Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imetoa elimu kwa wamiliki wa Vyombo vya moto ikiwemo daladala na bajaji juu ya umuhimu wa kuwa na ushirika wao wa pamoja ama kuwa na kampuni ambayo itakua inatetea maslahi yao.
Meneja wa Leseni wa mamlaka hiyo Ngowi wakati akizungumza na wamiliki wa daladala na Bajaji Jijini Arusha leo Januari 29, 2024 amesema kuna umuhimu wa wamiliki hao kuanzisha ushirika wao ama kuwa na kampuni ambayo lengo lake litakua ni kuboresha huduma ya usafirishaji lakini pia wao wenyewe kujiimarisha kiuchumi.
Ngowi ameendelea kubainisha kuwa washiriki katika semina hiyo walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo faida za kuwa na umoja huo ambao kama ukifanikiwa kuanzishwa utasaidia kuwa na mfumo wa kisasa ukilinganisha na mfumo wa sasa ambao unatumika usiokidhi viwango.
Halikadhalika amesema kuwa baada ya Kuanzishwa kwa Chama hicho cha ushirika huduma za usafirishaji katika Jiji hilo zitaimairika na kuboreka kwa kiasi kikubwa.
Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Jiji la Arusha Bwana Maulid Athuman amesema kuwa baada ya kupata elimu hiyo amebaini kuwa watapata faida kubwa ambapo itawafanya wamiliki wote wa daladala kuwa pamoja na kuomba Mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wamiliki wote ili wapate uelewa wa pamoja.
Kwa upande wa Bwana Musa Chuga ambaye ni Dereva na Mmiliki wa daladala amesema wamejifunza mambo mengi katika semina hiyo ikiwemo umuhimu wa kuwa na kampuni itakayowasimamia ama Chama cha Ushirika ambazo zitasaidia kutatua kero au malumbano ambayo yamekua yakijitokeza baina yao na Latra na Jeshi la Polisi.
Aidha ametoa wito kwa Mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa makundi yote kwakua kwa namna walivyofundishwa faida za kuwa mfumo wa kisasa wa uendeshaji kuna haja ya kufanya mabadiliko kuondokana na mfumo wa zamani wa uendeshaji.