Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Charles Mahera amesema katika zama hizi za maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, Uhitaji wa matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji ni hitaji muhimu na lisiloepukika kwa ajili ya kurahisisha ufanisi katika utoaji Elimu bora.

Ameyasema hayo leo Disemba 18, 2024, akimwakilisha katibu Mkuu Prof Carolyne Nombo Katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Matumizi Bora na salama ya vifaa vya TEHAMA na stadi za kidigitali kwa walimu wa Awali na Msingi

Dkt. Mahera amesema Serikali kupitia programu ya BOOST Serikali ina dhamira ya kusambaza vifaa vya TEHAMA katika Vituo vya Walimu au Shule teule zipatazo 800 na kwa awamu ya Kwanza, vifaa hivyo vya TEHAMA vimeshasambazwa katika Vituo 200 vikiwemo Vituo vya Walimu 57 na Shule Teule 143 nchini

“Kwa mwaka huu Serikali kupitia Programu ya BOOST itanunua na kuweka vifaa vya TEHAMA katika Vituo vya Walimu na Shule Teule 600 zilizobaki ili kukamilisha Vituo vya Walimu/Shule Teule 800 vilivyopangwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa Programu ya BOOST” alisema Naibu Katibu Mkuu mkuu huyo

Sambamba na hilo Dkt Mahera amesema kuwa Mradi huu umetoa Mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu na Walimu wa TEHAMA kutoka katika Vituo hivyo 200 na imepanga kutoa mafunzo kwa washiriki 1800 kutoka katika Mikoa yote na Halmashauri zote Tanzania Bara wakiwakilisha vituo vyote 600 vilivyobaki

Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Lina Rujweka amesema TEHAMA ni mojawapo ya fani zilizowekewa msisitizo kufundishwa katika shule za sekondari mkondo wa Amali. Hivyo ni vema kuanza kuandaa wanafunzi ngazi ya elimu ya awali na msingi kupata stadi za TEHAMA.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa shule Mwl. Ephraim Simbeye amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini, ili kuandaa wahitimu wabunifu wenye maarifa na ujuzi utakao wawezesha kujitegemea, kujiajiri na kuajiriwa wanapohitimu mafunzo yao.