Baadhi ya wateule wa Baraza la Mawaziri la Rais mteule wa Marekani Donald Trump wanakabiliwa na uchunguzi mkali, ikiwa ni pamoja na madai ya utovu wa nidhamu.

Pete Hegseth aliyeteuliwa kuwa waziri wa ulinzi anakanusha madai ya unyanyasaji wa kijinsia na huku mwanasheria mkuu mtarajiwa Matt Gaetz akikabiliwa na uchunguzi wa maadili.

Robert F Kennedy Jr, aliyeteuliwa na Trump kuwa waziri wa afya anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusiana na msimamo wake juu ya chanjo.

Trump atahitaji Baraza la Seneti la Marekani kuwaidhinisha baraza lake la mawaziri atakapoingia madarakani mwezi Januari mwakani.

Baraza hilo litadhibitiwa na Warepublican wenzake, wateule wake katika baraza la mawaziri watakabiliwa na maswali magumu wakati wa vikao vya pande mbili.