Watu watatu akiwemo mama mzazi wa mtoto Zawadi Msagaja (20) na mkazi wa kijiji cha Mahaha wilayani Magu mkoani Mwanza, wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kike kwa kumzika akiwa hai ili wapate mali.

Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kusomewa shtaka la mauaji ya mtoto huyo ni dada yake Zawadi aitwaye Elizabeth Kaswa na mumewe, Mussa Mazuri ambaye ni mganga wa kienyeji.

Akiwasomea shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Fortunatus Kubaja, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale ameieleza Mahakama kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 13, mwaka huu.

Ameendelae kusema, washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 7/2022 walitenda kosa hilo katika mtaa wa Kisundi Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela mkoani humo kwa kumzika mtoto huyo akiwa hai ili wapate mali kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu marejeo namba 16 ya mwaka 2022.

“Washtakiwa wote mchana wa siku hiyo mlishirikiana kumpatia mtoto wa Zawadi dawa za kienyeji akalewa kisha mkamfukia akiwa hai na kumsababishia kifo kwa malengo ya kujipatia mali kinyume na sheria,” alieleza Changale.

Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya washtakiwa kusomewa shtaka linalowakabili, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kubaja aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatano Desemba 28, mwaka huu, itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.

“Washtakiwa hamtakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hii haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi yenu. Wote mtaendelea kukaa rumande kwani shtaka linalowakabili halina dhamana,” amesema Kubaja.

Novemba 29, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa SACP-Wilbroad Mutafungwa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kwa makosa ya kula njama na kumzika mtoto wa Zawadi Msagaja (jina linahifadhiwa) kama kafara ili wajipatie utajiri jambo ambalo ni kinyume na sheria na kukiuka haki za binadamu.