Na: James Mwanamyoto-OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hatosita kumchukulia hatua Mkurugenzi yeyote wa Halmashauri ambaye atabainika kushindwa kutekeleza kikamilifu ujenzi wa miradi ya miundombinu ya afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Mhechengerwa amesema hayo leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Idara ya Afya, ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI kilicholenga kujadili utekelezaji wa majukumu ya idara hiyo pamoja na kuhimiza uwajibikaji.
Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kujipanga kikamilifu kusimamia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya afya kwa wakati.
Mchengerwa amesema kuwa, kama kuna halmashauri imepelekewa fedha na kubainika kushindwa kukamilisha kikamilifu ujenzi wa miradi ya miundombinu ya afya, hatosita kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi.
“Nipatieni orodha ya wote walioshindwa kukamilisha miradi, wabadhilifu wa fedha za miradi, waliojenga chini ya kiwango na wale ambao wamepelewa fedha lakini bado zipo kwenye akaunti ili niwachukulie hatua za kinidhamu bila kuchelewa,” amesistiza Mchengerwa.
Mchengerwa amewahimiza watendaji wanaosimamia ujenzi wa miradi ya miundombinu ya afya kufanya kazi kwa bidii na weledi kwani haofii kuchukiwa na wale atakaowawajibisha kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Aidha, Mchengerwa amewataka watendaji wa ofisi yake kushirikiana na wawakilishi wa wananchi katika kubaini maeneo ya kujenga miradi ya miundombinu ya afya kulingana na uhitaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Ndugange amemhadi Mhe. Mchengerwa kuwa, Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe haitomuangusha katika kutekeleza majukumu yake na maelekezo yote aliyoyatoa katika kikao kazi hicho.