Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Jenista Mhagama amesema walengwa wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini Manispaa ya Morogoro unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wamewezeshwa kuendesha mradi wa funza chuma kwa ajili ya kuzalisha chakula cha mifugo ambacho kinawaongezea kipato na kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mifugo.
Jenista amesema hayo, mara baada ya kukagua mradi wa kuzalisha funza chuma, unaotekelezwa na walengwa wa TASAF wa kikundi cha faraja kilichopo katika Kata ya Mazimbu, Mtaa wa Mazimbu Darajani Manispaa ya Morogoro.
Jenista amesema, kumekuwa na shida ya upatikanaji wa chakula cha mifugo hivyo mradi huo unaotumia teknolojia rahisi kuzalisha funza chuma kwa ajili ya chakula cha mifugo utatatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kuku, kondoo, samaki, bata na nguruwe.
“Mmesema hapa kupitia taarifa yenu kuwa, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimefanya utafiti na kubaini kuwa funza chuma ni chakula kizuri cha mifugo kuliko vyakula vingine ambavyo vimekuwa vikitumika kulisha mifugo hivyo mradi huu ni mzuri na wa kimkakati ambao unapaswa kuendelezwa,” amesema Jenista.
Jenista ameongeza kuwa, mradi huo utasaidia kuhifadhi mazingira na kutatua changamoto ya uchafu wa mazingira katika masoko kwani badala ya takataka kutupwa hovyo ndani ya masoko, zitachukuliwa ili kuzalisha chakula cha mifugo na kuacha masoko yakiwa safi.
“Huu mradi ni suluhisho kubwa sana la changamoto ya uchumi, uchafu wa mazingira na suala la ajira kwa makundi yote ya akina mama, vijana na wenye ulemavu na walengwa wa TASAF, kwani ni mradi fungamanishi wenye faida nyingi,” amesema Jenista.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro,Pascal Kihanga amemshukuru Jenista kwa kufanya ziara katika mradi huo wa funza chuma ambao una faida kubwa katika jamii, kwani utasaidia manispaa yake kuwa na mazingira safi na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwaongezea kipato.
Kutokana na faida ya uwepo wa mradi huo,Kihanga amemhakikishia Jenista kuwa, manispaa yake itawatumia Wahandisi waliopo kuwajengea walengwa wa TASAF na wananchi wengine vizimba vya kufuga funza chuma ili waweze kuzalisha kwa wingi chakula cha mifugo ambacho kitawaongezea kipato.