Mimi sina shaka kuwa mtoto wangu angekuwa miongoni mwa wanafunzi watakaothibitika kuchoma moto shule, nyumbani angepaona pachungu.

Sina hakika kama sheria inamhukumu mzazi kwa kumcharaza mtoto wake viboko, lakini ningemcharaza kwanza viboko halafu ndiyo nijielimishe juu ya sheria iliyopo.

Tumetumbukia kwenye mjadala wa adhabu kali kwa watoto baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, kuripotiwa kuwachapa viboko wanafunzi wa kidato cha  tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja, iliyopo Wilaya ya Chunya, wanaodaiwa kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo baada ya kunyang’anywa simu zao za viganjani na walimu.

Wakati tukiwa wadogo nakumbuka kuwa wazazi hawakuvumilia utukutu kwa watoto wao, hata wa kinadharia tu. Mzazi mmoja alikuwa mtaalamu wa kutushushia makonzi tulipotenda makosa. Mwingine alikuwa hachelewi kushika fimbo na kutucharaza. Na utaratibu shuleni ulikuwa hivyo hivyo. Leo hii mmoja wa walimu ninayemkumbuka sana kwa viboko nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Isike ya mjini Tabora mwaka 1973 ni Mwalimu Luleka. Wengine siwakumbuki majina.

Tungeishi kwenye jamii zinazoitwa zimeendelea, leo hii kama ningefika kuonana na mtaalamu wa saikolojia na kuonekana kuwa na tatizo la kisaikolojia ningeambiwa limesababishwa na athari za ubongo kuhama kwa sababu ya makonzi niliyoyapata utotoni.

Hata hivyo, siamini kama adhabu kali ni suluhisho la kumaliza utukutu, au kama ni adhabu inayopaswa kutolewa kila mara. Naamini kuwa kila adhabu inapaswa kupimwa ikilinganishwa na kosa lililofanyika.

Nimelazimika kujipima mwenyewe iwapo nilitumia adhabu kali dhidi ya watoto wangu walipokuwa wadogo. Kwa kiasi kubwa sikufanya hivyo, na naamini sikujenga uhusiano wa woga kati yangu na wao.

Sitapinga kuwa zipo athari mbaya ambazo zinaweza kujitokeza kwa sababu ya kutumia adhabu kali dhidi ya watoto kwa muda mrefu. Kutumia adhabu kali kila wakati hakumsaidii mtoto kujifunza. Zaidi, kutamfanya kuwa mwoga tu wa kuepuka adhabu.

Lakini tukubali wapo wengi ambao utotoni walinyooshwa kidogo kwa adhabu kali na kujirekebisha kuwa watu wazima na raia wa kutegemewa na familia zao na jamii. Ni kwa sababu hii siamini kama adhabu kali dhidi ya mtoto haina manufaa yoyote.

Kwa bahati mbaya kutokana na tukio la Chunya mjadala umehama kutoka kuwa tatizo la kuporomoka kwa uadilifu ndani ya jamii yetu na kugeuka kuwa uhalali wa mkuu wa mkoa kucharaza watoto viboko. Vyote vingejadiliwa kwa wakati wake bila kutumia nguvu nyingi kuvutia upande mmoja.

Kisichokuwa na ubishi wowote ni kuwa taratibu zinaruhusu wanafunzi waliyofanya makosa ya aina fulani kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko. Kosa linapothibitishwa, na linapaswa kuwa kosa la jinai au linalodhalilisha taswira ya shule, mwanafunzi anaadhibiwa na mwalimu mkuu au mwalimu aliyepewa mamlaka na mwalimu mkuu. Aidha, daftari maalumu la adhabu linapaswa kutunzwa na kuwekwa sahihi na mwalimu mkuu inapotolewa adhabu.

Viboko alivyoshusha mkuu wa mkoa vingeshushwa na mwalimu aliyepewa dhamana, mjadala huu ungekuwa mfupi zaidi.

Lakini hakuna ulazima wa kuufupisha. Isipokuwa kama ukiukwaji wa taratibu unapewa uzito, basi kuna ulazima wa kuweka mezani mjadala mpana zaidi na kupima: tuhoji tu utaratibu wa kuchapwa viboko wanafunzi, au tupime pia tatizo la kulea vijana ambao wanaonekana kutumbukia kwenye tabia ambazo zinahatarisha ustawi wa taifa letu?

Mjadala ukianzia hapo, basi tutaanza kujadili moto unaozuka, badala ya kujadili tu moshi uliyojitokeza. Vyote vina athari, lakini suluhu ya kudumu inahitaji tutafute dawa ya kuzima moto kwanza. Ama sivyo tunatuma ujumbe kwa watoto kuwa wakinyang’anywa simu shuleni na kuamua kuchoma moto shule, basi hilo siyo tatizo linalozidi la kuwacharaza viboko bila kufuata utaratibu.

Ninahofu kwamba jamii inaharibikiwa kwa kukosa vijana ambao wanaandaliwa kushika jukumu la uongozi katika miaka ijayo. Inawezekana tumeanza kuharibikiwa bila kutambua kuwa hilo linatokea. Sina hakika kama upo mfano mzuri wa kuharibikiwa zaidi ya kitendo cha mwanafunzi kuamua kuchoma moto mabweni kwa sababu tu kanyang’anywa simu na walimu wake.

Sasa hivi tungefanya mjadala juu ya tumefikiaje hatua ya kuwapo vijana wa aina hii miongoni mwetu. Na hatuwezi kukamilisha mjadala au kupata suluhisho bila kuhoji pia kama wazazi wao wanaweza kuwa wamechangia kuibuka kwa tabia hizi.

Aidha, upo uwezekano kuwa umiliki wa simu hizo za viganjani na matumizi yake ndiyo chanzo cha kuwaingiza vijana hao kwenye tuhuma zinazowakabili. Kama kuna utetezi ambao unaweza kutolewa kwao ni kukubali kuwa simu hizi za viganja zinawajengea uraibu wanaozitumia kiasi kwamba wanapozikosa kwa muda wanakumbwa na matatizo ya kisaikolojia.

Kwa hiyo tuwe tayari kupokea ukweli kuwa kitendo cha kuchoma moto mabweni kinaweza kuwa kitendo cha mgonjwa wa akili badala ya mtuhumiwa anayetenda kosa akiwa na akili zake timamu. Na ikiwa huu ndiyo ukweli mkuu wa mkoa ataendelea kulaumiwa kwa kuadhibu wanafunzi ambao wanahitaji tiba.

Kwa vyovyote vile, tusiurahisishe huu mjadala kuwa ni suala la ukiukwaji wa taratibu peke yake. Kama tunataka kuwa wakweli tuweke mezani ajenda pana zaidi: kuporomoka kwa maadili miongoni mwa vijana wetu na athari zake kwa mustakabali wa nchi yetu.

Barua pepe: [email protected]