Wanachama zaidi ya 300 wa Wazalendo Saccos wanakusudia kuwafikisha mahakamani viongozi wa chama hicho, uongozi wa chuo na taasisi za fedha zilizotoa mikopo kwa tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 6.
Wakizungumza na JAMHURI, mwishoni mwa wiki iliyopita, wanachama hao wanasema kwamba hawawezi kuvumilia tuhuma hizo ambazo zinaonesha wazi mkakati wa wizi huo ulifanywa makusudi kwa lengo la kukitia hasara chama hicho.
Wanasema miamala ya fedha isiyozingatia utaratibu iliyofanywa na waliokuwa viongozi wa Saccos kwa kumtumia Reuben Mwandambo, huku wakigawana fedha hizo kwa kuorodhesha wanachama hewa ambao walipewa mikopo ya mamilioni.
“Sasa tunakusudia kuwafungulia kesi watu hawa, kwani kisingizio wanachokitoa kwa muda mrefu ni kwamba kesi iko mahakamani wakati fedha zetu zimechukuliwa na watu hawa na kinachoendelea ndani ya Saccos ni ubabaishaji mtupu.
“Zaidi ya Sh milioni 600 za hisa zetu ndani ya Saccos nazo zimetafunwa, tukifuatilia tunazungushwa kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote na sasa tumerudishwa nyuma na viongozi hawa ambao hawachukuliwi hatua zozote,” anasema mmoja wa wanachama hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Anasema uongozi wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU) unahusika na upotevu wa fedha hizo kwa kutokana na kushindwa kuwachukulia hatua wahusika kwa kuendelea kuingiza visingizio kuwa wahusika wamefikishwa mahakamani, lakini ukweli ni kwamba kinachoendelea ni kutafuta namna ya kulindana.
Wanachama hao wanasema, wanapohoji kuhusu upotevu wa fedha hizo na wahusika kuachwa wakiendelea na kazi kama hakuna kilichojitokeza, uongozi wa chuo umekuwa ukitishia kuwafukuza kazi.
Fedha hizo zilikopwa na Wazalendo Saccos kwa udhamini wa chuo hicho kuanzia mwaka 2008 hadi 2012 kutoka CRDB, KCBL, SELF, PPF na OIKO Credit na kusababisha upotevu wa Sh bilioni 6.
Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika nchini katika ripoti yake baada ya kufanya ukaguzi katika chama hicho, anasema chama kilikopa kiasi kikubwa cha mikopo kutoka katika taasisi za fedha ikifikia jumla ya Sh 6,803,610,000 bila kufanya tathmini kutoka taasisi mbalimbali.
Mwaka 2008 hadi 2011 kilikopa tena Sh 4,243,700,000 kutoka katika taasisi hizo za fedha huku mikopo yote kwa asilimia 50 ikitolewa bila kuzingatia taratibu wakati asilimia 11.8 ya mikopo hiyo ikitumika katika urejeshaji wa mikopo kutoka taasisi moja na kwenda nyingine.
Bodi, Menejimenti na Kamati ya Usimamizi waliokuwapo kati ya 2008 hadi 2012 ilihusika na upotevu wa Sh 3,381,899,103 ikiwa ni mikopo ama malipo yasiyozingatia taratibu yanayofikia Sh 3,099,102,303 na upotevu wa Sh 254,516,890 na kusababisha kiasi hicho kikubwa cha fedha kuwa nje na kutorejeshwa.
Waliotajwa na ripoti hiyo kuhusika na upotevu wa fedha hizo ni Mbonea Maghimbi, Mwandambo, Emrode Kimambo, Dk. John Haule, Jasinta Tarimo, Ibrahim Shughuru, Gloria Chuwa na Paul Kibiriti ambaye ni askari polisi akihusishwa pia na uchukuaji wa fedha zilizokabidhiwa kwa Maghimbi.
Pia uongozi wa chama hicho ulishindwa kusimamia vizuri uendeshaji na usimamizi wa chama kwa kuzingatia Sheria ya Ushirika, kanuni pamoja na miongozo mbalimbali iliyoko ndani ya chama ikiwa ni pamoja na sera ya mikopo na fedha.
Katika ripoti yake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika anaeleza kwamba dosari zilizogundulika ni pamoja na kubadilisha utaratibu wa malipo kwa njia ya fedha taslimu badala ya hundi na kumtumia Mtunza Fedha Mkuu wa Chuo, Mwandambo, kuchukua fedha kwa kumhusisha askari asiyekuwa mtumishi wa chama, Kibiriti, kubeba fedha na kuzifikisha sehemu ambayo si ofisi ya chama.
Kitendo hicho ni ukiukwaji wa taratibu za kazi na Sheria ya Ushirika kifungu cha 48 (2,7 na 8) na Kanuni ya Ushirika namba 44 (2) b,c,f,g,h,v na w.
“Kumekuwa na mchezo wa kuiga saini za watu na kuchukua fedha na kuashiria uwepo wa matumizi yasiyokuwa ya halali, huku fedha nyingi zikilipwa kwa kutumia majina yasiyokuwa ya kweli na hivyo kutokuwa na uhakika wa mahali zilikopelekwa fedha hizo,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Sh 1,377,534,000 ni miongoni mwa matumizi yasiyokuwa halali na saini zilizoigwa za Kimambo zimehusika na upotevu wa Sh 618,970,000 na Dk. Haule Sh 758,564,000 na muhusika akitajwa kuwa Maghimbi.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba mtiririko wa fedha ya Wazalendo Saccos sio mzuri na hivyo kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa, hadi Juni 2012 ilikuwa inadaiwa Sh 4,792,559,064 kutoka katika taasisi zilizokopesha.
Marejesho ya mikopo kwenda nje kwa mwezi ni Sh 146,527,175.76 ambazo chama hicho kimeshindwa kulipa huku kikiwa na uwezo kurejesha Sh milioni 45 nazo kimeshindwa kuzilipa na kuwakwepa wadai kwa kuacha kuweka fedha katika akaunti yake ya CRDB.
Kutokana na ufisadi huo chama hicho kimeshindwa kutekeleza baadhi ya vifungu vya sheria ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ushirika namba 20 ya mwaka 2003 na kanuni zake za 2004, huku ikielezwa kwamba chuo kilipojiingiza moja kwa moja kuwa mdhamini wa Saccos ikawa mwanzo wa wizi wa fedha hizo.
Bodi, Menejimenti na kamati ya usimamizi iliyokuwa madarakani kati ya mwaka 2008 hadi 2012, ilimkodisha mtunza fedha wa chuo Mwandambo, kufanya kazi za uhasibu upande wa Saccos na kumtambulisha rasmi benki kwamba atakuwa anahusika na utoaji na uwekaji wa fedha katika akaunti ya chama hicho.
Majina ya wanachama hewa na wengi wao si wafanyakazi wa chuo hicho, yaliingizwa na kupewa mikopo huku fedha hizo zikidaiwa kuwanufaisha watu wachache wakiwamo viongozi wa Saccos na chuo walikokuwa wakigawana.
Pia uchunguzi wa Mrajisi ulibaini madudu mengine ya chama hicho kwamba daftari la wanachama halikutunzwa ipasavyo, hivyo kushindwa kuelewa idadi kamili ya wanachama ambao ni watumishi wa chuo na wale wasiokuwa watumishi na namba moja kupewa zaidi ya mtu mmoja.
Bodi ya uongozi na Menejimenti hazikuwa na kumbukumbu sahihi za wananchama kwa mujibu wa kanuni namba 27, 44 (n), 51 na 15 na kusababisha upotevu wa fedha hizo.
Pamoja na hayo upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha za mikopo unazihusisha moja kwa moja benki za KCBL, NMB, CRDB na KCB ambazo ziliidhinisha hundi mbalimbali za malipo kutoka Wazalendo Saccos bila kufanya uhakiki wa saini zilizowekwa kwa ajili ya kuchukulia fedha benki bila kulinganisha na saini zilizokuwapo katika benki hizo.
Mwandambo aliingizwa kufanya kazi za uhasibu wa Saccos hiyo huku ikiwa na mhasibu wake na menejimenti inayotambulika. Hivyo lengo la kumwingiza katika jukumu hilo likitajwa kuwa nia chafu ya kufanya ufisadi wa kugawana fedha zilizokopwa kwa madhumuni ya kuwainua wanachama.
Chanzo chetu cha habari ndani ya chuo hicho kimelieleza JAMHURI, kwamba uongozi wa chuo kwa kushirikiana na Kamati ya Uongozi wa chama hicho walitengeneza majina ya wanachama hewa ambao sio waajiriwa wa chuo na kuwakopesha mikopo ya mamilioni ya shilingi ambazo ziliingizwa katika mgawo kwa waasisi wa wizi huo.
Katika Akaunti namba 4036600238 benki ya NMB, kati ya Juni 13 hadi 17, 2008 kwa nyakati tofauti, Mwandambo alilipwa jumla ya Sh 115,800,000 kwa hundi zilizosainiwa na Maghimbi (aliyekuwa Mwenyekiti wa Saccos) na Dk. Haule.
Pia katika akaunti namba 01J104298101 benki ya CRDB Septemba 2008 kwa nyakati tofauti Mwandambo alichukua Sh 317,960,000 kwa hundi zilizosainiwa na Maghimbi, Dk. Haule na Kimambo.
Kutokana na wingi wa mikopo isiyozingatia utaratibu baadhi ya wajumbe wa Bodi na Kamati ya Usimamizi, watendaji wamekuwa wakichukua mikopo zaidi ya mara tatu na kufikia mara 31 kinyume kabisa na taratibu za uendeshaji wa Saccos na kutozingatia uwezo wa mkopaji kurejesha na kuvunja kanuni za Ushirika namba 90 (1), 94 (1) na 96.
Wengine wanaotajwa na ripoti ya Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika kwamba waliohusika na upotevu wa fedha hizo ni Jasinta Tarimo aliyekuwa Meneja wa Saccos, Shughuru akiwa Mtunza Hazina na Chuwa aliyekuwa Mtunza Fedha (cashier) huku fedha zilizochukuliwa benki na kwenye taasisi nyingine kwa kiasi kikubwa matumizi yake hayaeleweki.
Tume iliyokuwa ikichunguza tuhuma za upotevu wa fedha hizo zilizokopwa na Saccos hiyo bila kuzingatia taratibu ikiwa chini ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika kati ya mwaka 2012 hadi 2013.
Ilibaini pia mkopo wa zaidi ya sh bilioni 1 kutoka kampuni ya Oiko Credit ambao ulikopwa kwa njia zisizoeleweka na uongozi wa chama hicho.
Mikopo mingine ambayo haikuzingatia taratibu iliyokopwa na Saccos hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja tu wa 2011 ni Sh 316,970,000 NMB, KCBL Sh 262,000,000 na CRDB Sh 102,260,000.
“Aliyekuwa Mwenyekiti, Maghimbi, alitwaa madaraka ya kutoa mikopo kinyume na taratibu kwa baadhi ya wanachama na wasio wanachama bila kibali cha Kamati ya Mikopo na kuvunja kanuni za ushirika namba 65 (1) na 88 (1-5) na kwenda kinyume cha kanuni 93 (1),” imeeleza sehemu ya ripoti ya Mrajis.
Wanachama hao wanaeleza kwamba mikopo iliyokopwa holela na uongozi wa Saccos hailipiki na kinachofanyika sasa ni wahusika kuzikwepa taasisi hizo za fedha kwa kufungua akaunti mpya benki kwani kila kilichoingizwa kinachukuliwa kama malipo ya deni.
Mwandambo ambaye alikuwa na jukumu la kuchukua fedha benki licha ya kuwa sio mfanyakazi wa Saccos hiyo, amelieleza JAMHURI wiki iliyopita kwamba alikuwa anatumwa na Kamati tangu mwaka 2008 kuchukua fedha kwa utambulisho wa barua maalumu na kuwakabidhi wahusika.
Anasema baada ya kuwakabidhi kiasi cha fedha zilizohitajika kutoka benki, kazi yake iliishia hapo na utaratibu wa utoaji wa mikopo ilikuwa ni kazi ya kamati.
“Kamati ilikuwa inanituma kuwachukulia fedha benki, walikuwa wanazitumia wao na mimi ni mwanachama wa kawaida tu ndani ya Saccos, na walipogawana mimi sikuambulia hata senti moja. Wanajua walikuwa wanamlipa nani.
“Tangu mwaka 2013 nasumbuliwa na Polisi ambako nimekuwa nikiripoti mara moja kila mwezi kwa kupangiwa tarehe tu na hakuna kinachoendelea. Kama ni uchunguzi wanikutanishe na wahusika wote nieleze ukweli badala ya kunisumbua hivi bila sababu za msingi,” anasema Mwandambo.
Naye Maghimbi aliyekuwa Mwenyekiti wa Saccos hiyo aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma za ufisadi huo wa kutisha, ameieleza JAMHURI, kwamba kati ya mwaka 2005 hadi 2012 kiasi cha mkopo kilichokopwa na Saccos kutoka benki ni Sh bilioni 6 tu.
Maghimbi anasema kutokana na tuhuma hizo za ufisadi ni yeye pekee aliyeshtakiwa kati ya viongozi wote huku suala hilo likiwahusu watu wengi.
“Jambo hili limenisikitisha sana kwani limefikishwa mahakamani tangu mwaka 2012, kwa ufupi niseme liko huko na mzigo wote nimebebeshwa mimi,” anaeleza.
Mwenyekiti wa sasa wa Saccos hiyo, Tito Haule, anasema tuhuma hizo za upotevu wa mamilioni ya shilingi zilipelekwa mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria.
Anasema haiwezekani watu wahusike na upotevu wa fedha nyingi kiasi hicho halafu walalamike kwamba wameonewa. Wahusika wameulizwa walikopeleka fedha hizo lakini hakuna ushirikiano wowote walioutoa.
Anasema Mwandambo alihojiwa kuhusu fedha hizo zilikopelekwa lakini hakutoa ushirikiano wowote na kueleza kwamba tutakutana mahakamani.
“Huyu anachota fedha zote hizo halafu anasema nini? Hilo la kuwaingiza watu wengine ndani ya chama ambao sio watumishi wa chuo ndiyo chanzo cha ufisadi huu na kusababisha hasara kwa kipindi cha miaka sita.
“Hawa wanachama waliokueleza tuhuma hizi wamevunja kanuni za chama, kwani walipaswa kuwasilisha madai yao katika uongozi ili yajadiliwe katika mkutano mkuu,” anasema mwenyekiti huyo.
Anasema tangu mwaka 2012 wamekuwa wakifanya mkutano mkuu kila mwaka na kwamba mikopo yote ilidhaminiwa na chuo isipokuwa wa Oiko Credit uliodhaminiwa na Bodi ya Wadhamini wa Saccos.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Faustine Bee, ameieleza JAMHURI kwamba suala hilo linashughulikiwa kisheria na wanaolifahamu kwa undani ni viongozi wa Saccos hiyo.
Lakini baadhi ya wanachama wametuhumu Profesa Bee kwamba anawalinda wahusika wa wizi wa fedha za chama kwa kutishia kuwafukuza kazi watumishi wanaofuatilia upotevu wa fedha hizo kwa madai kwamba liko mahakamani.
Baadhi ya malipo yasiyozingatia taratibu
Katika Akaunti namba 4036600238 Benki ya NMB kiasi cha Sh 115,800,000 zililipwa kwa Mwandambo Juni 13, 2008 kwa stakabadhi namba 4060, hundi namba 5839811 yenye kiasi cha Sh 17,600,000, stakabadhi namba 4067, hundi 5839818 ya Sh 6,500,000, stakabadhi namba 0, hundi 5839819 ya Sh 23,400,000 na stakabadhi namba 4068, hundi 5839816 ya Sh 16,000,000.
Juni 16,2008 stakabadhi namba 4078, hundi namba 5839820 ya Sh 14,700,000, stakabadhi namba 0, hundi 5839825 ya Sh 7,600,000, stakabadhi namba 0, hundi 5839827 ya Sh 12,000,000, stakabadhi namba 0, hundi 5839828 ya Sh 11,000,000 na Juni 17,2008, stakabadhi 4086, hundi 5839829 yenye kiasi cha Sh 7,000,000.
Hicho ni kiasi kidogo cha fedha kilichochukuliwa na Mwandambo huku waliotia saini hundi hizo wakiwa ni Mbonea na Dk Haule, ambao ni miongoni mwa watu wanaotajwa na ripoti ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kuhusika na ufisadi huo.