Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali inaendelea na uhakiki wa mali zote za Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) na kuonya kuwa hakuna atakayepona kwa wale wote watakaobainika kufuja mali za chama hicho kikongwe nchini.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi.
“Mwaka jana tulibaini madudu KNCU, nikatuma timu yangu ikaja kufanya uchunguzi na tukawakamata baadhi ya viongozi na mpaka sasa hata nyie mnajua wako wapi,” amesema waziri mkuu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai. Kiongozi huyo yuko ziarani mkoani Kilimanjaro.
Amesema serikali inakusudia kumega baadhi ya mashamba makubwa ya kahawa yanayomilikiwa na KNCU ili kuwapa wananchi wayatumie kwa kilimo cha mazao ya chakula.
Chama hicho kinamiliki mashamba makubwa ya kahawa katika wilaya za Hai, Siha na Moshi Vijijini. Kwa muda mrefu mashamba hayo hayatumiki kwa malengo yaliyokusudiwa ya kulima kahawa, bali hukodishwa kwa wananchi kwa kilimo cha msimu.
Mwaka jana vigogo watano wa ushirika mkoani Kilimanjaro wakiwamo watatu kutoka KNCU na wawili kutoka Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing (TCCCo) walifikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uhujumu uchumi na kuzisababishia taasisi hizo hasara ya Sh bilioni 4.5.
Waliokamatwa ni Meneja wa KNCU, Honest Temba (38); Makamu Mwenyekiti wa KNCU, Hatibu Mwanga (70) na Mwenyekiti mstaafu, Aloyce Kitau (70). Kwa TCCCo walioshtakiwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, Maynard Swai, na Meneja wa kiwanda hicho, Andrew Kleruu (56).
Walifikishwa mahakamani Julai 10, mwaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Pamela Mazengo na kusomewa mashtaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, akisaidiana na mawakili Jacqueline Nyantori na Shiza Kimera.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanadaiwa kuwa kati ya Julai, 2014 na Novemba 2017, wakiwa viongozi wa KNCU walitumia madaraka yao vibaya.
Kwamba, katika tarehe tofauti, waliilipa Kampuni ya Oceanic Link Shipping Services iliyokuwa imewekeza kwenye shamba la kahawa la Gararagua linalomilikiwa na KNCU fidia ya Sh bilioni 2.9; kitendo kilichoinyima haki KNCU.
Katika shtaka la pili, Chavula alidai kuwa katika kipindi hicho washtakiwa kwa kukusudia, waliilipa kampuni hiyo na kuisababishia KNCU hasara ya Sh bilioni 2.9. Hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
KNCU ililiuza shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 3,429 ukiwa ni mkakati wake wa kujinasua katika madeni yaliyokuwa yakiiandama ya Sh bilioni 5.2 kutoka Benki ya CRDB.
Kwa upande wao viongozi wa TCCCo, Swai na Kleruu, wanadaiwa kuwa kati ya Januari, 2014 na Desemba, 2015 walitumia madaraka yao vibaya na kununua mtambo wa kukoboa kahawa bila kufuata taratibu.
Wanadaiwa kununua mtambo huo kutoka Kampuni ya Brazafric ya Brazil na kuisababishia TCCCo hasara ya Sh bilioni 1.67.
Kama ilivyokuwa kwa vigogo wa KNCU, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi inayowakabili ni ya uhujumu uchumi, ambayo inapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu.
Kwenye maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, Julai mwaka jana jijini Mwanza, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali watu wenye nia ya kuhujumu jitihada za kuendeleza nguvu ya kuvifufua na kuviimarisha vyama vya ushirika nchini.
Alisema wizi na ubadhirifu wa rasilimali za ushirika kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama hivyo umerudisha nyuma maendeleo ya wanachama na wananchi kwa jumla.
“Naomba niwape salamu zenu – hakika hatuna mzaha katika hili, watu wamechezea mali za ushirika kwa sababu ya masilahi yao binafsi, naagiza usimamizi unakuwa wa kutosha na atakayehujumu jitihada za serikali huyo yatamkuta,” alionya waziri mkuu.