Rais John Magufuli ameutolea uamuzi mjadala wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaopata mimba.
Rais Magufuli, akiwahutubia wananchi mkoani Pwani, amesema bayana kuwa hayuko tayari kuona wanafunzi wanaotiwa mimba wakiendelea na masomo katika shule za Serikali.
Akayaambia mashirika yasiyo ya Serikali kwamba kama yanatetea hao ‘wazazi’ kuendelea na masomo, basi yawaandalie shule, lakini yeye hatokuwa tayari.
Msimamo huo umepokewa kwa hisia tofauti. Wapo waliomuunga mkono, na wapo waliompinga na wanaoendelea kumpinga.

Shida ninayoiona hapa haipo kwa wanaopinga, au wale wanaounga mkono suala hili. Shida ipo kwetu Watanzania kutokuwa na uamuzi wa wengi kwa masuala yanayolihusu Taifa letu. Badala ya kuvutana juu ya faida au hasara za uamuzi huu, ingekuwa vizuri kukawapo uamuzi wa wengi ili kuona hao wengi wanataka nini. Kwa kawaida si lazima uamuzi wa wengi uwe sahihi, lakini ni vizuri ukaheshimiwa.
Hakuna ubishi kuwa Tanzania tumeridhia mikataba mingi ya kimataifa ya haki za makundi mbalimbali ya raia katika nchi yetu. Miongoni mwa mikataba hiyo, umo wa haki ya kila mtoto kupata elimu. Hilo nchi yetu imejitahidi kulitekeleza licha ya vikwazo vingi.
Kama hivyo ndivyo, iweje watoto wanaopata mimba wasiruhusiwe kuendelea na masomo? Kwanza tukubaliane jambo moja hapa.  Nalo ni kwamba Rais Magufuli hajazuia aina hiyo ya wazazi kupata elimu. Anataka wapate elimu, lakini kwa njia nyingine, na si kupitia shule za msingi na sekondari umma. Ndiyo maana anazitaka NGOs kama zinaona zina hoja kwenye jambo hili, zijenge shule za kupokea hao wazazi.
Tunachoweza kuona ni kuwa kwenye jambo lolote sharti kuwe na miiko. Ni haki ya mtoto kupata elimu, lakini ni wajibu wake pia kuzingatia mambo yanayompasa kuyatekeleza ili apate hiyo elimu. Haki na wajibu havitengani. Ni tofauti na lila na fila ambavyo aslani havitangamani.

Kila Mtanzania wa kuzaliwa angeweza kusema ana haki ya kugombea urais, lakini upo utaratibu wa kikanuni wa sifa zinazomruhusu nani agombee, nani asigombee. Kuna kanuni na hata sheria zinazozuia mtu aliyekengeuka kwenye jambo fulani la maadili, asigombee. Mtanzania aliyefungwa kwa makosa ya ujambazi ni Mtanzania. Utanzania wake hauondoshwi na ujambazi wake. Lakini jambazi aliyethibitika kuwa ni jambazi hawezi kusema ananyimwa haki ya kuwania urais licha ya kuwa na sifa kuu – Mtanzania wa kuzaliwa. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba unapokiuka miiko, kanuni, taratibu au sheria fulani fulani, ujue kuna matokeo yake. Kwa jambazi, kitendo chake cha kukiuka taratibu za kimaisha kinamnyima haki ya kugombea urais! Ndivyo ilivyo.
Mtoto wa kike ana haki ya kusoma. Anapokiuka miiko au taratibu zinazomwezesha kusoma, ajue kuna mambo atayakosa mbele ya safari. Kadhalika, mvulana au mwanaume anayemtia mimba mwanafunzi ajue atafungwa hata kama akisema mwanafunzi aliridhia.
Vijana wanaotaka kujiunga katika mafunzo ya kijeshi, wanapimwa afya zao. Walioathirika hawapewi nafasi hiyo. Leo wanaweza kuamka watu kuhoji kwanini hao wanyimwe nafasi ilhali nao ni vijana Watanzania? Wananyimwa kwa sababu ili kujiunga jeshi, kumewekwa vigezo na sifa. Leo vijana wanajua wakiwa wameambukizwa HIV hawawezi kujiunga JWTZ, JKT, Polisi, Uhamiaji, Magereza, Usalama wa Taifa, nk. Huu si uamuzi wa bahati mbaya, bali ni uamuzi unaotokana na kanuni na sheria. Nchi ya watu makini inaishi kwa utaratibu wenye manufaa kwa hiyo jamii.

Nimesikiliza mijadala katika redio na nimesoma mengi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli. Wapo wanaojaribu kuhalalisha mimba miongoni mwa wanafunzi na ugumu wa maisha waliyonayo wasichana wengi. Sababu hii naikubali kabisa. Je, tunaweza kutenganisha ushabiki wa mimba za wanafunzi au uzazi usio na mpango na ongezeko la umaskini? Je, kwa sababu ya umaskini, turuhusu dhambi ya kuvuruga na kuua maadili?
Tukiamua kuchukua sababu ya ugumu wa maisha kama ndiyo huruma ya kuzikubali mimba miongoni mwa wanafunzi; je, itakuwaje kwa wavulana? Turuhusu wavulana wawe mashoga kwa sababu ya ugumu wa maisha kwenye familia zao? Wapi tunakwenda?
Sharti tuukubali ukweli

Wazazi na jamii hatupaswi kuwa na njia za mkato kwenye suala hili. Lazima tukiri makosa yetu yaliyosababisha tufeli kwenye malezi ya watoto wetu. Wazazi au walezi wangapi wana muda (kama ilivyokuwa zamani) wa kuketi na watoto na kuwafundisha mambo ya kimaadili? Waafrika tumekuwa kama panya wa kutumiwa maabara. Tumeutupa utamaduni wetu mzuri na kuukumbatia ‘uzungu’ ambao una mambo mengi yasiyo ya staha. Zamani zile ilikuwa fedheha kwa mtoto wa kike kupata mimba akiwa hajaolewa.
Tulikuwa na mila ya jando na unyago. Wasichana na wavulana waliofikia umri walipelekwa kwenye makambi ya jando na uyango. Huko walipata mafunzo murua kutoka kwa manyakanga na makungwi. Wazungu wametuaminisha hayo ni mambo ya kishenzi. Wakayafananisha na ushirikina. Matokeo yake vijana wamekosa elimu ya uzazi na nyingine za kimaisha.

Suala hili la watoto wanaopata mimba kutoendelea na masomo limekuwapo kwa miaka mingi. Halikuwa na mshawasha wala mjadala kama uliopo sasa. Huu msukumo unatoka wapi?
Lakini ni Wazungu hawa hawa waliotuletea dini zao na kuzifanya zetu zionekane kama mikusanyiko ya kishirikina tu. Wakatuaminisha kuwa kuzaa nje ya ndoa ni dhambi. Leo Watanzania wengi, kama si Wakristo, basi ni Waislamu. Dini zote hizi zinazuia zinaa. Tumeaminishwa kuzaa nje ya ndoa ni zinaa. Madhehebu mengine yameenda mbali hadi kufikia hatua ya kuwaua wasichana au wanawake waliopata ujauzito hata kwa kubakwa!
Leo hao hao waliotuletea dini hizi na kutufudisha hivyo wanatulazimisha turuhusu zinaa. Kama mtoto anafundishwa kosa la dhambi ya kusema uongo au wizi, kwanini asifundishwe kosa la kupata mimba akiwa shuleni?
Msukumo huu unatoka kwa wafadhili na NGOs zao. Kuna fedha nyingi sana zinazomwagwa Afrika kuvuruga mambo ya maana yalivyosalia katika mila, desturi na utamaduni wetu. Tunaletewa fedha ili turuhusu watoto wetu – wa darasa la pili au la tatu – wapate mimba na tuone hilo ni jambo la kawaida! Tunahimizwa watoto wetu wakae madarasani wakilamba ndimu na wakati mwingine wakitafuna pemba! Turuhusu mtoto mwenye mimba awafundishe wenzake mbinu za kuupata ujauzito! Hapana. Wanataka Serikali, katika shule zetu ijenge vyumba maalumu vya kutumiwa na ‘wazazi wanafunzi’ kunyonyesha watoto wao.

Mataifa ya Ulaya na Marekani yana mbinu nyingi. Yameharibu utamaduni wao, sasa yanataka nasi tupokee mambo yao ya ovyo ili tuharibikiwe. Wakati Fulani, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alitangaza mashati makali. Akasema nchi (hasa za Kiafrika) ziruhusu ushoga, vinginevyo hakuna kupokea misaada. Rais Jakaya Kikwete, kati ya mambo ya maana aliyoifanyia nchi hii kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ni kupinga masharti hayo ya kifedhuli.
Ukiacha mafundisho ya kidini, mila zetu Waafrika si tu haziruhusu, bali zinazuia kabisa kuwazia upuuzi wa wanaume kuoana. Pamoja na umaskini wetu (ambao kimsingi ni umaskini wa mawazo tu), tumepinga upuuzi huo.
Wazungu hawa hawa na mawakala wao wameingiza nchini na kusambaza vilainishi kwa mashoga. Wameona hakuna aina nyingine ya msaada wa maana, isipokuwa kutuletea vilainishi!
Rais Magufuli hakuzuia wanaopata mimba kuendelea na masomo. Amesema zipo sehemu nyingi ambazo huyo mwenye mimba anaweza kuendelea na masomo yake. Amezitaka NGOs kama kweli zina uchungu, zianzishe shule kwa ajili ya kundi hilo la wenye mimba.
Naamini uamuzi huu si wa kuwakomoa watoto wetu wa kike, bali unalenga kuimarisha wajibu wa jamii katika kuwalinda watoto wa kike, na wakati huo huo kujenga jamii yenye kufuata maadili. NGOs na watetezi wengine kama wanaweza kuchimba visima ilhali wakijua kazi hiyo ni ya Serikali, sioni kwanini zisijenge shule maalumu kwa watoto wanaopata mimba. Au kama hilo haliwezekani, basi mabilioni ya shilingi yanazopata kutoka kwa wafadhili, yazitumie kutoa elimu kwa watoto wa kike na jamii ili kuepuka janga la mimba kwa wanafunzi.
Au fedha hizo zitumike kujenga mabweni kwa watoto wa kike. NGOs ziwe sehemu ya utatuzi wa matatizo badala ya kuwa sehemu ya mawakala wa uvurugaji maadili ya Taifa letu. Rais Magufuli usigeuke jiwe. Naamini wananchi wengi wanakubaliana na wewe katika hili.