Kwanini awe ni Lowassa na si wengine waliotia nia ya kuwania urais? Ukimshtukiza mtu yeyote na kumuuliza ni kada gani kati ya hao waliotia nia angependa awe rais ajaye, kila mmoja atatoa jibu lake kutokana na mapenzi aliyonayo kwa mgombea wake.
Na mimi napenda kutumia makala hii kutoa sababu zinazonifanya nimkubali Edward Lowassa. Awali ya yote natanguliza kuwaomba radhi Watanzania popote walipo ambao nitakuwa nimewagusa kwa hisia hasi, kwani kila mtu ana chaguo lake.
Pia niwaombe radhi baadhi ya watu nitakaowataja kwa majina, nikiwatolea mfano katika kukazia hoja yangu. Niliyoandika humu ni muono wangu na si mwongozo, vigezo, utabiri wala masharti ya chombo kilichonipa nafasi kuandika haya.
Kwa kuanzia, napenda nitamke kwamba wagombea wote waliotia nia kikatiba wanafaa kuchagua na kuchaguliwa. Rejea ibara ya 21 (1) inayosisitiza uhuru wa kushiriki shughuli za umma sheria ya 1984.
Napenda pia kunukuu ibara ya 21 (2) inayosema “Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa” hususan kwenye kuchagua na kuchaguliwa.
Baada ya dibaji hiyo fupi, naomba sasa nijielekeze kwenye mada yangu ya leo inayosema “Kwanini awe Lowassa na siyo mwingine.”
Mchakato wa kumchagua mgombea ni suala mtambuka linalomgusa mtu akiwa na sababu zake binafsi kama vile uhusiano wa kiukoo, baba, mama, dada, kaka, mkwe, shemeji, shangazi, bibi, babu, mjomba na kadhalika.
Zipo pia sababu za kijamii kama jirani, mshirika wa kibiashara, mshirika wa kiroho, urafiki vyuoni, mashuleni, mshirika wa kikazi, na kadhalika. Ukimuuliza Mama Regina Lowassa au Fredy Lowassa kwamba chaguo lao ni nani atakupa jibu ni Lowassa.
Kwa msingi huo, watu wana chaguzi zinazosigana kutokana na kuwapo kwa vinasaba, koo, makazi, kiroho, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Katika uchaguzi pia kuna wapenzi, wafurukutwa, mashabiki, maswahiba, wafuasi na wengineyo.
Kwa mfano, leo hii likitolewa tangazo kuwa wafuasi wa Lowassa popote pale walipo wakamatwe. Amini usiamini, watakaobakia kutetea msimamo wao ni wachache kwa sababu wengi wanamfuata mtu na si chama.
Hata kwenye vitabu vitakatifu tunaelezwa kwamba wakati Yesu Kristo alipokaribia kumaliza muda wake duniani, aliwaita wanafunzi wake na kuwaambia “Kesheni mkiomba, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili dhaifu.” (Mathayo 26:41).
Bila shaka Yesu alitoa tahadhari hiyo akijua kwamba wanafunzi wake walikuwa ni binadamu wa kawaida. Ukweli huo ulibainika baadaye mmoja wa wafuasi wake alipokuja kumsaliti. Turejee (Mathayo 26:47-49).
“Yuda, mmoja wa wale thenashara akaja, na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu, na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema nitakayembusu, huyo ndiye mkamateni. Mara akamwendea Yesu akasema, salamu Rabi, akambusu.” Yuda akawa amemsaliti rafiki yake Yesu.
Sambamba na hilo, Biblia inatukumbusha mfuasi mwingine aliyekuja kumsaliti Yesu. Nanukuu. “Na Petro alikuwa ameketi nje behewani, kijakazi mmoja akamwendea akasema, “Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya?” Akakana mbele ya wote, akisema sijui usemalo.
Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, “Huyu alikuwepo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, simjui mtu huyu”.
Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, “Hakika wewe nawe u mmoja wao, kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo. Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, ‘kabla ya kuwika jogoo utanikana mara tatu.’
Nimelazimika kurejea vifungu hivi kutoka kwenye Biblia Takatifu ili kunisaidia kutoa picha ya kile ninachojaribu kukielezea kuhusu wafuasi, wapenzi, maswahiba na kadhalika, kwamba wako ambao msukosuko ukimtokea mgombea wao, hawawezi kumudu kumtetea kutokana na vitisho.
Nirejee kwenye sababu ambazo zimenigusa mpaka kumwona Lowassa kuwa ndiye chaguo la wengi. Sifa ya kwanza, ni kwamba Lowassa ana uwezo wa kuhimili misukosuko ya kisiasa. Kwa wale wanaomfuatilia Lowassa kisiasa, watakubaliana na mimi kwamba ni kiongozi mvumilivu na mkomavu wa kisiasa.
Ukiachana na mashambulizi haya ya majitaka, Lowassa alipokubali kuachia nafasi yake ya uwaziri mkuu, hakujitokeza kumtuhumu wala kumkashifu mtu kutokana na tukio hilo. Hakusikika kwa muda wote alipokaa bungeni akimnyooshea mtu kidole ama viongozi wenzake, au watendaji kuwa ndiyo waliosababisha apoteze uwaziri mkuu.
Hili linaonesha namna alivyokubali kuupa kipaumbele uzalendo na utaifa. Kitendo hicho kinathibitisha kwamba Lowassa anaweza kuhimili misukosuko ya kisiasa akipata urais. Ni mtu ambaye hana ubinafsi, visa, unafiki. Ni mwepesi kukubali matokeo ya aina yoyote kisiasa.
Sambamba na hilo, kwa kipindi chote alichofungiwa na Kamati ya Maadili ya chama chake kwa sababu za kuanza kampeni mapema, hakuwahi kulalamika wala kuikosoa Kamati hiyo. Hii inaonesha namna anavyoheshimu viongozi wake wa chama.
Sifa ya pili, Lowassa ni chaguo la Mungu. Lowassa amejitokeza na kujikusanyia wapenzi na wafuasi wa dini zote hapa nchini. Wakristo, Waislamu na wapagani, kila kona ya nchi wanamwombea Lowassa afanikiwe.
Ifahamike kwamba viongozi wa kiroho (mapadri, mashehe, wachungaji) wanamwakilisha Mungu duniani. Hivyo sauti zao ni sauti ya Mungu. Maombi yao inaashiria chaguo la Mungu ambaye ni Lowassa.
Sifa ya tatu, Lowassa ana kipaji. Mtu mwenye kipaji cha uongozi, kamwe kipaji chake hakiwezi kuzikwa kwa matakwa ya watu wachache. Kipaji cha Lowassa kilianza kung’ara akiwa kijana mdogo (Leo sitaingia kwenye historia yake). Kama hiyo haitoshi, kipaji chake kimeonekana katika kila wizara alikopita, kwani aliacha kumbukumbu tofauti na mawaziri wengine.
Sifa ya nne, Lowassa ndiye tochi ya wanyonge tofauti na watu wanavyomchukulia. Lowassa anatoka katika kabila la Wamaasai. Asilia ya Wamaasai ni wafugaji ambao utajiri wao unatokana na mifugo.
Wamaasai hawana tabia ya wizi wa kutumia kalamu (teknolojia), nguvu, wala wizi wa kutumia vyeo. Kawaida ya Wamaasai ni kuchapa a kazi. Wanapata utajiri kutokana na jasho lao. Nitaendelea kujadili hili wiki ijayo.
Mwandishi wa makala hii ni mwanasiasa na msomaji wa gazeti hili. Kadhalika, ni mchambuzi wa masuala ya siasa hususani za hapa nchini. Aliwahi kuwa Mbunge wa Temeke. Anapatikana kwa simu namba 0713-399094 / 0767-399004 au barua pepe: [email protected]