Rais Dk. John Magufuli, ameombwa aingilie kati sakata la mauji ya meneja wa baa ya Mo-Town ya mjini Moshi, James John aliyeuawa kikatili na wafanyabiashara wanne ndugu ambao hadi sasa wanatamba mitaani.
John aliuawa Juni 9, 2009 katika kijiji cha Kindi kilichopo Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.
Katika barua yao kwenda kwa Rais Magufuli, ndugu wa marehemu, Beda Massawe na Peter Massawe, wanamwomba Rais aagize uchunguzi wa mauaji hayo uanze upya bila kuwashirikisha askari wa upelelezi kutoka Ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Chanzo cha barua hiyo kwenda kwa Rais Magufuli ni kutokana na familia hiyo kushindwa kupata msaada kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Watuhumiwa hao ambao hadi sasa hawajakamatwa ni John Joseph Kisoka (Magazeti), Mussa Joseph Kisoka, Deo Joseph Kisoka na Lucas Joseph Kisoka; ambao walitoroka baada ya mauji hayo hivyo kesi hiyo kufutwa mwaka 2012.
“Tunakuandikia barua hii tukiwa wanyonge na tuliokata tamaa kutokana na namna watuhumiwa wanne tuliowashuhudia wakimuua ndugu yetu James John mnamo Juni 09, 2009 wakiwa mitaani huku jalada la polisi la uchunguzi likipotea au kuibwa,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Familia hiyo imehoji nguvu waliyonayo watuhumiwa hao hadi kuweza kula njama na kuweza kuiba majalada yote yahayohusiana na mauaji hayo.
Inadaiwa kuwa jalada hilo lilikuwa limesheheni maelezo ya mashahidi muhimu sita ambao ni Alfonsina John, Ludovick Munisi, Lelo Selengia, Peter Gerald, Boniface Munishi na Fulgence Gerald, lakini maelezo hayo yote yalinyofolewa kwa lengo la kuwalinda watuhumiwa.
Familia ya ndugu wa marehemu imemwomba Rais Magufuli afanye mambo matatu ya kuliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwakamata wafanyabiashara hao ili kuepusha kuvuruga upelelezi; kuunda tume kuchunguza mazingira ya kuibwa kwa jalada la polisi la uchunguzi pamoja na majalada madogo ya shauri hilo; na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliofanya hujuma hiyo.
Wameomba uchunguzi huo usihusishe askari wa Kilimanjaro ambao ndiyo watuhumiwa kama ilivyofanyika wakati wa uchunguzi wa mauji ya yaliyofanywa na mfanyabiashara Abubakar Jaffar (JJ) mwaka 2002
HISTORIA YA SAKATA HILI
Faili kesi ya mauaji ‘lapotea’ Moshi
Jalada la kesi ya mauaji ya Meneja wa Baa ya Mo-Town mjini Moshi, James John Massawe, limepotea katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kilimanjaro.
Massawe aliuawa Juni 9, 2009 katika Kijiji cha Kindi Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kutekwa,
Jalada hilo la uchunguzi lilikuwa limesheheni ripoti zinazoeleza jinsi wafanyabiashara wanne ndugu walivyoshiriki katika mauaji hayo.
Vilivyopotea ni pamoja na maelezo ya mashahidi sita, huku ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ambayo ndani yake inaeleza sababu za kifo hicho nayo ikidaiwa kupotea.
Kutokana na hali hiyo, familia ya marehemu Massawe, imemwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, ikimuomba aingilie kati jambo hilo kutokana na kile familia hiyo inachodai kuwa ni kushindwa kwa jitihada zao za kulishawishi Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa hao.
Familia hiyo imeainisha mambo manne ambayo yanalifanya Jeshi la Polisi kutowakamata watuhumiwa, likiwamo la kwamba jalada halisi la kesi hiyo limeibwa ikiwa ni mpango mahsusi uliosukwa na baadhi ya maofisa katika ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Inadaiwa kuwa maelezo ya mashahidi sita muhimu yaliondolewa na maofisa hao kwa makusudi katika jalada lililopelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gama amethibitisha kupokea barua ya malalamiko kutoka kwa wanafamilia wa Massawe ambao ni Beda Massawe na Peter Massawe.
Gama ameliambia JAMHURI kwamba suala hilo analifanyia kazi kwa uzito unaostahili.
Katika barua hiyo, inaelezwa kwamba mashahidi ambao maelezo yao yamenyofolewa kwa lengo la kuwalinda watuhumiwa hao ni ya Alfonsina John, Ludovick Munisi, Lelo Selengia, Peter Gerald, Boniface Munishi na Fulgence Gerald.
“Ni kwa msingi huo, tunakuomba utumie mamlaka yako kumuomba IGP afuatilie mahali lilipo jalada la kesi hii na kama limeibwa kama ambavyo tumedokezwa, basi wahusika wote watafutwe na kufunguliwa mashitaka ya kijeshi kwa kulidhalilisha Jeshi la Polisi,” inasema sehemu ya barua hiyo ambayo JAMHURI ina nakala yake.
Familia inamuomba Gama aamuru uchunguzi ufanyike upya bila kuwashirikisha maofisa wa polisi wa Ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Mauaji yalivyofanywa
Massawe anadaiwa kutekwa katikati ya Mji wa Moshi na wafanyabiashara ndugu wanaomiliki vitega uchumi kadhaa katika Jiji la Mwanza na kupelekwa katika moja ya nyumba za wafanyabiashara hao eneo la Kibosho ambako inadaiwa alipewa mateso hadi kuuawa.
Baada ya mauaji hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko aliueleza umma kuwa Massawe aliuawa na wananchi, lakini baada ya kelele nyingi kupigwa na familia, hatimaye aliyataja majina matatu ya wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuhusishwa na mauaji hayo.
Wafanyabiashara hao ambao baada ya mauaji hayo walikwenda mafichoni nje ya nchi, walitajwa na Kamanda Ng’hoboko kuwa ni John Joseph Kisoka (Magazeti) na wadogo zake Musa Joseph Kisoka na Deo Joseph Kisoka.
Hata hivyo, pamoja na wafanyabiashara hao kutajwa na Kamanda huyo na kutangaza kuwasaka, Jeshi la Polisi liliishia kuwakamata vijana wawili, Idrisa Hassan Munishi na John Mallya (Small Boy) na kufikishwa mahakamani ambako walishitakiwa kwa mauaji ya Massawe.
Vijana hao walifikishwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Makahama Kuu Kanda ya Moshi, Stella Mugasha katika shauri la jinai namba PI 9/2009, lakini Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawe aliliondoa shauri hilo mahakamani.
Kiini cha kutekwa kwa kijana huyo kinatokana na madai ya wafanyabishara hao kwamba Massawe alihusika na mauaji ya mama mzazi wa wafanyabiashara hao, Martha Kisoka (68) aliyeuawa na watu wasiojulikana Mei 2009 baada ya kuvamiwa nyumbnai kwake Kindi, Kibosho.
Mwaka 2007, Massawe na wenzake wanne walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba nyumbani kwa ajuza huyo, lakini mwaka 2008 waliachiliwa huru baada ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo.
Katika barua yao ya Oktoba 7, mwaka jana kwenda kwa DPP, familia hiyo inalalamika kutokamatwa kwa watu muhimu kwenye mauaji ya Massawe lakini pia wakihoji kigezo kilichotumika kuwaachilia huru baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo.
Barua hiyo ya familia iliyotiwa saini na Beda Massawe kama Msemaji wa Familia na Peter Lelo Massawe, inadai kuwa kifo cha ndugu yao kilikuwa cha kinyama kwani alitekwa na kupelekwa umbali wa kilometa 15 ambako aliteswa kwa kupigwa huku akiwa amening’inizwa kichwa chini miguu juu na kuingizwa chupa ya bia katika sehemu ya haja kubwa.
Baada ya barua hiyo kumfikia DPP ilipelekwa moja kwa moja Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ambako ofisi hiyo ilimwandikia barua Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ikimtaka afuatilie malalamiko hayo haraka ili abaini ukweli.
“Inspekta Jenerali wa Polisi anakuagiza ufanye ufuatiliaji wa haraka kuhusiana na lalamiko hilo ili kubaini ukweli iwapo kuna ukiukwaji wa maadili wakati wa kushughulikia lalamiko hilo na umjulishe matokeo kabla ya tarehe 30/10/2014,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Oktoba 9, mwaka jana.
Barua hiyo iliyosainiwa na S.M. Ambika ambaye ni Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACPA) nakala yake ilipelekwa kwa Beda Massawe wa kijiji cha Kindi, Kibosho ikimtaarifu kufika ofisi ya DCI kwa ajili ya kupata kile kilichoelezwa kwenye barua hiyo kuwa ni ufumbuzi wa suala lake.
Akizungumza na JAMHURI, Beda amesema kuwa licha ya kwenda mara kwa mara ofisi ya RCO Mkoa wa Kilimanjaro, wamekuwa wakipewa matumaini hewa kwamba suala lao linashughulikiwa, lakini wanachoambulia ni kuwaona watuhumiwa wakitamba mitaani na kuwatolea lugha za kejeli.
Amesema kuwa hivi sasa wameanza kukosa imani juu ya maendeleo ya kesi ya mpendwa wao na kuiomba ofisi hiyo ya DCI kuwapa msaada zaidi baada ya ofisi ya RCO Kilimanjaro kutowapa ushirikiano.
Kutokana na danadana hizo wanazozipata kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi wengi, familia hiyo imemwandikia tena barua DCI ikimuomba asikilize kilio chao juu ya malalamiko hayo.
“Kwa barua hii, tunakuomba upitie kumbukumbu ya malalamiko yetu na kutuambia hatua iliyofikia au inayotakiwa kufuata ili walau haki ionekane ikitendeka juu ya malalamiko ya ndugu yatu,” inasema sehemu barua ya familia hiyo ya Machi 10, mwaka huu.
Beda anahoji iweje iwe rahisi kwa polisi kuwakamata waandamanaji na kuwafikisha mahakamani, lakini iwe vigumu kwa polisi kuwakamata watuhumiwa wa mauaji.