Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Njombe
Mwanaunzi wa darasa la sita Marko Sanga (12), amekutwa amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia mnyororo wa baiskeli kwa kile kinachodaiwa kuwa kutokana na radio, nguo za shule pamoja na madaftari kuungua kwa shoti ya umeme.
Kwa mujibu wa mama yake mkubwa na marehemu huyo Obina Mbilinyi amesema kuwa mtoto huyo walikuwanaye shambani na jioni ilipofika walimwambia atangulie nyumbani ili akafungue ng’ombe malishoni na kuwarudisha nyumbani ambapo alipofika nyumbani alikuta vitu hivyo vimeungua kwa shoti ya umeme iliyosabishwa na radio ambayo marehemu alikuwa ameichomeka kwenye umeme.
Amesema marehemu alifungua ng’ombe kama alivyoagizwa na kisha kujinyonga na waliporudi nyumbani walimtafuta na kumkuta marehemu akiwa amekufa huku akining’inia kwenye mnyororo wa baiskeli.
“Tunahisi kuungua kwa radio na baadhi ya vitu vyake inaweza kuwa ni sababu ya kujinyonga kwake maana mpaka tunaagana shambani alikuwa katika hali ya kawaida”.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issah amethibisha kutokea kwa tukio hilo liliotokea jana katika Kijiji cha Maleutsi wilayani Makete mkoani Njombe ambapo mwanafunzi huyo alikuwa amekufa huku akining’inia juu ya mti baada ya kufunga mnyororo wa baiskeli.
Kamanda Issa amewataka wazazi kuishi vizuri na watoto wao kwani inawezekana mtoto huyo alikuwa anahofia kuadhibiwa kwa kile kilichotokea ndipo akaona ni heri kufa.
“Wazazi kuweni makini na watoto msipende kuwaadhibu kila wanapokosea kwani watoto wa siku hizi ni kama yai, ukiwa unamuadhibu mara kwa mara matokeo yake huwa kama haya maana wanajawa na hofu” amesema kamanda.