WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kalangalala mkoani Geita wameandamana kwenda kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita kupinga kitendo kile kinachodaiwa kwamba mwanafunzi mwenzao kupigwa na mwalimu hadi kupoteza fahamu.

 

Mwanafunzi huyo, Jonathan Mkono anadaiwa alipigwa na Mwalimu waliyemtaja kwa jina moja la Lawi jana Agosti 30, 2018 kwa kosa la kuingia bwenini wakati vipindi vikiendelea darasani.

Mmoja wa wanafunzi, Aron Mathias amesema hali ya mwenzao aliyelazwa hospitali ya mkoa sio nzuri na kwamba hawezi kuzungumza, kukaa wala kusimama.

 

“Huyu (Jonathan) ni kiongozi, alikuwa anasimamia usafi alivyomaliza alirudi bwenini kuchukua vifaa lakini mwalimu Lawi alimwadhibu na sio kwa fimbo alimpiga makofi na marungu. Tulimpeleka hospitali akiwa mahututi tulipofika daktari alikataa kumpokea akishinikiza kupewa taarifa ya Polisi, tulivyoipata ndio wakaanza kumtibu majereha yake,” amesema Mwanafunzi huyo.