2110Wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne nilijitahidi kuyapigia kelele masuala mbalimbali ya elimu. Lakini hayupo aliyejali lakini hali hiyo haikunikatisha tamaa.

Namkumbuka vyema William Wilberforce, yule mbunge wa Bunge la Uingereza. Huyu hakuchoka kupigania Uingereza ipitishe sheria ya kukomesha biashara ya watumwa mpaka sheria hiyo ikapitishwa mwaka 1807. Nami sitachoka kupigania kile ninachokiamini.

Nazungumzia fedha za chenji ya rada iliyokuwa imetengwa na Bunge kwa ajili ya kununulia vitabu na madawati. Ninaamini kwamba sehemu kubwa ya fedha hiyo haikufanya kazi iliyokusudiwa.

Kama tujuavyo, Serikali ya Awamu ya Nne kilikuwa ni kipindi cha kutafuna fedha za umma. Na hapana shaka hii fedha ya rada iliyokuwa imeamuliwa na Bunge inunue madawati na vitabu, sehemu yake kubwa ilitafunwa. Nina sababu za kutosha kuamini hivyo.

Tuanze na madawati. Kuanzia wakati huo mpaka leo haijulikani ni wilaya zipi za Tanzania Bara zimepatiwa madawati. Tulichoshuhudia ni kila wilaya kufanya juhudi zake kushughulikia tatizo hili la madawati.

Tanzania tulikuwa na tatizo sugu la watumishi hewa kulipwa mishahara. Tukafika mahali kila mtu aliamini kwamba hakuna mtu aliyeweza kulimaliza tatizo hili, naye si mwingine bali ni Rais John Magufuli.

Kufumba na kufumbua tumeweza kujua idadi ya watumishi hewa kwa kila mkoa. Karibu wakuu wa mikoa wote wa Tanzania Bara walisimamia kwa ufanisi mkubwa. Kazi ya kutafuta watumishi hewa wakapatikana na kila mkuu wa mkoa alikusanya takwimu za mkoa wake kuhusu watumishi hewa.

Haijulikani ni sababu ipi iliyofanya takwimu za wilaya zilizopata madawati ya fedha za rada zishindikane kupatikana.

Kinachoshangaza ni kuona kwamba wananchi wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na wabunge wao, wameendelea kulalamika kwamba shule za maeneo yao hazina madawati lakini hakuna aliyechukua hatua kutafuta ukweli wa mambo.

Polisi hawajachukua hatua. Taasisi ya Kuzuiana na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haijachukua hatua. Nayo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajafanya kazi ya kukagua na kubainisha maeneo yenye harufu ya ufisadi, ubadhirifu na ukiukwaji wa sheria ya manunuzi kwa upande wa fedha hizi za rada. Kwa hiyo, waliotafuna fedha hizi za chenji ya rada wameendelea kuwa salama.

Kwa kuwa tumekuwa na Serikali sikivu, Serikali ya Awamu ya Tano, hapana shaka italivalia njuga suala hili. Inawezekana fedha ya rada peke yake isingeweza kutupatia madawati ya kumaliza shida yetu, lakini ingesaidia kupunguza shida.

Hakuna wilaya hata moja inayoweza kudai au iliyodai kwamba ilinufaika na madawati yaliyotokana na fedha ya rada.

Kwa hiyo, hakuna haja ya Rais Dk. Magufuli kuwaagiza wakuu wa mikoa kukusanya takwimu za madawati yaliyonunuliwa kwa fedha za rada. Au kazi hii inaweza kurahisishwa kwa kuitaka taasisi iliyosambaza madawati kutaja shule ambazo ilipeleka madawati na idadi yake kisha wakuu wa mikoa wawaagize watu wao kwenda kuthibitisha hivyo.

Rais Dk. Magufuli ameendelea kusema kwamba haiwezekani watu waliowatesa Watanzania na kula fedha yao waachwe hivi hivi, lazima wachukuliwe hatua. Watangazwe na kuadhibiwa ili watu wengine wapate fundisho.

Bora watafutwe watu waliotafuna fedha za rada. Kisha mali zao ziuzwe ili zipatikane fedha za kuzipatia shule zetu madawati.

Sasa tuangalie upande wa vitabu. Kuna fedha ya kutosha iliyotengwa kutoka fedha za rada iliyopangwa kununua vitabu. 

Kabla haijatolewa fedha hiyo ya rada, wadau wa elimu tuliandika magazetini tukitaka Wizara ya Elimu isinunue vitabu kutoka kwa wachapishaji wa vitabu mpaka kwanza walimu wa masomo husika wavipitishe na kuamua vitabu vipi vichapwe na marekebisho fulani na vitabu vipi visichapwe kabisa kutokana na kuzidi kuwa vibovu.

Tulisisitiza kwamba nchi maskini kama Tanzania  ni muhimu itumie kwa uangalifu mkubwa fedha inayopata kwa ajili ya kuboresha vitabu.

Hatukuona sababu ya kufanywa haraka kununua vitabu vibovu wakati ulikuwapo muda wa kutosha kutumia fedha hiyo kwa kununua vitabu vilivyoboreshwa.

Ukweli ni kwamba baadhi ya watu walioko au waliokuwako wizarani walibuni kampuni za vitabu haraka na vikapewa mgawo. Mashuleni vikasambazwa vitabu hivyo vibovu ambavyo hakuna anayevitumia. Badala yake vimehifadhiwa kwenye bohari mashuleni.

Kama habari kwamba viongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu walihakikisha kuwa wanagawana kila senti ya rada hata kama haikuwa lazima kufanya hivyo, aliyekuwa Waziri wa Elimu anatakiwa kutumbuliwa. Ni jipu sugu.

Tazama! Kuna habari kwamba baada ya kutumika sehemu ya fedha ya vitabu kununua vitabu vilivyokuwa vimekusudiwa kununuliwa ilibaki fedha ya kutosha. Fedha hiyo ingeweza kutumika kununua madawati au kulipa madeni ya walimu. Lakini viongozi na watendaji wa wizara waliamua kuitafuna fedha hiyo.

Kwa mfano, kuna habari kwamba watu wa wizarani walimtaka mchapishaji mmoja wa vitabu achukue shilingi bilioni sita za ziada ili aiuzie Serikali vitabu vyake vyote vilivyokuwa vimebaki kwenye bohari yake. Akaiuzia Serikali vitabu vibovu sana na hiyo ilitoa nafasi kwa wakubwa kugawana shilingi bilioni sita kununua vitabu vibovu kwa bei ya chee.

Wananchi hatuelewi Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii inayohusisha pia elimu inafanya kazi gani. Au ni kwa sababu watoto wa wakubwa wanasoma shule zenye madawati ya kutosha na vitabu bora hata hawajali shule hizi zinazotumiwa na watoto wa wananchi maskini wanaowakilishwa bungeni?

Wananchi tunatazamia wabunge kuona wakidai CAG akague hesabu ya fedha ya rada iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya shule zetu.

Watanzania tunataraji kuona Rais wetu mwenye uchungu na maisha yetu haya ya ‘pata potea’ yanakuwa historia. Anaweza kuyabadilisha kutokana na dhamira yake njema aliyoionesha tangu aingie madarakani.