Hatua ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kutunga sheria ya kuwaondoa ombaomba jijini inapingwa na Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA), kikidai kutozingatiwa kwa hali na utu wa watu wenye ulemavu. 

Manispaa ya Ilala imetunga sheria ndogo kupiga marufuku ombaomba katika mitaa ya katikati ya jiji na kuwatoza faini ya Sh 200,000 watu wanaowasaidia.

Mwenyekiti wa CHAWATA, Hamad Komboza, ameliambia gazeti hili kuwa utekelezaji wa sheria hiyo utawaathiri zaidi watu wenye ulemavu ambao wengi hawana ajira rasmi na wanaangukia katika kundi la wasiojiweza.

“Kuwarudisha makwao ombaomba si suluhisho. Watu hawa wanaishi wakitegemea misaada kutoka kwa wahisani kwa kuomba katika maeneo mbalimbali baada ya kukosa fursa.

“Chama chetu kilifanya utafiti na kugundua kuwa jamii imewasahau watu hawa ingawa nao wana mahitaji mbalimbali muhimu. Hii ndiyo sababu ya wao kuwa ombaomba,” anasema Komboza. 

Anasema miji mikubwa kama Dar es Salaam ndilo kimbilio la watu hawa waliosahauliwa na jamii, wakiamini wingi wa wakazi wa Dar es Salaam unawapa nafasi ya kupata wafadhili wa kuwapatia fedha za kutatua matatizo yao.

Anashauri serikali kutafuta namna mbadala ya kuwasaidia, ikiwamo kuwapa mitaji wajikwamue kimaisha badala ya kuwaadhibu watu wanaotoa pesa zao kusaidia ombaomba hasa walemavu.

“Maofisa Utawi wa Jamii ndio chanzo cha wingi wa ombaomba mitaani, wameshindwa kubuni mbinu mbadala na sasa wanataka kuwapa nauli za kuwarudisha makwao huku ikifahamika kuwa watarudi tena jijini muda si mrefu,” anasema.

Ameitaka Manispaa ya Ilala kurudi na kusoma tafiti zilizofanywa kama kweli imedhamiria kuliondoa kabisa tatizo hilo, akiongeza kuwa kama mbinu stahiki hazitatumika kuna uwezekano mkubwa wa lengo kutokamilika kama ilivyotokea mara kadhaa.

Mmoja wa watu wenye ulemavu, Siasa Ramadhani, ameliambia JAMHURI kuwa manispaa haiwatendei haki kwa kuwa haijawaandaa kwa namna yoyote kujiimarisha kiuchumi.

“Laiti tungewezeshwa halafu ndipo watuzuie kuonekana mitaani, hakuna ambaye angerudi huku. Kutufukuza ghafla kutatuathiri sana sisi wenye ulemavu kuliko watu wenye nguvu zao,” anasema Ramadhani.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, anasema sheria hiyo ndogo imetungwa kuondoa uharibifu wa mazingira na kero kadhaa zinazosababishwa na ombaomba hao katika mitaa ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Anasema uwepo wao pia umesababisha ongezeko la ukatili kwa watoto.

“Sasa sheria hii itawanusuru watoto wadogo wanaoingizwa kwenye ajira na mazingira hatarishi ili sasa wapate fursa ya kwenda shule. Ni kampeni endelevu itakayosababisha walemavu kuja kwetu (halmashauri/manispaa) kuomba mikopo ya kujikimu kimaisha na kuacha kuombaomba,” anasema Shauri.

Hadi sasa halmashauri hiyo imekwisha kutoa Sh bilioni saba kwa ajili ya kuwawezesha wenye ulemavu, vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi.

Zaidi ya watu 100 wenye ulemavu wamekwisha kupata mikopo ya Bajaj na wanafanya kazi rasmi zinazowapatia kipato halali baada ya kuwezeshwa na halmashauri.

Takriban ombaomba watu wazima 27, wazee 10, wagonjwa wanne na watoto 17 wamekwisha kukamatwa jijini Dar es Salaam na mipango inaendelea ili watoto hao wapelekwe shule kupitia taasisi ya Baba Watoto.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, ameungana na Komboza, akidai kuwa sheria hiyo ndogo iliyotungwa si suluhu la kuondoa tatizo hilo kwa sasa.

“Manispaa ilitakiwa kwanza kujua sababu ya watu hawa kila wanaporudishwa makwao hurejea tena mjini ndipo wajue namna nzuri ya kuwasadia.

“Kazi hii ni ya muda mrefu tangu enzi za Yusuf Makamba (aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam). Alifanya hivyo na bado wakarudi,” anasema Anna.

Anasema suala la ombaomba linahitaji kutafutiwa suluhisho la kudumu ili kuwaondolea changamoto zinazowakabili kama ukosefu wa ajira na umaskini.