema Jafo.