*Mashahidi wazungumza na JAMHURI, walieleza ya moyoni

*Wamsifu Rais Samia kurejesha utawala wa sheria nchini

*Wataka wateule wapate fundisho kwani ipo siku yatawakuta

*Gazeti la JAMHURI lilikuwa la kwanza kufichua uovu wake

DAR ES SALAAM, ARUSHA

Na Waandishi Wetu

Mashahidi kadhaa ambao ushahidi wao umechangia kumtia hatiani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, wamesema haki imetendeka, JAMHURI limeambiwa.

Pia wananchi wamesema hukumu ya Sabaya ni fundisho la wazi kuwa cheo ni dhamana, hivyo wanaopata nafasi wazitumie kwa uangalifu.

Ijumaa iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilimtia hatiani Sabaya na wenzake wawili kwa makosa matatu, likiwamo la unyang’anyi wa kutumia silaha, yaliyowafanya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, mashahidi hao, Diwani wa Sombetini, Bakari Msangi na mmiliki wa duka la Shaahid, Ally Aljarin, wametoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuingilia kati uovu waliotendewa.

“Kitendo cha Rais kutengua uteuzi wa Sabaya kupisha uchunguzi kilionyesha wazi jinsi Mama anavyochukia uovu na uonevu,” anasema Msangi.

Pia Msangi na Aljarin wamemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salum Hamduni, kwa kusimamia haki.

Wakati Sabaya na genge lake wakifanya uovu huo, Hamduni alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha. Aljarin anasema ameridhishwa na hukumu iliyotolewa, akisisitiza kwamba haki imetendeka.

“JAMHURI mlikuwa wa kwanza kuandika habari iliyosababisha hatua kuchukuliwa. Wengine walikuwa wanaogopa au hawataki, lakini ninyi mkathubutu. Tunawashukuru sana kwa kweli,” anasema Aljarin.

Katika toleo Namba 492 la Machi 2 – 8 mwaka huu, JAMHURI lilichapisha kwa undani habari iliyohusu kisa cha Sabaya kuvamia duka la Aljarin, kuwapiga wafanyakazi pamoja na Msangi, kisha kuwateka nyara.

Baada ya kuandika habari hiyo, watangazaji wa Wasafi FM wakiongozwa na Maulid Kitenge walisoma kichwa cha habari hiyo; ‘DC amtembezea kipigo diwani’, lakini aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (kabla wizara haijatenganishwa), Innocent Bashungwa, alilaani habari hiyo akidai kuwa ni ya uzushi.

Miezi michache baadaye, Sabaya aliondolewa kwenye ukuu wa wilaya na kushitakiwa, ambapo sasa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kudhihirisha kuwa yaliyoandikwa na Gazeti la JAMHURI yalikuwa sahihi.

Iwe fundisho

Aljarin na Msangi wameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kutoa haki, wakisema hukumu hiyo iwe fundisho kwa wote wanaopewa dhamana ya uongozi, wafahamu nyadhifa walizopewa ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na si kuwatendea ukatili. Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo Oktoba 15, 2021.

“Kama alivyosema Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia, kwamba mshitakiwa wa kwanza Lengai ole Sabaya alikuwa mkuu wa wilaya aliyeteuliwa na Rais, kitendo alichofanya kinadhalilisha taasisi ya urais,” amesema Amworo na kuongeza:

“Na hakuna ubishi kwamba washitakiwa wote ni vijana na wanahitajika, kama walivyoeleza mawakili wao. Kwa mujibu wa sheria hakuna ubishi kwamba mikono yangu imefungwa. Naweza kuwafunga miaka 100, lakini kurudi chini, siruhusiwi kuwafunga chini ya miaka 30.

“Mbali ya kwamba wakili wa serikali ameomba wachapwe viboko, na walistahili kuchapwa, manake nao walikuwa ‘wanawatoa wenzao wenge’ (mahakama ikaangua kicheko), lakini mawakili wenzetu wameshindwa kuinyambulisha sheria ya zamani ya watoto waliokuwa wanapigwa viboko, kwa kuwa sheria mpya hawapigwi viboko. Hawa wamepenyea hapo angalau.

“Basi mikono yangu imefungwa. Adhabu ya chini ni miaka 30 na viboko. Kosa la kwanza kila mshitakiwa miaka 30 kila mmoja; kosa la pili miaka 30 kila mmoja na kosa la tatu miaka 30 kwa kila mmoja. Kwa viboko, mawakili wameshinda. Sitatoa adhabu ya viboko. Adhabu hizi ziende pamoja. Rufaa iko wazi.”

Ni kama ndoto

Sabaya ameshindwa kuchomoka. Alipowasili mahakamani alikuwa anatabasamu, akaondoka akiwa na majonzi na hukumu iliposomwa alikuwa kama mtu aliyenyeshewa mvua. Ni kama ndoto yenye jinamizi la kutisha kwa Sabaya na wenzake; Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Jinamizi la kesi hiyo limewaandama kwa miezi minne huku umma ukishuhudia umahiri wa kuchambua vifungu vya sheria kati ya mawakili wa upande wa Serikali na wa utetezi.

Akina Sabaya walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27, mwaka huu huko Kinondoni, Dar es Salaam.

Baada ya hukumu, wakili wa Sabaya na wenzake, Mosses Mahuna, amesema hawajaridhika nayo kwa sababu ina kasoro kadhaa; kauli inayoonyesha nia ya kukata rufaa.

Mambo mengi ametuhumiwa kuyafanya yakiwamo ubabe, ubakaji, uporaji, utekaji nyara, vitisho, rushwa na ubambikiaji kesi, huku baadhi wakimtuhumu kuiga mwenendo wa wakuu wa mikoa watatu ambao nao watu wanasubiri kuwaona mahakamani.

Kabla ya Sabaya kusimamishwa kazi na Rais Samia kupisha uchunguzi Mei 13, mwaka huu, alikuwa amehudumu nafasi ya ukuu wa wilaya kwa miaka miwili na miezi 10 baada ya kuwa ameteuliwa Julai 28, 2018 na Rais Dk. John Magufuli.

Akiwa madarakani, Sabaya amejinasibu kama kiongozi mwenye nguvu, anayeogopwa wakati wa utawala wa Rais Magufuli na inadaiwa aliunda genge binafsi la uhalifu lililotumika kutisha watu na kuwapora, waliokataa kumpa fedha akawatishia kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi au utakatishaji fedha.

Taarifa nyingine zinadai kwamba vitendo vya kibabe amewafanyia zaidi mahasimu wake wa kisiasa aliokinzana nao wakati wa vuguvugu za siasa ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) jijini Arusha.

Muathirika mmoja wa vitendo vya Sabaya amewahi kunukuliwa akisema alilazimishwa kuchagua namna ya ‘kushughulikiwa’.

Akijitetea kuhusu mwenendo wake uliokuwa ukilalamikiwa na wengi, Sabaya anadai kuwa ‘ilikuwa ni maelekezo kutoka juu’ bila kutoa uthibitisho wowote.

Sabaya amewahi kuonyesha ujeuri hata kwa wateule wenzake, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira. Hai ni moja ya wilaya za mkoa huo.

Kabla ya kuteuliwa kuwa DC, Sabaya amewahi kutuhumiwa kwa utapeli akijifanya ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) anayefanya kazi maalumu.

Wakati kesi yake na wenzake ikiunguruma, amewahi kujitetea akisema operesheni alizokuwa anafanya ni maagizo kutoka kwa Magufuli; na kwamba aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango ambaye sasa ni Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alizifahamu; utetezi ambao haukumsaidia

Wachambuzi wanasema hukumu ya Sabaya iwe funzo kwa wateule wote wa Rais kuanzia kwa mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu, manaibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya, halmashauri za manispaa na miji.

“Kwamba cheo ni dhamana, kwa hiyo ukipewa unaweza kunyang’anywa muda wowote na aliyekupa.

“Kama hivyo ndivyo, viongozi hao na wengine wanatakiwa kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu na weledi wa hali ya juu,” amesema mmoja wa watu waliozungumza na JAMHURI.

Rais Samia amewahi kunukuliwa hivi karibuni akisema: “Kwa ujumla niseme kuwa uongozi ni dhamana. Sitegemei kumuona mkuu wa mkoa anaingia katika vitendo vya rushwa. Sitegemei wala sitastahamili. Sitegemei wakuu wa mikoa mnakuwa miungu watu kule mlipo. Mpo kule kuwatumikia watu, si watu wawatumikie nyie.”

Baada ya hukumu hiyo, baadhi ya watu wametoa maoni tofauti akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, ambaye siku za nyuma amewahi kutofautiana na Sabaya.

“Ole Sabaya leo (Oktoba 15, mwaka huu) ni siku mbaya kwako, familia yako pamoja na wenzako. Nilituma salamu zangu kwako nami nilipokea salamu zako kupitia Wakili wangu Sheikh Mfinanga. Iko njia ya amani mbele yako, nayo ni kutubu uovu wote. Mwamini Mungu ili uishi na amani yake, yeye ni njia pasipo na njia,” anasema Lema.

Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu, Peter Madeleka, anasema somo kubwa la kujifunza kupitia katika hukumu ya Sabaya ni kwamba jinai haizeeki.

“Wale viongozi wote wasiofuata sheria watambue kwamba kile kilichotokea mahakamani Oktoba 15, mwaka huu kitawakuta siku chache zijazo. Jinai haizeeki. Tubuni na mheshimu sheria sasa,” anasema Madeleka: 

“Kwa hiyo utafanya leo utatoka, muda utapita, lakini hata kama ni kipindi cha awamu ya 10, hiyo jinai yako itakufuata. Kwa hiyo watu wote wanatakiwa kufuata sheria kama ibara ya 26 (1) ya Katiba inavyotutaka kutii Katiba na tufuate sheria, kwa sababu tusipofuata yatakuja kutukuta kama haya yaliyomkuta Sabaya.

“Utajiona wewe ni mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, sijui wewe ni kamanda, sijui wewe ni mkurugenzi, utafanya kinyume cha sheria, lakini kesho yake hao hao waliokuwa wanakutuma, maana Sabaya naye amesema alikuwa anatumwa, hawatakuwa na wewe. 

“Watakuuliza, kwani sheria inasemaje? Kwa hiyo tukumbuke jinai haizeeki na tukumbuke pia kwamba hiyo ni dhamana na tunatakiwa kutenda haki na mwisho tunatakiwa kutenda majukumu yetu kwa kufuata sheria za nchi.” 

Madeleka anasema Sabaya alipojitetea mahakamani alisema ametumwa, hivyo akaomba apunguziwe; “Adhabu, je, kisheria hiyo imekaaje?” anahoji.

Anasema hakuna sheria inayosema kitendo chochote haramu kinachofanywa kwa kutumwa kinakuwa halali na hakuna sheria inayosema hivyo.

 “Hakuna sheria yoyote inayosema kwamba kitendo chochote kilichokatazwa na sheria kwamba kikifanywa na maelekezo ya mtu fulani basi kinakuwa ni halali,” anasema Madeleka na kuongeza:

 “Kwa hiyo Sabaya alikuwa hajui hilo, akafikiri kwamba ukitumwa inakuwa ni kinga, kwa sababu chini ya ibara ya 13 (1) ya Katiba inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria. Kwa hiyo hata huyo anayekutuma lazima ujiulize hayo maelekezo anayokutuma yapo katika maelekezo ya sheria?

“Na ukiyakataa unakuwa haujafanya kosa kisheria.  Kwa hiyo Sabaya alifanya kosa kwa sababu alitekeleza maelekezo ambayo yako kinyume cha sheria, na nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria.”

Habari iliyofichua uovu wa Sabaya

Gazeti la Machi 2, 2021 Gazeti la JAMHURI lilichapisha habari hii:

DC amtembezea kichapo Diwani

ARUSHA

Na Hyasinti Mchau

Diwani wa Sombetini, jijini Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bakari Msangi, amejikuta katika wakati mgumu alipojaribu kuingilia kati ugomvi kati ya wahudumu wa duka moja jijini hapa na ‘wateja’ wao watano.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 11 jioni ya Februari 9, mwaka huu baada ya wateja hao kuvamia duka linalomilikiwa na Mohamed Ajarin lililopo Mtaa wa Nyamwezi, maeneo ya Soko Kuu katikati ya Jiji la Arusha, linalofahamika kwa jina la Shaahid Stores.

Msangi amelieleza JAMHURI kuwa awali watu hao walidhaniwa kuwa ni wateja, lakini kumbe ni ‘mabaunsa’ (walinzi/wapambe) wa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya.

“Mimi nilipigiwa simu na (mfanyabiashara) jirani wa duka hilo (anaitwa Ally Saji), akaniambia kuwa kuna vurugu kwenye duka la Ajarin. Nikaenda haraka,” anasema Msangi ambaye ni rafiki wa mmiliki wa duka hilo.

Anasema alipofika dukani hapo alikuta mlango umefungwa, akaufungua na kuingia ndani ambako alimkuta Ole Sabaya na vijana wake wakiwahoji na kuwapiga wahudumu wa duka hilo; wakitaka kujua aliko bosi wao.

“Nikawataka waache kuwapiga kwa kuwa ni kinyume cha sheria na kama wamefanya makosa, basi wapelekwe polisi. Nikamuuliza Ole Sabaya ni nini kimetokea?

“Hilo likawa ndilo kosa langu. Akasema, ‘tena wewe nilikuwa ninakutafuta, una kiherehere sana, bora umejileta’, akawaamuru vijana wake wanishughulikie. Wakaanza kunipiga!” anasema Msangi kwa mshangao.

Kuanzia wakati huo, Msangi na wafanyakazi wa duka hilo waliendelea kupata kipigo hadi saa tatu usiku.

Kwa mujibu wa Msangi, baada ya kuzidiwa kipigo wakaahidi kuwapeleka akina Ole Sabaya nyumbani kwa Ajarin ‘kuzungumza’ naye.

Akiwa katikati ya mabaunsa wawili ndani ya gari la Ole Sabaya huku wafanyakazi wakiwa kwenye gari jingine, safari ya kuelekea Ngarenaro nyumbani kwa Ajarin ikaanza na kufika huko saa tatu na nusu usiku.

Majibu ya mke wa Ajarin yalikuwa sawa na yaliyotolewa awali na wafanyakazi dukani, kuwa mfanyabiashara huyo amesafiri.

“Sikuachiwa mara moja hadi nilipofanikiwa kumpigia simu mke wangu na kumuelekeza kuwa ‘nimetekwa’ na Ole Sabaya na wakati huo tupo Hoteli ya Tulia, Sakina.

“Nikamwambia awaeleze majirani ili waje kunikomboa. Wakaja,” anasema Msangi.

 Baada ya patashika za hapa na pale, hatimaye Msangi aliachiwa huru na kuondoka na majirani waliokwenda kumkomboa.

Awataarifu viongozi wa mkoa

Msangi anasema alipofika nyumbani aliwatafuta kwa njia ya simu bila mfanikio Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).

 “Bahati nzuri nikampata mkuu wa mkoa. Akasikitika sana na kunielekeza tukutane Kituo cha Polisi usiku huo huo.

 “RC alifanikiwa kuwapata makamanda hao wa polisi na saa saba usiku huo huo tukakutana kituoni, nikapewa PF3 kwa ajili ya matibabu,” anasema.

Gwaride la utambulisho

Siku chache baadaye, Jeshi la Polisi mkoani Arusha chini ya RPC Salum Hamduni liliandaa gwaride la utambulisho katika jitihada za kuwanasa watuhumiwa wa tukio hilo.

Gwaride hilo lililofanyika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha, liliwahusisha vijana 10 ambapo Msangi na mfanyakazi mmoja wa Shaahid Stores, Lomorn Jasin, walitakiwa kuwatambua wanaodaiwa kuwatesa.

Wakati Msangi akiwatambua mabaunsa wawili kati ya watano waliohusika, Jasin hakumtambua hata mmoja.

“Nisingeweza kuwasahau kwa kuwa tulipanda nao gari moja kutoka dukani kwenda nyumbani kwa Ajarin. Walikuwa na Ole Sabaya wakati wote. Hawa ndio waliokuwa wakinilinda wakati nikiwa ‘nimetekwa nyara’,” anasema.

Akizungumzia sababu ya kushindwa  kuwatambua watesi wake, Jasin anasema mbali na hofu aliyokuwa nayo wakati wote, sababu kubwa ni:

“Walikuwa wamevaa ‘masks’ (barakoa au kitambaa cha kufinya uso), sikuweza kuwaona vema,” anasema Jasin.

Kisa ni nini?

Mmiliki wa duka hilo na mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Ajarin, ameliambia JAMHURI kuwa tukio hilo limemfedhehesha yeye na familia yake.

“Walipofika nyumbani, wale vijana (mabaunsa) walimsukasuka sana mke wangu wakitaka awaeleze niko wapi. Hawakumtendea haki na hadi leo bado yupo kwenye ‘shock’,” anasema Ajarin ambaye bado hajarejea kazini kwa kuwa yu mgonjwa.

Anasema kabla ya tukio hilo amewahi kupokea vitisho kwa njia ya simu kutoka kwa Ole Sabaya, kwa madai kuwa anazo taarifa zake kuwa anabadili fedha za kigeni kinyume cha sheria na kwamba angemchukulia hatua kwa kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi.

“Sikutegemea kama kuna siku angevamia dukani kwangu! Wala sikuwa na hofu kwa kuwa mimi sifanyi biashara ya kubadili fedha,” anasema.

RPC wa Arusha, Salum Hamduni, amelithibitishia JAMHURI kuwapo kwa tukio hilo na kwamba malalamiko hayo yapo mezani kwake.

“Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili waliotambuliwa na diwani (kwenye gwaride la utambulisho). Upelelezi unaendelea ili kuwakamata wote waliohusika,” anasema Afande Hamduni.

Ally Saji, jirani wa Shaahid Stores, anasema siku ya tukio alishangazwa kuona vijana watano wakishuka kwenye ‘Land Cruiser’ mbili zenye namba sa usajili za DFP na kuingia kwenye duka hilo huku wakitanguliwa na mwanamke mmoja.

“Walipoingia wakafunga mlango wa duka, nikaenda kuchungulia, nikaona wahudumu wa duka lile wanapigwa ndipo nikampigia simu diwani kwa kuwa ninajua ni rafiki mkubwa wa Ajarin,” anasema Saji.

Akizungumzia yaliyojiri wakati huo, Jasin anasema baada ya watu hao kuingia dukani, walimuuliza ni nani amemruhusu kumbadilishia dola yule dada waliyekuwa naye.

“Kabla hata sijajibu, nikaanza kupigwa. Muda huo huo na wenzangu nao wakaanza kupigwa huku tukitakiwa kuwaonyesha aliko mmiliki wa duka.

“Nikawaambia kuwa amesafiri, lakini hawakuelewa. Kwa kweli tulipigwa sana, ninadhani ndiyo maana hata kwenye gwaride la kuwatambua nilishindwa kumjua hata mmoja,” anasema.

Ole Sabaya agoma kuzungumza

Tangu kuanza kuvuja kwa taarifa za tukio pamoja na video kwenye mitandao michache ya kijamii, JAMHURI limekuwa likimtafuta bila mafanikio Ole Sabaya kutaka kujua undani wa habari hii.

 Mwandishi wetu amempigia simu zaidi ya mara tano na mara zote ama ilikatwa au iliachwa bila kupokea.

 Hata siku ya gwaride la utambulisho, JAMHURI halikuweza kuzungumza na Ole Sabaya, wala hakujibu ujumbe mfupi wa maandishi alioandikiwa.

 Katika ujumbe huo, mbali na kuelezwa tuhuma za Msangi dhidi yake, JAMHURI lilitaka kufahamu sababu ya yeye kuondoka kituo chake cha kazi mkoani Kilimanjaro na ‘kupeleka’ vurugu mkoani Arusha.