*Kwenye orodha wamo majenerali wa JWTZ
*Mboma, Sayore, Yona, Chenge, Mgonja ndani
*AG akiri kazi ni ngumu, aomba waongezwe muda
*Asema mwanga muhimu umeanza kuonekana
Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuchunguza Watanzania walioficha fedha kwenye mabenki ughaibuni, imeshawahoji vigogo, wakiwamo mawaziri wa zamani, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wanasiasa na wafanyabiashara maarufu.
Orodha ambayo JAMHURI imefanikiwa kuipata imeonesha kuwa miongoni mwa wanaotakiwa kutoa maelezo yao ni Mkuu mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Robert Mboma.
Mboma ameshawahi kuzungumza na gazeti hili na kusema hayumo kwenye mambo hayo, na akaapa kwamba akihusishwa kwa kuandikwa, atatafuta haki yake kisheria.
Pamoja naye, yumo Luteni Jenerali mstaafu, Gidion Sayore ambaye alikuwa Msaidizi Mkuu wa Jenerali Mboma. Baadhi ya majina mengine makubwa ni ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona; Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ilitakiwa iwasilishe taarifa yake bungeni Aprili, mwaka huu, lakini ilishindwa kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni kukutana na mambo mengi na mazito.
Kamati hiyo, baadhi ya wajumbe wanatoka Usalama wa Taifa, Polisi, wataalamu wa masuala ya benki na fedha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Benki Kuu ya Tanzania inawakilishwa na Mwanasheria aliyetajwa kwa jina la Mustapha Ismail. Baadhi ya watu wamekuwa wakiitwa kwa hati zinazosainiwa na mtu anayejitambulisha kwa jina la Mmari.
Orodha ya maswali wanayoulizwa watuhumiwa ni ndefu, yakiwamo ya idadi ya watoto, shughuli anazofafanya, kama ana akaunti nje ya nchi, kwa miaka mitatu amesafiri kwenda nchi gani, na kadhalika.
Hata hivyo, kumekuwapo maoni yanayokinzana kutokana na habari kwamba wanaohojiwa wengi ni wafanyabiashara ambao kwa kawaida wanaweza kuwa na akaunti nje ya nchi kutokana na shughuli zao. Wanasiasa ambao wengi wana ukwasi unaotajwa kwamba haulingani na mishahara na biashara zao, bado hawajatajwa kwa wingi.
Baadhi ya wabunge, akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), wamekwishahojiwa. Habari kutoka ndani ya Kamati hiyo zinasema baadhi ya wanaohojiwa wanapatwa na shinikizo la damu, hasa wanapoulizwa chanzo cha utajiri wao kiasi cha kuwawezesha kuwa na akaunti ughaibuni.
Pamoja na viongozi hao, JAMHURI imefanikiwa kupata majina karibu yote ya watuhumiwa wa wizi wa fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jaji Werema amekiri kuwa kazi ya kufuatilia jambo hilo ni kubwa, na kwamba Waziri Mkuu ataomba muda zaidi ili Kamati iendelee na uchunguzi.
Katika mahojiano yake na JAMHURI, Jaji Werema amesema, “Kazi ni kubwa, kubwa kuliko tulivyofikiria, bado tunaendelea. Kamati inapaswa iongezwe muda. Siwezi kukutajia majina ya tuliokwishawahoji kwa sababu miiko inakataza. Isitoshe, kuhojiwa kwenye Kamati siyo kwamba mtu ni mtuhumiwa au vinginevyo, tunafanya hivyo ili kupata taarifa zitakazotusaidia kuikamilisha kazi hii vizuri.”
Alipoulizwa kama anaona kuna mwelekeo wa kuwapo mafanikio, Jaji Werema alisema, “Mwelekeo upo, tunachoangalia, na kwa kweli tunachogundua ni mianya ya kutorosha fedha kwenda nje. Mianya ipo mingi. Kazi ni ngumu, msubiri tu wakati ukifika tutawapa taarifa.”
Anasema ugumu wa kazi, pamoja na mambo mengine, unatokana na namna ya kupata taarifa kutoka kwenye nchi ambako watu wanadaiwa kuweka fedha kwenye mabenki.
“Unapoandika barua kwenda huko ni lazima iwe na jina la mhusika, ujue namba ya akaunti yake, unaomba ujue hizo fedha zilitokea wapi na kama zina uhusiano na uchumi wako. Mafanikio kwenye kazi hii yanaweza kuwapo but we need (lakini tunahitaji) ushirikiano kutoka taasisi za nje na za ndani pia na watu binafsi. Kama ninyi waandishi wa habari mna taarifa, tafadhali sana tuleteeni,” anasema.
Amesema kazi ya kupata ukweli kuhusu ufichaji fedha ughaibuni inahitaji pia kuwahusisha wapelelezi wa kimataifa. “Hii ni kazi ngumu, huwezi kuanza leo ukaimaliza kwa wiki mbili au tatu.”
Hata hivyo, wapo wenye akaunti ughaibuni kutokana na kuwa wanafunzi au watumishi wa kada mbalimbali. Miongoni mwa wajumbe kwenye Kamati hiyo ni Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, ambaye anaelezwa kwamba ana akaunti nje na aliipata kutokana na utumishi wake kwenye Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Jaji Werema, kwa upande wake, anasema walikuwa makini kufuatilia mkutano wa Mataifa Tajiri (G8) uliomalizika hivi karibuni ambao pamoja na mambo mengine, ulizungumzia ufichaji fedha unaofanywa na raia wa mataifa mbalimbali.
Anatoa wito kwa Watanzania wote, kwa uwazi au kwa kutotaka kujulikana, kuwasilisha taarifa za uhakika za watu walioficha fedha ughaibuni.
“Watanzania walete taarifa, kama hutaki kujulikana wewe lete na sisi pale tuna watu makini hawatatoa siri za mtu. Hii kazi tunapaswa kushirikiana wote, hatuwezi kuifanikisha kwa kutoa list of shame Mwembeyanga. Majina hayo hayo yanazungumzwa kila mahali,” amesema Jaji Werema.
Mwanzo wa kuundwa Kamati
Mwishoni mwa mwaka jana mjadala mkali uliibuka bungeni baada ya Zitto kuwalipua baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali, akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010.
Kutokana na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili, 2013.
“Mbali na hilo napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma au mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalum na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema Zitto.
Pia Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai , Mauritus na maeneo mengine ziweze kurejeshwa.
Aliwataka Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata wapi na Takukuru wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.
Alipendekeza kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2013/2014 ianzishe kodi maalum ya asilimia 0.5 ya thamani ya fedha zilizotoroshwa ili kuweka rekodi za uhakiki fedha za ndani na zinazotoka nje.
Mbunge huyo alisema mazungumzo yake na wachunguzi wake binafsi, kiwango cha fedha kinachomilikiwa na Watanzania nchini Uswisi peke yake ni takriban mara 20 ya kiwango kilichotangazwa na benki ya taifa ya nchi hiyo.
Alisema fedha hizo ni sehemu tu ya fedha ambazo Watanzania wamezificha katika benki mbalimbali za nje.
Alitoa mfano wa Benki ya UBS peke yake iliyopo katika nchi hiyo, ina maofisa 240 ambao wanashughulikia wateja wa Tanzania na kila ofisa mmoja husimamia mteja mmoja mwenye kiwango kisichopungua dola za Marekani 10 milioni.
Zitto alisema Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola milioni 196 za Marekani zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za benki za nchi hiyo.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema hata kama ni Rais aliyeko madarakani au Waziri Mkuu ama kiongozi yeyote atajwe bungeni ili Bunge limwondolee kinga aburutwe mahakamani.
Alimtaka Zitto kuwataja kwa majina watu hao ili wachukuliwe hatua.
Kwa upande wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Cahdema), aliwataja marehemu Daudi Ballali, Andrew Chenge na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, kwamba walihusika na tuhuma za ufisadi wa Tan Gold, hivyo Bunge linapaswa kuchukua hatua.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alitaka watu walioficha fedha nje ya nchi watajwe kwa majina ili wananchi wawafahamu. Mpina aliwahi kuwasilisha hoja ya kuwapo mabilioni yaliyofichwa nje ya nchi na baadhi ya Watanzania.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema wapo Watanzania wanaotoa fedha nyingi kwenye uchaguzi na kutoa misaada mbalimbali kiasi cha kuiharibu nchi, hao peke yake wanatosha kudhihirisha kwamba ni mafisadi walioficha fedha nje.
Zitto anasema taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonesha kuwa baadhi ya fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo hapa nchini.