Na Veronica Mwafisi,Kasulu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuendelea kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa ya uwepo wa mikopo ya vikundi ya asilimia kumi inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, iliyotengwa kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia 4:4:2.
Ndejembi ametoa wito huo kwa walengwa wa TASAF wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa mpango huo katika Kijiji cha Nyakitonto, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwenye wilaya hiyo.
Ndejembi amewahimiza walengwa wa TASAF nchini, kujiongezea mtaji kupitia mikopo ya asilimia kumi inayohusisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ili waweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuboresha maisha yao.
“Licha ya kuwa mna vikundi vyenu vya kuweka na kukopa, vilevile mjitahidi kukopa mikopo ya asilimia kumi ya Halmashauri ili muitumie kuboresha maisha yenu, kwani Wakurugenzi walishaelekezwa kutoa kipaumbele pia kwa walengwa wa TASAF wenye sifa ya kukopesheka,’’ alisema Ndejembi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi kwa kufanya ziara katika Halmashauri ya Kasulu ili kuwahimiza walengwa wa TASAF kutumia ruzuku vizuri katika kuboresha maisha yao, na kuahidi kuwa wilaya yake itaendelea kusimamia utekelezaji wa mpango wa TASAF ili kuunga mkono kwa vitendo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.
Naye,Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bi. Catherine Kisanga amesema kuwa, TASAF inategemea walengwa wataunda vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo na kuanza kufanya shughuli za kuwaongezea kipato ili kuondokana na umaskini.
Walengwa wa TASAF wamehimizwa kuichangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 ya Mwaka 2019, iliyotungwa Chini ya Kifungu 37A (4) pamoja na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya Asilimia 10 ya mapato ya ndani za Mwaka 2019 na Marekebisho yake ya Mwaka 2021, inayozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutenga fedha asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia 4:4:2.