Watuhumiwa 20 wa makosa ya kuingilia mifumo ya mawasiliano wamefikishwa Mahakamani jana jioni katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha huku wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi yanayojumuisha makosa 120 ikiwemo Utakatishaji wa Fedha.

Akisoma mashtaka katika kesi namba 30977 ya mwaka 2024, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Regina Oiye, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nurat Manja akisaidiana na Wakili wa Serikali, Shundai Michael alisema watuhumiwa 11 wanashtakiwa kwa makosa 75.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Onesmus Wambua Kamolla, Charles Kavoi King wote raia wa Kenya, Noel Morijoi, Jofrey Samson Mbise, Hussein Abdillah Majid, Philimon Melekwa, Ibrahim Ramadhani Mkunda, Daudi Nathanael, Alfayo Eliahu Mollel, Reginald Joshua Tartoo na Josephat Peter Mrisho.

Baadhi ya makosa waliyoshtakiwa nayo ni pamoja na kutakatisha fedha, Kuendesha genge la uhalifu na kusabanisha hasara ya 40,319,100/=, Kuingiza Nchini vifaa vya kielekroniki kinyume na Sheria bila leseni, Matumizi mabaya ya taarifa za mteja.

Nurat aliieleza mahakama hiyo kuwa Washtakiwa wengine 10 mmoja kutoka kundi la kwanza ambaye amejumuishwa katika kundi hili wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kesi namba 30975 ya mwaka 2024 ambayo inajumuisha makosa 120.

Mwendesha Mashtaka huyo aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Derick Odira Onyango, Walater Okoth Jabuya wote raia wa Kenya, Noel Morijoi Mollel, Julius Msuya Mgema, Calvin Evariste Maganga, Sharif Juma Athuman, Julius Johanes Kweyemba, Jackson Joseph Mollel, Ignas Henericko Leverian na Wilson Emanuel Malolela.

Baadhi ya Makosa waliyoshtakiwa nayo ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu na kuisababishia Serikali hasara ya 150,740,460/=, Kuwa na nia ya kuzuia viwango vya malipo kwa simu za kimataifa.

Aliendelea kutaja makosa mengine yanayowakabili kuwa ni Kutakatisha fedha Tshs 150,740,460/=, kutumia laini ya simu ya mtu mwingine, kutumia vifaa ambavyo havijaidhinishwa na Mamlaka yaani Sim Box.

Kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka, hakimu Regina aliwaeleza hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Pia shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika shauri hilo washtakiwa 12 kati ya 20 Hakimu alieleza kuwa dhamana zao zipo wazi ikiwa watatimiza vigezo vya dhamana ambapo kati yao 07 walidhaminiwa na wengine 05 walishindwa kutimiza vigezo vya dhamana. Washtakiwa wengine 08 walishtakiwa kwa makosa ya Kutakatisha fedha kosa ambalo halina dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14, 2024 saa nne asubuhi ambapo watuhumiwa 13 walirudishwa rumande huku 07 wakipewa dhamana.