Taifa linahitaji fedha. Haya mambo makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano yatawezekana tu endapo ari ya kubuni, kuendeleza na kusimamia vyanzo vya mapato ya ndani vitatambuliwa na kulindwa kwa nguvu zote.
Kama ambavyo Rais John Magufuli amekuwa akisema mara kwa mara, Tanzania ni tajiri kiasi kwamba tukijipanga vema tunaweza kujitosheleza kwa mapato yetu. Dalili zimeanza kuonekana. Tunafanya mambo makubwa kwa fedha zetu wenyewe.
Haya mambo yatanoga endapo tutakuwa wakweli na kuisaidia serikali katika kuhakikisha kuwa wigo wa ukusanyaji mapato unapanuliwa.
Tunayo sekta ndogo ya utalii wa picha na uwindaji wa kitalii. Aina hizi mbili za utalii ni nzuri kwa mapato ya nchi, lakini ni kweli kwamba fedha nyingi ziko kwenye uwindaji wa kitalii.
Kwa bahati mbaya Wizara ya Maliasili na Utalii imekubali kuyumbishwa. Mkwamo wa awali umesababishwa na muda wa umiliki wa vitalu. Waziri, ama kwa kujua, au kwa kutokujua ameendelea kuiyumbisha sekta hii. Alikwisha kutangaza kufuta muda wa umiliki wa vitalu, tukamkosoa. Akatusikiliza, akaongeza miaka miwili. Juzi, ameongeza mwaka mwingine mmoja kimya kimya. Asione aibu. Akubali tu kuwa uamuzi wake ulikuwa mbaya na umeliumiza taifa. Vitalu karibia 90 vimerudishwa.
Uwindaji wa kitalii ni biashara ngumu inayohitaji uwekezaji wa hali ya juu. Ni biashara inayohitaji muda kustawi. Si biashara ya leo leo. Wizara kukosa msimamo kumeiyumbisha sekta hii na kwa kweli inachungulia kaburi.
Kumekuwapo wazo la vitalu vya uwindaji kupigwa mnada. Huu ni mpango mbaya. Hauzingatii uhifadhi. Mtikisiko ulioletwa na wizara umesababisha vitalu hivyo (90) virejeshwe serikalini. Kama ni majaribio ya mnada, kwanini wizara isianze na hivi? Kwenye makala zijazo nitaeleza kwa urefu athari za mpango huu.
Sasa kuna mpango mwingine unaopikwa ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ni mpango hatari. Kuna kampuni za utalii wa picha za raia wa Marekani na Afrika Kusini – zinataka kufutwa kwa uwindaji wa kitalii!
Zinataka maeneo yote ambayo sasa kuna uwindaji wa kitalii yawe ya utalii wa picha! Hawa Wamarekani wameshupalia vitalu kiasi kwamba walikwisha kutushtaki katika Seneti yao na kwa Rais Barack Obama wakitaka maeneo hayo yawe yao. Tanzania si koloni la Marekani. Hii ni nchi huru. Hawajakoma, wanaendelea.
Kampuni hizi zinataka kuchukua eneo lote la Maswa, Lake Natron na Ngorongoro. Zimehakikisha zinawatumia mawakala wao wapya na wa zamani kushawishi Wizara ya Maliasili na Utalii iingie mkenge huu. Wamarekani hawa hawa wameshindwa kulipa maduhuli ya serikali na sasa wanadaiwa mabilioni ya shilingi.
Kampuni ya Afrika Kusini inayotaka imiliki eneo la Ngorongoro hailipi chochote serikalini, isipokuwa inakilipa kijiji Sh milioni 200 kwa mwaka! Huu ni wizi ambao sasa wanataka waupanue zaidi. Leo wanataka maeneo yote haya makubwa yawe yao! Tusikubali.
Bahati mbaya tunao viongozi serikalini – ngazi ya mkoa na wizara wanaohaha ili Wamarekani na hawa Waafrika Kusini wapate vitalu vya uwindaji wa picha. Hawataki maeneo ya hifadhi za taifa kwa sababu huko wanabanwa walipe maduhuhi. Wakiwa nje wanajua hawatalipa kodi.
Maeneo ambayo ni vitalu vya uwindaji kwa mwaka mzima yanalindwa na waliokodishwa; na kwa sababu hiyo wamekuwa wakikabiliana vilivyo na ujangili. Kazi hiyo haifanywi kwa kiwango kama hicho na kampuni za utalii wa picha.
Uwindaji ni uhifadhi katika kulinda ikolojia ya maeneo yaliyohifadhiwa. Hili linapata nguvu zaidi kwa kuwa uwindaji unafanywa nje ya hifadhi za taifa.
Kisheria si wanyama wote wanaowindwa. Hapa walengwa ni wanyama madume waliozeeka. Uwindaji ni ulinzi wa kiikolojia, kwani kisayansi kufanya hivyo husaidia kupunguza wanyama ambao ni wazee au wale wanaoelekea kuathiri jamii nyingine ya wanyama.
Uwindaji upo duniani kote, na kama haufanywi na watu binafsi, basi hufanywa na serikali yenyewe. Tangu zamani yapo maduka ya nyama ya pori iliyotokana na kupunguza aina fulani ya wanyama waliozidi katika eneo fulani.
Bahati mbaya uwindaji wa kitalii unachukuliwa kama ujangili. Huu ni upotoshaji mkubwa. Uwindaji wa kitalii si ujangili. Hakuna mnyama anayewindwa bila kuwapo ofisa wanyamapori. Ada ya kitalu cha uwindaji daraja la kwanza ni dola 60,000 za Marekani kwa mwaka. Mapato haya ni mbali kabisa na bei ya nyara. Hizi ni fedha nyingi. Zinaweza kuongezeka endapo serikali itaamua.
Kampuni za uwindaji zinatakiwa ziwe na askari wa doria kulinda kitalu kwa kipindi chote cha mwaka. Kampuni moja inaweza kutumia Sh milioni 50 kwa ajili ya doria tu kwa mwaka. Hizi ni gharama kubwa ambazo serikali pekee haiwezi kuzimudu.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inasimamia eneo la kilomita za mraba takriban 170,000. Humo kuna mapori ya akiba, hifadhi za jamii (WMA) na mapori tengefu. TAWA pekee haiwezi kusimamia maeneo haya. Haina rasilimali. Kwa hiyo wadau, hasa kampuni za uwindaji wa kitalii ni muhimu kwenye kazi hii.
Napendekeza, badala ya kufuta uwindaji wa kitalii, Wizara ya Maliasili na Utalii iongeze ada ya nyara na iongeze ada za vitalu. Kama kitalu daraja la kwanza sasa ni dola 60,000; kipandishwe hadi dola 150,000 za Marekani. Anayekimiliki kama anaweza kulipa aendelee, kama hawezi apishe wanaoweza. Kinachotakiwa wabanwe tu, watalipa.
Hatua hiyo itasaidia kuimarisha sekta hii na kuifanya ichangie mapato makubwa. Rais anahitaji hizi fedha ili zitumike kuijenga nchi yetu. Uwindaji wa kitalii ni uhifadhi na ni chanzo kizuri sana cha mapato ya nchi.