Serikali imeamua kuwapanga upya wananchi wa vijiji viwili vya Mbagala Mbuyuni na Marumba wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara ili kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na kuleta usalama kwenye maeneo hayo.

Akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Wanika kata ya Mkonona tarafa ya Nanyumbu wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara tarehe 28 Desemba 2022 wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta, Waziri wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, kitakachofanyika kila kijiji kitapewa utaratibu utakaosimamiwa na mkuu wa mkoa atakayewapanga wananchi wake na kuyaacha maeneo ambayo si salama kukaliwa na wananchi huku akisisitiza hakuna haki ya mtu itakayopotea.

“Mhe Rais anatambua tunayo shule yenye madarasa matatu, na hapa tulipo kuna kaya 94 ambazo ziko hapa na ukienda kitongoji jirani ziko kaya 134 hivyo serikali inajua idadi ya watu kwenye maeneo hayo na mahitaji yao” alisema Dkt Mabula.

Aliongeza kuwa, timu ya mawaziri nane wa wizara za kisekta inayozunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi
sambamba na kuwafahamisha dhamira njema ya serikali yao katika kuhakikisha inalinda usalama wao pamoja na usalama
wa mipaka ya nchi

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri nane wa wizara za kisekta, serikali itafuata
utaratibu mzuri wa kuwapanga wananchi wa maeneo hayo kwenye vijiji husika ili kila mtu aweze kuendelea na maisha yake


bila tatizo kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan amejibu hoja ya changamoto
iinayowafanya wananchi kuhama hama maeneo hayo.


“Kama Mheshimiwa Rais ametoa kinachostahili kipi ambacho kitakuwa kimebaki, ecolojia tunataka kuiona inavyokwenda
ninyi wote ni mashahidi ukipita huo kina cha maji ki azidi kupungua kuna mahali unaona mchanga ni kwa sababu shughuli
za kibinadamu zimeenda katika vyanzo vya maji,” alisema Dkt.Mabula.


Awali wananchi wa Nanyumbu waliieleza Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta kuwa, wao wamepokea maelezo
na kusubiri kitakachofanyika.

Mkazi wa Kitongoji cha Wanika, Othman Said maarufu Gonga alibainisha kuwa, wao wanaishi kwenye vijiji hivyo kama
nyumbani lakini pia kama walinzi na kueleza kuwa huko nyuma waliwahi kuwakamata watu waliodhaniwa kuwa ni
alshabab.


Aidha, waliomba serikali kuchukua tahadhari wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri na kushauri muda
kuzingatiwa kwa kuwa hiki ni kipindi cha kilimo na watu wanaanza kwenda mashambani.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Bi. Mariamu Chaurembo aliwaambia wananchi wa wilaya yake kuwa, uamuzi wa serikali
kupanga upya vijiji hivyo utatoa nafasi kwao kuanza kufanya shughuli za uchumi maeneo sahihi na kubainisha kuwa, vijiji
vitatengenezewa matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kubainisha maeneo ya kilimo na ufugaji.

Awali akizungumza na uongozi wa mkoa wa Mtwara Dkt.Mabula alisema mkoa huo unahusisha migogoro ya matumizi ya
ardhi katika vijiji na mitaa 12 iliyoainishwa sehemu kuu tatu kulingana na aina ya mgogoro.


Aliitaja sehemu ya kwanza kuwa vijiji na mitaa 10 ambayo wananchi wake wataondolewa kwenye eneo la hifadhi na
shamba la MATI na TARI huku sehemu ya pili ikihusisha kijiji kimoja ambacho mgogoro wake wa mipaka na hifadhi
umerejewa kwa njia shirikishi kati ya halmashauri ya wilaya ya Masasi, Halmashauri ya kijiji cha Chingulungulu na
Wataalamu wa Pori la Msanjesi lilipo chini ya TAWA.


Dkt. Mabula alisema, sehemu ya tatu inahusu kuviondoa vitongoji 4 vilivyoingia hifadhiya Msitu wa Mbagala na kuvimegea maeneo kutoka hifadhini karibu na vijiji mama huku sehemu ya nne ikihusisha kumega eneo la hifadhi ya Ndechela na kuwaoa wananchi wa kijjji cha Nakopi ambapo halmashauri ya Nanyumbu kwa kushirikiana na TFS pamoja na serikali ya kijjji wamelitekeleza.