Wakati naandika haya, huko Marekani kampeni ya kugombea urais imepamba moto. Hakuna anayeweza kutabiri kwa hakika ni nani atakayeshinda kati ya wagombea wakuu wawili- Donald Trump na Hillary Clinton. Inawezekana baada ya uchaguzi kufanyika Novemba 8 matokeo yakajulikana.
Kwa muda huu miye nisingependa kujifanya Sheikh Yahya Hussein. Ila tu ningependa kutoa maoni kuhusu wagombea wote wawili ili tujiweke tayari. Kwa maneno mengine, ulimwengu utarajie nini kutoka kwa yeyote atakayekuwa rais wa Marekani.
Vyombo vya habari huko Marekani kwa idadi kubwa vinapenda Clinton ashinde. Nchini Marekani asilimia 96 ya vyombo vya habari vinamilikiwa na kampuni sita kubwa. Na vyombo vingi vimekuwa vikiegemea upande wa Clinton.
Pia wataalamu wa uchumi zaidi ya 670 wameandika risala ya kuwataka wananchi wamchague Clinton, kwa vile wanaona Trump akishika madaraka, basi uchumi wa Marekani utatetereka. Hawa wanaongozwa na Profesa Oliver Hart ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel (2016) akiwa mwanauchumi.
Trump ni bilionea asiyekuwa na uzoefu wa siasa. Yeye si mwanasiasa. Jambo hili ndilo linampatia kura, kwa sababu wananchi wengi wamepoteza imani na wanasiasa ambao wanatoa ahadi ambazo hawazitimizi.
Kaulimbiu yake ni “Kuirudishia Marekani Hadhi yake Kama Taifa Kuu.” Anasema kwa sasa nchi hiyo imepoteza hadhi kwa vile wawekezaji wa Marekani wamekuwa wakihamisha viwanda vyao na kuvipeleka China, Mexico na kwingineko. Huko bidhaa huzalishwa na kisha kuuzwa nchini Marekani.
Anasema: “Nchi yetu inatumiwa kama soko, wakati uzalishaji unafanyika nchi za nje kwa kutumia mitaji yetu”. Ahadi yake ni kuwa atapunguza kodi kwa wawekezaji ili warejeshe Marekani viwanda vyao. Anasema atapunguza kodi kutoka asilimia 35 hadi 15 ili kuwavutia.
Kwa maelfu ya wafanyakazi waliopoteza ajira zao, jambo hili linawaingia akilini na ndio maana wanamuunga mkono Trump. Lakini hata kama atawapunguzia kodi matajiri, hakuna uhakika kuwa watahama kutoka China na Mexico. Ukweli ni kuwa huu utandawazi unawatajirisha wawekezaji. Huko China mishahara ni midogo wakati bidhaa huziuza kwa bei kubwa nchini Marekani.
Watatokaje Asia ambako mshahara ni dola kama tatu kwa siku na kurudi Marekani ambako mshahara ni dola 80 kwa siku?Bepari katika biashara yake hatumii uzalendo, anasukumwa na tamaa ya faida ndio maana hata Trump mwenyewe anafanya vivyo hivyo.
Licha ya kujifanya kuwa bepari wa kizalendo, yeye mwenyewe amefunga viwanda vyake nchini Marekani na kuvihamisha kusini kwenye mishahara midogo. Baada ya muda akavirudisha Michigan kwa masharti kuwa wafanyakazi watakubali kupokea mishahara midogo.
Ahadi ya Trump ya kuzuia kampuni kuhamia Asia na kuifanya Marekani iwe nchi ya kibabe inawavutia maelfu ya wafanyakazi waliokosa ajira. Pia ahadi yake ya kuzuia Waislamu kuingia nchini na kuwatimua wahamiaji kutoka Mexico na kujenga ukuta katika mipaka ya nchi inawavutia Wazungu wenye mawazo ya kikaburu.
Hawa wanaamini kuwa “wageni” ndio wanaosababisha uhalifu, ubakaji na ugaidi nchini. Wanaamini kuwa ni hawa ndio wanaosababisha wao kukosa ajira wakati nchi inakabiliwa na “baa” la kutawaliwa na raia wasio weupe. Trump anachukia wageni wakati baba yake alihamia Marekani kutoka Ujerumani.
Trump aliingia katika biashara mwaka 1973 wakati alipojenga maghorofa ya kupangisha. Wakati huo sera yake ilikuwa kutowapangisha watu weusi. Mara mbili alifunguliwa mashitaka kwa kosa la ubaguzi wa rangi kutokana na sera hii ya kuwabagua wapangaji weusi.
Yeye anaahidi kuwa siku ya kwanza tu atakapoingia White House (Ikulu) atawatimua wageni “haramu” wote. Sasa nchini Marekani kuna wafanyakazi milioni 11 wasio na kibali. Hata hivyo wameishi humo kwa miaka mingi na ndio msingi wa uchumi.
Wao ndio wanaochimba mitaro, wanaobeba zege, wanaolima mashamba na wanaovuna mboga na matunda na kuyasambaza nchini. Hakuna anayeamini kuwa inawezekana kuwatimua kama anavyoahidi Trump. Si ajabu hata baadhi ya viongozi wa chama chake cha Republican wametangaza kuwa hawatampigia kura.
Tukiangalia upande wa Hillary Clinton, yeye ameahidi kujenga uchumi utakaonufaisha matabaka yote. Kwa maana hiyo ataongeza mshahara kima cha chini pamoja na kutoa fursa sawa kwa wanawake. Atajenga mazingira bora kwa wafanyabiashara wa kati ili kuzalisha ajira. Kampuni kubwa nazo zitahimizwa kuongeza mapato ili waajiriwa wao wote wafaidike badala ya mabosi peke yao.
Chini ya uongozi wake, Clinton ameahidi kuunda sheria ya mafao ya wafanyakazi kama vile likizo ya kila mwaka, matibabu bure kwa familia, posho ya watoto na mikopo nafuu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Hizo ni ahadi ambazo zinaweza zisitekelezwe. Kwani hata Rais Obama ametoa ahadi ambazo hajazitekeleza. Kwa mfano, amesema ataifunga jela ya Guantanamo na kuwaachia wafungwa ambao hawajafikishwa mahakamani. Mpaka leo jela inaendelea kuwaweka wafungwa wasio na hatia.
Lakini tukiachia ahadi za Clinton, kuna mzigo mkubwa ambao anaubeba na unamfanya alaumiwe na hata kukosa kura. Shirika la Upepelezi wa Makosa ya Jinai (FBI) limetangaza kuwa linafanya uchunguzi wa maelfu ya barua pepe za siri ambazo amekuwa akizipata kupitia anwani yake binafsi badala ya anwani rasmi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Akiwa Waziri, mawasiliano yake rasmi na ya siri yalitakiwa yatunzwe kiofisi. Badala yake inasemekana yeye aliyafuta. FBI inasema inawezekana kwa kufanya hivyo, Clinton amevunja sheria. Sasa hizi ni shutuma ambazo hazijathibitishwa, lakini Trump amedandia na kusema Clinton hafai kuwa rais wa nchi.
Clinton kwa upande wake ameitaka FBI iweke bayana barua pepe hizo ili ithibitike kama kweli amevunja sheria, kitu ambacho yeye anakanusha. Muhimu zaidi ni kujiuliza, iweje FBI itangaze uchunguzi huu siku chache kabla ya uchaguzi? Kitendawili.
Tukiachana na kadhia ya barua pepe, Clinton pia anashutumiwa amekuwa akidhaminiwa na kampuni kubwa. Kwa mfano benki maarufu ya Goldman Sachs imemlipa dola 675,000 kutokana na mada tatu alizoziwasilisha. Katika hotuba hizo aliainisha hatua atakazozichukua ili kuzisaidia kampuni za kimataifa. Hivyo fedha alizolipwa ni “mkopo” ambao itabidi aulipe atakapoingia White House.
Trump naye anakabiliwa na shutuma za kuwadhalilisha kijinsia wanawake. Kanda imesambazwa ikiwa na matamshi yake mwenyewe akijigamba kuwa ana uwezo wa kufanya hivyo. Yeye amekubali kutamka maneno hayo, lakini anasema hakuwahi kufanya kitendo.
Lakini tayari wanawake kadha wamejitokeza hadharani wakidai kuwa walidhalilishwa kijinsia na Trump. Clinton naye ametumia hili kumshambulia mpinzani wake.
Katika kampeni wakati wote kumekuwako mabishano kuhusu barua pepe au wanawake. Ni nadra kusikia mahasimu hawa wakitangaza sera zao za mambo ya nje.
Hata hivyo, Trump amewahi kutamka kuwa Shirika la Kujihami (NATO) limepitwa na wakati hasa baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti (USSR). Yeye anaamini kuwa ni vizuri Marekani ikawa na uhusiano mzuri na Urusi badala ya kuendeleza vita baridi.
Pia anasema si jukumu la Marekani kulinda usalama wa mataifa ya kigeni. Ni vizuri kila nchi ikajilinda yenyewe. Kwa nchi ya kibeberu kama Marekani yenye vituo vya kijeshi zaidi ya 100 duniani kote hili jambo muhimu sana. Si vizuri Marekani ikajiteua kuwa mlinzi wa dunia.
Clinton anatofautiana na Trump. Amewahi kumshutumu Rais Putin wa Urusi kwa kumfananisha na Hitler. Katika hotuba yake ya Goldman Sachs amesema Marekani inapaswa kuizingira China kwa vituo vya kijeshi kama ilivyoizingira Urusi. Kwa maneno mengine Clinton ana nia ya kuendeleza ubeberu.
Kuhusu hatua za kuchukua nchini Syria mahasimu hawa wawili wanakubaliana, kwa vile wanataka majeshi ya Marekani yaingie Syria na kuidhibiti nchi hiyo.
Lakini kuna ripoti iliyotolewa na Jenerali Joseph Dunford, Mkuu wa Majeshi ya Marekani. Yeye aliwaambia wabunge kuwa kuingiza majeshi ya Marekani huko Syria ni kuanzisha vita dhidi ya Syria na Urusi. Ni kuanzisha Vita Kuu ya Tatu.
Bila shaka Jenerali huyo anajua asemalo, kwani baada ya Marekani kuikalia kijeshi Iraki gharama yake kwa Marekani ni dola trilioni sita zilizotumika pamoja na maelfu ya askari wa Marekani kupoteza maisha na wengi kupoteza viungo. Wairaki zaidi ya milioni moja wameuliwa na mamilioni kuwa wakimbizi.
Ukichanganya na uvamizi wa Syria na Libya hali inazidi kuwa mbaya zaidi. Na athari zake zinaonekana hadi nchi za magharibi ambako maelfu ya wakimbizi wamemiminika. Katika hali kama hii Clinton na Trump wanataka waendeleze vita ya Mashariki ya Kati.
Ndio maana Wamarekani wengi hawaoni tofauti baina ya Donald Trump na Hillary Clinton. Yeyote atakayeshinda, wao wanaona kuwa uchumi wa nchi yao utaendelea kudhibitiwa na matajiri (asilimia moja).
Haya yalisemwa hata na Rais mstaafu Jimmy Carter. Yeye alitamka kuwa: “Marekani sasa ni nchi inayotawaliwa na tabaka la mabilionea ambao wanatumia fedha zao kuwanunua wanasiasa”.