Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Shule za St Mary’s nchini zimeendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la saba kwa wanafunzi wake kupata wastani wa alama A kwenye matokeo yao.
Katika matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), wanafunzi wote wa shule hizo wamefaulu kwa alama A na wachache wamefaulu kwa wastani wa alama B.
Mkuu wa Shule ya Msingi, St. Mary’s Tabata Thomas Samson, alisema kuwa siri ya mafanikio ya shule hizo ni kuwa na walimu bora wanaotambua wajibu wao na kufanyakazi usiku na mchana kuhakikisha wanafunzi wanaelewa.
Alisema walimu wa shule hiyo wamefanyakazi kubwa ya kuwaandaa wanafunzi wake kwa kuwapa mitihani ya majaribio ya mara kwa mara hivyo wanafunzi wake kufaulu mitihani ya darsa la saba haijawashangaza.
Alisema walianza kuona dalili nzuri ya kufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo baada ya kuwa wanafanya vizuri zaidi kwenye mitihani ya majaribio ya kimkoa na kiwilaya ambapo nako walikuwa wanapata wastani wa alama A.
“Sisi tunachojua ni kufundisha, mzazi ukitukabidhi mtoto wako ukae ukijua kwamba umemleta sehemu sahihi kwasababu hata kama angekuwa ni slow leaner tutamfundisha mpaka atakwenda na kasi ya wenzake wenye matokeo mazuri,” amesema.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi St Mary’s Mbezi, Isaac Tamaro, alisema amefurahi kuona wanafunzi wake wamefaulu kwa kiwango cha juu na kuahidi kuwa hawatabweteka na matokeo hayo na badala yake wataongeza juhudi.
“Siri ya ufaulu huu ni moja tu kufundisha na kuwawekea wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza kwa kuwapa vitabu vya kutosha na walimu wenye kujua wajibu wao kwamba ni kufundisha tu na kwa kweli matokeo ya juhudi zetu tumeyaona nawapongeza walimu,” alisema
Isaac alisema wanafunzi wa shule za St Mary’s wamekuwa wakipewa motisha mbalimbali wanapofanya vizuri ikiwemo kupelekwa kwenye mbuga za wanyama kama Mikumi, Serengeti, Ngorongoro na Ruaha kwaajili ya kutalii na kujionea wanyama mbalimbali.
“Tunaushukuru uongozi wa shule za St Mary’s kwa kuendelea kujali walimu wake na kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kusomea binafsi naona hii imekuwa chachu ya mafanikio haya na tunawashukuru wazazi kwa kutuamini na sisi tunawaahidi kwamba tutaendelea kufanya vizuri zaidi,” alisema