Kashfa nzito imeukumba Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), baada ya baadhi ya walinzi wake kudaiwa kujihusisha na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.
Imedaiwa kuwa walinzi hao wanapomaliza kufanya matukio hayo yakiwamo ya utekaji na uporaji, fedha zinazopatikana huzitumia kuwaziba midomo baadhi ya viongozi wa vyombo vya dola wasiwafikishe katika mkono wa sheria.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya GGM, vimeiambia JAMHURI kuwa mara nyingi ujambazi unaofanywa na walinzi hao huwa umepata baraka za baadhi ya viongozi wao katika idara ya ulinzi mgodini hapo, ambao inadaiwa kuwa ndiyo wamekuwa wakifunika tuhuma kwa kuwanyamazisha baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Habari zinasema wananchi wanaopita jirani na mgodi huo kwenye barabara itokayo mjini Geita kuelekea Kijiji cha Nungwe na Nyakabale, wengi wao wakiwa ni wachimbaji wadogo wadogo, wamekuwa wakiporwa fedha na mawe yanayodaiwa kuwa ni dhahabu.
Katika tukio la Februari 22, mwaka huu, majira ya jioni, walinzi hao waliokuwa na bunduki walidaiwa kumteka Ramadhani Mashaka (24), mkazi wa Mtaa wa Misheni mjini Geita, kisha kumpora Sh milioni 1.5.
Mashaka alikuwa akitokea mjini Geita kuelekea Kijiji cha Nyakabale kupitia barabara ya Nungwe kupeleka malipo ya wafanyakazi wa kaka yake wanaochenjua mchanga wa dhahabu kijijini hapo.
Vyanzo vya habari vimesema Mashaka alivamiwa na walinzi watano wakiwa wamevalia sare za kazi za mgodi huo, ambapo wawili kati yao walimweka chini na kumwamuru kulala kifudifudi huku wakimtisha kumuua.
Baadaye walinzi hao ambao wametajwa kwa majina ya Maneno Nangi na John Magige, walimpora Mashaka kiasi hicho cha fedha, kisha kumwamuru atoweke.
Watuhumiwa wakamatwa, waachiwa
Hata hivyo, hawakuweza kufungua kesi kwa siku hiyo, badala yake ilifunguliwa Februari 25 baada ya kujiridhisha waliomteka na kumpora ni wafanyakazi wa GGM, ambapo baadaye Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa wote wawili na kuwaweka rumande.
Hata hivyo, katika mazingira yanayodaiwa kutawaliwa na rushwa, watuhumiwa hao waliachiwa muda mfupi baadaye na kutoka wakitamba kuwaweka mfukoni baadhi ya askari wasio waaminifu.
“Yaani hawakukaa sana kituoni hapo… baada ya muda walitoka huku wakitamba kwamba hawakuanzia kwetu, ni wengi wamekwishawafanyizia na hakuna walichofanywa, na kumtaka jamaa waliyempora awe mpole vinginevyo yeye ndiye atakayewekwa rumande,” kimesema chanzo chetu.
Mlalamikaji abambikiwa kesi, akamatwa
Katika hali inayothibitisha tambo hizo za watuhumiwa hao, Februari 27, ikiwa ni siku mbili baada ya watuhumiwa hao kuachiwa, mlalamikaji [Ramadhani] alikamatwa na askari polisi mmoja (jina limehifadhiwa) na kubambikiwa kesi ya wizi wa pikipiki, tukio lililotokea katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, na kuwekwa mahabusu ya polisi akisubiri kusafirishwa kwenda Kahama kujibu tuhuma hizo.
Akiwa mahabusu ya polisi, kaka yake, Maganga, alipata taarifa na kuamua kwenda kulalamika kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paul, na baadaye aliruhusiwa kumdhamini baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya saa nne.
Kutokana na tukio hilo la mlalamikaji kubambikiwa kesi, Kamanda Paul alimwamuru Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Geita, Busee Bwire, kuchunguza tukio hilo, ambapo inadaiwa upelelezi ulibaini kuwa Ramadhani hakufanya wizi wa pikipiki wilayani Kahama na kwamba alibambikiwa kesi hiyo kumtisha asifuatilie kesi yake ya kutekwa na kuporwa mali.
Kwa mjibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, tayari askari aliyehusika kumkamata Ramadhani na kumbambikia kesi amekwishafunguliwa jalada la uchunguzi.
Habari zaidi zinadai kuwa baada ya kumalizika kwa kesi aliyobambikiwa, jalada la kesi ya awali liliwasilishwa kwa Mwanasheria wa Serikali, Kilie, ambaye pia alilipitia na kulirudisha Polisi kwa maelekezo kwamba watuhumiwa ambao ni walinzi wa GGM wafikishwe mahakamani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya jalada namba GE/IR/856/2014.
Machi 8, mwaka huu saa sita mchana, OCD wa Geita, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) wa Geita, Saimon Pasua, watuhumiwa, viongozi wa ulinzi wa GGM na mlalamikaji walizuru eneo la tukio na kubaini kuwa unyang’anyi huo ulifanyika nje ya mgodi na si ndani ya mgodi kama ilivyodaiwa na watuhumiwa hao.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa Machi 14, mwaka huu watuhumiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Geita.
Watuhumiwa watoroshwa mahakamani
Hata hivyo, wakiwa mahakamani hapo wakisubiri kusomewa shitaka linalowakabili, ghafla watuhumiwa hao waliondolewa na askari polisi wakarudishwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita.
Walipokwenda kuuliza sababu ya walalamikiwa wao kuondolewa mahakamani kabla ya kusomewa shitaka, hawakupata msaada wowote zaidi ya kurudishwa kwa RCO Saimon Pasua ambaye naye aliwarudisha kwa RPC.
Kutokana na maelekezo ya RCO Pasua, Machi 17, Ramadhani na kaka yake, Maganga, walifika ofisini kwa Kamanda Paul, lakini hawakumkuta na walipompigia simu alidai yuko mkoani Mwanza kikazi na hadi anahamishiwa mkoani Morogoro hivi karibuni, hakuna hatua zozote zilizokwisha chukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Kijana aliyetekwa azungumza
Kijana Ramadhani alipohojiwa na JAMHURI alikiri kutekwa na kuporwa mali na walinzi hao wa GGM na kwamba umaskini wake ndiyo umesababisha haki kutotendeka kutokana na walalamikaji wake kutuhumiwa kutumia fedha kujinasua kwenye tuhuma hizo.
“Nikwambie tu kwamba hawa watu wametumia fedha nyingi kujinasua… Huyu aliyekuwa RCO alitaka haki itendeke, lakini kila alipokuwa akijaribu alishindwa maana wale watu walikuwa karibu na bosi wake. Unavyoniona nimeamua kukaa kwa wasiwasi, sijui hatima yangu maana hawa watu wameshaniahidi nikiendelea kuwafuatafuata nitakiona cha moto, hivyo naogopa, naomba mamlaka za juu zinisaidie nipate haki yangu,” amesema Ramadhani.
Afisa habari GGM akwepa mwandishi
Kwa upande wake, Afisa Habari wa GGM, Tenga Bill Tenga, alipotafutwa ili atoe ufafanuzi wa tuhuma zinazoelekezwa kwa walinzi wa mgodi huo, simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi (SMS) hakujibu.
Naye Mwanasheria wa Serikali, Kilia, alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi iwapo faili hilo liliwasilishwa ofisini kwake na kulitolea ufafanuzi wa kisheria, hakupatikana kwa kile kilichodaiwa ametingwa na majukumu ya kikazi.
RPC Joseph Konyo atangazia kiama
JAMHURI ilipomfuata Kamanda mpya wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo, ili kujua iwapo amekwishapata taarifa zozote kuhusiana na jalada hilo, alikiri na kusema atahakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani, huku akisisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
“Tena imekuwa vizuri kufika ofisini kwangu, unaliona hili jalada ndiyo la hao watu unaowaulizia, nimeshaanza kulifanyia kazi na nitamwita huyu kijana aliyetendewa nitamhoji, nitawakamata watuhumiwa nao tutawahoji, lakini nakuhakikishia tu kwamba sintokubali kurithi migogoro, nitatenda haki na ninakuhakikishia hawa watafikishwa mahakamani maana hakuna aliye juu ya sheria,” amesema Kamanda Konyo.
Askari atekwa, RPC amkingia kifua mtuhumiwa
Tukio jingine linalofanana na hilo, ni la mwaka 2012 wakati Leonard Paul akiwa RPC Geita.
Askari polisi mwenye namba G7109, PC Mashauri Richard wa Kitengo cha Usalama Barabarani wilayani Geita, alinusurika kuuawa baada ya kudaiwa kutekwa, kuporwa gari na mfanyabiashara maarufu wa dhahabu mjini hapa.
Pia askari huyo alipewa kipigo kilichosababisha kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye paji la uso upande wa kulia.
Imeelezwa kuwa baada ya kipigo hicho mfanyabiashara huyo aliyetajwa kwa jina moja la Majaliwa, alimnyang’anya askari huyo ufunguo wa gari lenye namba T778 AVB aina ya Toyota Mark II kisha kutokomea nalo kusikojulikana.
Tukio hilo lilijiri Novemba 22, 2012 saa 11 jioni katika Mtaa wa Nyanza jirani na Benki ya NMB Tawi la Geita, wakati askari huyo alipomaliza kula chakula cha mchana kwenye mgahawa unaojulikana kwa jina la Technition.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, mbali ya mfanyabiashara huyo kukamatwa na kufunguliwa jalada la uchunguzi namba GE/RB/4950/2012 (unyang’anyi wa kutumia silaha), aliachiwa katika mazingira ya kutatanisha.
PC Mashauri alisema, “Nikiwa nageuza gari nilishtukia nikipigwa ngumi na kukabwa kisha kuoneshwa bastola na nikaamuriwa niwape watu hao funguo za gari, nikafanya hivyo, wakanipiga sana, wakatoweka.
“Baadaye nilikimbilia kituoni kutoa taarifa kwamba nimetekwa na kuporwa gari na watu wasiojulikana, nikaenda hospitali ya Geita ambako nililazwa kutokana na maumivu ya kipigo nilichopewa.”
Uchunguzi ulibaini kuwa baada ya PC Mashauri kufika kituoni, alipokewa na askari mwenye Namba G 8088 PC Masanja ambaye alichukua maelezo yake kisha kufungua jalada kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Mmoja wa askari kituoni hapo alidai kwamba kitendo cha mtuhumiwa huyo kuachiwa kimesababisha kuwapo kwa uhusiano mbaya kati ya askari wenye vyeo vidogo na viongozi wa ngazi za juu.
Hata hivyo, tukio hilo mbali ya kuwa mezani kwa aliyekuwa RPC Geita, Leonard Paulo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa, lakini baadaye askari polisi aliyetendewa uovu huo alihamishiwa kituo cha kijijini.