Na Stella Aron, JamhuriMedia, Bagamoyo
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mapinga, Johaness Nyambaza, anadaiwa kwenda shuleni akiwa na panga analoliweka ndani ya begi.
Kitendo hicho kinadaiwa kuwasababishia walimu na wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani kusoma na kufundisha katika mazingira magumu.
Awali inadaiwa kulikuwa hakuna kitendo hicho lakini tangu kutokea kwa ugomvi kati yake na Mwalimu Shaban Kivamba kumekuwa na sintofahamu hali iliyosababisha kuibuka kwa mgawanyo shuleni hapo.
Ugomvi huo umeibua makundi mawili ya walimu moja likifahamika kwa jina la Kanda ya Ziwa na jingine kwa jina la Pwani.
Walimu wa Kanda ya Ziwa wanadaiwa kuwa nyuma ya Nyambaza anayetoka Kanda ya Ziwa na wengine wako nyuma ya Kivamba anayetoka Pwani.
Ugomvi wa walimu hao umefikia hatua ya kushikana mashati mbele ya wanafunzi, walimu na wazazi waliofika kupata huduma shuleni hapo na tayari umefika katika vyombo vya juu vya sheria.
Chanzo cha ugomvi
Katika uchunguzi uliofanywa na JAMHURI, umebaini kuwa ugomvi wa walimu hao ulianza tangu mwaka 2023 baada ya Kivamba kutaka kuwaadhibu wanafunzi waliotoka nje ya shule bila ruhusa na kwenda kununua mahitaji yao katika duka linalomilikuwa na Nyambaza.
Kitendo cha Kivamba kutaka kuwaadhibu wanafunzi hakikubaliwa na Nyambaza anayemiliki duka hilo na aliwaamuru wanafunzi zaidi ya wanane waliopigishwa magoti kusimama na kwenda darasani.

Kutokana na hatua hiyo, Kivamba aliona anadhalilishwa mbele ya wanafunzi huku Nyambaza akiona wanafunzi wanaonewa ndipo wakaanza kurushiana maneno na kutoleana lugha chafu huku kila mmoja akiona yupo sawa hali iliyosababisha taharuki.
Walimu hao waliendelea kujibizana na kufikia hatua ya kuvutana na kushikana nguo na kusababisha vurugu kubwa shuleni hapo na baadhi ya walimu walifanya jitihada za kuamulia lakini ilishindikana.
Kutokana na mzozo huo, walimu walitoa taarifa ofisi ya kata ya mgambo na baada ya dakika kadhaa walifika eneo la shule na kisha kuwakamata walimu hao na kuwafikisha Kituo cha Polisi cha Mapinga.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Kivamba alifungua shtaka la jinai katika Mahakama ya Mwanzo Kerege na kesi hiyo iliunguruma kwa kipindi cha miezi mitatu na katika hukumu iliyotolewa Nyambaza alikuwa mshtakiwa hakukutwa na hatia.
Pia uchunguzi umebaini kuwa baada ya hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwaka juzi, Nyambaza aliamua kuandika barua ya malalamiko na nakala kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Shule, Ofisa Elimu Sekondari na kwa Kivamba iliyotoa siku 90 tu akilalamikia mambo zaidi ya sita ambayo ni kudhalilishwa, kuwekwa mahabusu kwa lazima na kushtakiwa kwa hila.
Pia alipatwa na mfadhaiko wa kiakili, taharuki na mfahadhiko katika familia yake kwa madai kuwa hali hiyo imesababishwa na Mkuu wa Shule, Albert Mganga na Kivamba, kutumia vibaya madaraka yao na kumdhalilisha na alitaka kuombwa radhi kwa barua.
Pia aombwe radhi hadharani mbele ya wanafunzi na walimu kama njia ya kumrejeshia heshima kwa wanafunzi, walimu wenzake na wazazi.
Pia ameomba kulipwa Sh milioni tani alizotumia kesi na pia alipwe fidia ya Sh milioni 295 na asipotekelezeka hayo atafikisha shauri la madai mahakamani.
Pia JAMHURI imebaini kuwa kutokana na mwenendo wa mgongano huo, taarifa zilifika Ofisi ya DED, Tume ya Utumisi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Bagamoyo na walimu hao walipewa adhabu ya kupumzishwa kutekeleza majukumu yao ya ualimu.
JAMHURI inayo nakala ya barua hiyo iliyowataka walimu hao kwa kutumia Kanuni ya 37 (1) za Kanuni ya Tume ya Utumishi wa Umma kupumzika kutekeleza majukumu aliyopangwa ya kiualimu kuanzia kwa barua hiyo wakati shauri linapitia mchakato wa kisheria.
Walimu wazungumza
Akizungumza na JAMHURI, mwalimu wa shule hiyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini, amesema mgogoro wa Nyambaza naKivamba ni wa muda mrefu na umesababisha kuwapo wa mambo yasiyo na tija kwa maendeleo ya shule.
“Hapa walimu tupo makundi mawili moja linalomtetea Nyambaza na lingine linalomtetea Kivamba. Hii imesababisha baadhi ya mambo kukwama kutokana na kutokuwapo kwa umoja.
“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2023 kipindi hicho hata huyu mkuu wa shule hakuwepo ndipo ambapo ugomvi ulipoanza ambapo pia ulimusisha mwalimu mkuu aliyeondoka na hadi leo bado unaendelea hivyo ninaamini wewe mwandishi utatusaidia kufikisha kero hii kwa ngazi za juu ili hatua zichukuliwe.
“Mgogoro huu umefika hadi mahakamani sasa hapo ni hatua mbaya kwani inatakiwa sisi walimu wa tuwe kitu kimoja na kushirikiana ili kuongeza ufaulu katika shule hii lakini sasa tumekuwa ni maadui na hata kufudisha katika mazingira magumu,” amesema huku akisisitiza kuwa wahusika walitafutie ufumbuzi suala hili.
Mwalimu mwingine (jina tunalihifadhi) amesema ili mgogoro huo umalizike ni vyema walimu hao wakahamishwa kwa kila mmoja kwenda shule nyingine na itasaidia kupunguza maneno kwani kila siku kunaibuka jipya na sasa itafika wakati watu watachoka na kuchukua uamuzi usio sahihi.
“Siku ya tukio nilikuwepo hapo nje nikiwa na walimu wengine wanne, nilimuona Kivamba akiwa ameshika fimbo na kuwaamuru wanafunzi waliokuwa nje kimakosa kupiga magoti kama utaratibu wetu ulivyo na pia muda huo walitakiwa kuwa darasani,” amesema na kuongeza:
“Wanafunzi hao walikuwa mkononi wameshika juisi na wengine maji walikuwa wakitoka kwenye duka la Nyambaza lililopo karibu na shule kununua mahitaji.
“Wakati tunaendelea kumwangalia mwalimu ghafla tukamuona Nyambaza amefika eneo alipokuwapo Kivamba na akawaamuru wanafunzi waliopewa adhabu ya kupiga magoti kunyanyuka kwenda darasani ndipo ugomvi ulipoanza na uliamriwa na walimu na wazazi waliofika shuleni kupata huduma na kusababisha vurugu kubwa,” amesema.
Mwanafunzi anena
Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu (jina linahifadhiwa) amesema siku ya tukio alikuwapo shuleni hapo na alishuhudia vurugu hizo zilizosababisha na wanafunzi kutoka madarasani.
“Siku ya tukio nilikuwa mmojawapo niliyepigishwa magoti na Kivamba na siku hiyo alikuwa ameshika fimbo, nilikwenda kununua juisi katika duka la Nyambaza pamoja na wanafunzi wengine na wakati tunarudi Kivamba alituona akatuamuru tupige magoti na wakati huo kengele ya darasani ilishagonga, ghafla alitokea Nyambaza na yeye alituamuru wote tunyanyuke.
“Wakati tunatafakari tufanye nini na wanafunzi wenzangu walimu hao waliendelea kujibizana na kutoleana lugha chafu na sisi tuliamrishwa na Nyambaza kukimbia darasani wote tulinyanyuka na kukimbia huku nyuma walimu waliendelea kujibizana,” amesema.
Naye mwanafunzi wa kidato cha nne (jina linahifadhiwa) amesema mbali ya tukio hilo kutokea na kusababisha mtafaruku lakini imepita miezi kadhaa walimu hao walitaka kupigana wakati mwalimu mmoja akitoka kufundisha na mwingine akitaka kuingia darasani na kugongana vikumbo kwenye chumba cha darasa.
“Walimu hawa hawana uhusiano mzuri ni vyema viongozi wetu wakakaa nao na kujadiliana namna ya kumaliza ugomvi huu kwani tunapata taarifa kuwa wamefikishana mahakamani na wakidaiana mamilioni ya fidia jambo ambalo si zuri,” amesema.
Ofisa elimu atoa kauli
Ofisa Elimu Kata ya Mapinga, Franco Zemba, amekiri kuwapo kwa ugomvi huo lakini amesema hawezi kuuzungumzia kwa kuwa si msemaji na kumtaka mwandishi kumtafuta DED wa Bagamoyo ili kutolea ufafanuzi zaidi.
“Mgogoro upo lakini mimi sio msemaji nakushauri mtafute Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo ndiye ana taarifa zaidi ya tukio hilo,” amesema.
Bodi ya shule yazungumza
Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, Dk. Veronica Nyerere, amesema ni kweli kuna mgogoro mkubwa na usipotatuliwa kwa haraka unaweza kusababisha mambo mengine.
“Ni kweli kabisa kuna mgogoro mkubwa kati ya Nyambaza na Kivamba na hivi sasa umetengeneza makundi mawili ya shule hiyo na kwa mtazamo huo unachangia kuzorotesha maendeleo ya shule yetu,” amesema na kuongeza:
“Sisi kama bodi tumefanya jitihada za kuwakutanisha walimu hao mara kadhaa ili kumaliza mgogoro huo lakini imeshindikana na hivi sasa Nyambaa kafungua kesi Mahakama Kuu akidai fidia ya Sh milioni 100 kutoka kwa Kivamba.
“Tulikaa nao na kila mmoja akaeleza kwa ufupi (gazeti hili inalo nakala yenye ukurasa tatu) alizojieleza Kivamba akisema kuwa aliwasimamishwa wanafunzi na kuwapigisha magoti na kuwahoji walijibu kuwa wanatoka dukani kwa Nyambaza.
“Wakati anaendelea kuwahoji alitokea Nyambaza na kuwaamuru wanafunzi kutawanyika kwani hawana makosa kwa kwenda dukani wake kisha akamnyang’anya fimbo hali iliyozua taharuki huku makamu mkuu wa shule akishuhudia vurumai hiyo na Kivamba alikwenda kutoa taarifa kwa mkuu wa shule na hatua nyingine zikafuata.”
Amesema katika kikao hicho, Nyambaza alijieleza (Gazeti hili inayo nakala ya ukurasa nne alizojieleza inazo) kuwa awali aligoma kutoa maelezo kwa madai hakupewa taarifa ya sababu ya kuitiwa nini lakini baada ya kueleweshwa aliendelea na mahojiano.
Amesema wajumbe walihoji ni kwa nini alileta notisi ya siku tisa kwa mkuu wa shule na Kivamba wakati yeye ni chanzo cha kuanzisha huduma katika mazingira ya shule baada ya kufungua duka.
Hata hivyo, amesema yeye alianzisha huduma hiyo ili kujikwamua kiuchumi lakini mkuu wa shule aliyeondoka (Agness Mmbanga) alipiga marufuku wanafunzi kwenda kununua vitu dukani kwake na ndiyo chanzo cha mgogoro huo hadi leo.
Kutokana na mgogoro huo, amesema alimua kulifunga duka hilo na baada ya muda mkuu huyo wa shule alipata uhamisho wa kwenda Shule ya Sekondari Fukayosi na kuja Mkuu mwingine mpya, Albert Mganga, aliyemuomba kufungua biashara na kumpa masharti.
Amesema mkuu wa shule alimtaka kuacha kutoa huduma nyakati za vipindi vya shule na kuajiri mtu mwingine wa kufanya kazi hiyo.
Itaendelea