Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amewataka walengwa wa TASAF Wilayani Makete kuchangia nguvu kazi yao ya asilimia 10 ili kuwezesha ukamilishaji wa miradi ya TASAF ya ujenzi wa miundombinu kwa wakati katika Shule ya Sekondari Mang’oto ambayo inatekelezwa kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC).

Ndejembi ametoa wito huo kwa walengwa wa TASAF, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Sekondari Mang’oto iliyopo katika Kijiji cha Mang’oto, Halmashauri ya Wilaya ya Makete, mkoani Njombe.

“Wananchi wa Mang’oto nawaomba mjitoe kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu inayowataka kuchangia nguvukazi yenu ya asilimia 10 ili mshiriki kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.” amesema Ndejembi.

Ndejembi ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada za kutafuta fedha kwa wadau wa maendeleo kuiwezesha TASAF kutekeleza miradi yake kwa lengo la kujenga miundombinu yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga, amemhakikishia Naibu Waziri Ndejembi kuwa, atawahamasisha wananchi wa jimbo lake wachangie nguvu kazi ili kuwezesha miradi yote ya TASAF inayotekelezwa katika jimbo lake ikamilike kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mang’oto, Prince Mwenda amesema, wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaboreshea mazingira ya kupata elimu kupitia ujenzi wa mabweni, madarasa, bwalo na nyumba za walimu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara ya kikazi ya wiki moja mkoani Njombe kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani huo.