Rugemalira

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mgogoro wa ubia katika kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited baina ya Mechmar kutoka Malaysia na VIP Engineering and Marketing Limited (VIP), ndiyo uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania, maarufu kama Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika kumiliki IPTL ni wazi kwamba Mkurugenzi wa VIP, James Burchard Rugemalira, aliingia ubia kwa kuchukua hisa tatu na kufanya awe na asilimia 30, huku Mechmar ikichukua hisa saba na kuifanya iwe na asilimia 70.


Kwa hiyo, kutokana na yeye kuwa na asilimia ndogo kwenye IPTL, ikawa hana sauti katika manejimenti ya kampuni hiyo ya kufua umeme nchini tangu kusimika mitambo yake eneo la Tegeta kwenye Barabara ya Bagamoyo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kuletwa kwa mitambo hiyo kulitokana na Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania (TANESCO) kuingia mkataba na IPTL kuiuzia umeme wa migawati 100 kufuatia tatizo la umeme lililotokana na uhaba wa maji ya kuendesha mitambo ya umeme kwenye Bwawa la Mtera huko Dodoma.


Kwa mujibu wa mkataba huo, TANESCO ililazimika kulipa tozo la ziada (capacity charge) kwa IPTL hata kama kampuni hiyo haizalishi umeme wa kuiuzia shirika hilo. Kwa hiyo, shirika hilo likawa linalipa tozo hiyo na manejimenti ya IPTL ikawa haijali kutoa taarifa kwa Rugemalira kuhusu mapato na matumizi ya shughuli zake za kila mwaka kati ya mwaka 1995 na 2002.


Tuelewe kuwa Rugemalira ndiye aliyewakaribisha wawekezaji hao kutoka Malaysia kwa nia nzuri ya kuliwezesha Taifa letu liondokane na tatizo la umeme. Lakini vizito wa Mechmar kwa kushirikana na vigogo wa Wizara wa Nishata na Madini wakamzidi akili. Hivyo, Rugemalira aliona bora apeleke suala lake katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.


Ni baada ya VIP kufungua shauri lake dhidi ya IPTL na Mechmar mwaka 2002, ambapo mimi niliweza kuripoti maendeleo ya kesi hiyo kwenye magezeti ya Financial Times, the Guardian na Sunday Observer. Ni katika kufuatilia mwenendo wa shauri hilo kwa karibu niligundua na kuripoti jinsi IPTL ilivyokuwa ikilipisha dola 3.60 za Marekani kama tozo ya ziada kila megawati kwa mwezi wote badala ya dola 2.60 za Marekani.


Naamini kasoro hiyo ndiyo iliyomsukuma Rugemalira kufikisha shauri lake kortini na hatimaye kuwezesha TANESCO nayo ifunguke na kulazimika kufungua kesi yake dhidi ya IPTL na Mechmar kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Ufumbuzi wa Migogoro ya Kibiashara huko Uingereza. Uamuzi wa Mahakama hiyo ndiyo uliowezesha kuwapo kwa Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania.


Kusema kweli, fedha zilizowekwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa kati ya TANESCO na IPTL, kwani fedha halisi za IPTL ni dola 2.60 za Marekani kama tozo ya ziada kwa kila megawati kwa siku, huku fedha ya TANESCO ikiwa ni dola 1.00 ya Marekani iliyozidi kwenye tozo ya ziada hiyo. Mtu yeyote mwenye hekima anajua hivyo.


Kadhalika, mtu yeyote mwenye hekima anajua kuwa katika dola 2.60 za Marekani kwa IPTL, VIP ya Rugemalira ilistahili kulipwa asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia kubakiwa na alimia 70 nyingine. Lakini, kulingana na fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, tunaambiwa VIP ya Rugemalira iliambulia dola za Marekani 75 milioni tu badala ya kulipwa dola za Marekani 600 milioni.


Kutokana na VIP kulipwa fedha hizo, Rugemalira alipata fedha za Kitanzania zinazofikia Sh. 120 bilioni na kuweza kulipa kiasi cha Sh. 38,000,000.00 kama kodi kwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA). Hata hivyo, fedha hizo alizolipwa kihalali kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndizo zinazopigiwa kelele!
Kuna fedha za kufuru zilizopelekwa kwenye Stanbic Bank kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow hazipigiwi kelele. Fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya PAP wakati kampuni hiyo haikuwa moja ya wabia wa IPTL. Tunaelezwa ni dola za Marekani 231 milioni zilizochotwa kutoka akaunti ya PAP kwenye Stanbic Bank iliyoko makutano ya Barabara ya Kinondoni na Ali Hassan Mwinyi jinini Dar es Salaam.


Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inatuthibitishia kuwa Akaunti ya Tegeta Escrow ilikuwa ikitunza fedha ambazo TANESCO ilikuwa ikiilipa IPTL hadi migogoro yake imalizike. Kwa hiyo, mwafaka ulivyofikiwa mbele ya Jaji John Utamwa wa Mahakama Kuu ndipo VIP ya Rugemalira ilipoweza kulipwa dola za Marekani 75 milioni kutokana na ubia wake wa asilimia 30 katika IPTL.


Sasa tujiulize, PAP ililipwaje dola za Marekani 231 milioni wakati haijawahi kuwa miongoni mwa wabia wa IPTL? Na kwanini waliokwapua fedha hizo kupitia PAP hawajashtakiwa na wala kufikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Watumishi wa Umma?
Kadhalika, tunaambiwa kuwa PAP ilinunua hisa za Mechmar katika IPTL kwa dola za Marekani 6 milioni, lakini ikalipa fedha kiduchu za kuhamisha hisa hizo kwenye Mamlaka ya Usajili na Leseni (BRELA). Pia tunaelezwa kuwa PAP ilidanganya katika kuilipa TRA kodi kidogo sana, huku baadhi ya maofisa wa TRA wakitolewa kafara. Na baada ya kufungua akaunti kwenye Stanbic Bank, ndipo fedha zote za Tegeta Escrow zikalundikwa kwenye akaunti yake na kugombewa na vigogo kama kunguru wagombeavyo mzoga.


Wananchi hawataelewa kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) haitachukua hatua za dhati dhidi ya wote waliohusika na uchotaji wa dola za Marekani 231 milioni kwenye Stanbic Bank kwa sababu ni fedha ambazo baadhi yake ni za TANESCO na nyingine zikiwa za IPTL.
Tunasubiri kwa hamu kuona vigogo waliohusika na uchotaji wa fedha hizo kupitia PAP wakifikishwa kortini.

Mwandishi wa makala hii ni mwanahabari mkongwe, anayeishi Dar es Salaam. Anapatikana kwa namba ya simu 0769 989 164.