Na Mwandishi Wetu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapandisha kizimbani wafanyabiashara watatu wanaodaiwa ni wamiliki wa jengo lililoporoka Kariakoo, wakikabiliwa na mashitaka 31 ya kuua bila kukusudia. Washitakiwa hao ni mkazi wa Mbezi Beach na mfanyabiashara, Leondela Mdete (49), mkazi wa Kariakoo Mwarabu Zenabu Islam (61) na mfanyabiashara na mkazi wa Ilala, Ashour Awadh Ashour (38).

Walisomewa mashitaka yao jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Lema akishirikiana na Grace Mwanga wakili wa serikali Mwandamizi na wakili wa serikali, Erick Kamala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini wakati kesi hiyo ilipoletwa (mpya).

Wakili Kamala alidai washitakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kuua bila kukusudia. Alidai, Novemba16, mwaka huu maeneo ya Mchikichi na Kongo, Kariakoo Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam isivyo halali washitakiwa kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.

Waliopoteza maisha ni Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu, Rashid Yusuph na wengine 21.

Baada ya kuwasomea mashitaka yao wakili Kamala alidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea. Hakimu Mhini alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Aliwasomea washitakiwa masharti ya dhamana kuwa ni kuwa na wadhamini wawili na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kila mshitakiwa, awe na kitambulisho cha Nida na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja. Washitakiwa wawili walishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Desemba 12, mwaka huu.