Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Katika kuadhimisha Siku ya Udongo Duniani, Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanaagronomia Tanzania (Tanzania Agronomy Society – TAS) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewakutanisha wadau wa kilimo ili kuhamasisha matumizi sahihi ya udongo kwa maendeleo ya kilimo na usalama wa chakula.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Boniface Massawe, Mkuu wa Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia kutoka SUA, alisema upimaji wa udongo ni hatua muhimu kwa wakulima ili kuelewa hali ya virutubisho vya udongo wanaotumia.
“Udongo ni msingi wa kilimo. Bila kujua hali yake, wakulima wanaweza kutumia mbolea zisizofaa au kupanda mazao yasiyofaa. Ndiyo maana leo tunatoa elimu kuhusu umuhimu wa kupima udongo kabla ya kulima,” alisema Dkt. Massawe.
Katibu Mkuu wa TAS, Emmanuely Zephaline, alisema ushirikiano wao na SUA unalenga kuelimisha wakulima kuhusu upimaji wa udongo ili kuboresha mavuno na kuchangia ustawi wa chakula.
Dkt. Sibaway Mwango, Mratibu wa Utafiti wa Udongo kutoka TARI Mlingano, alisisitiza kuwa wakulima wanapaswa kupima udongo wa mashamba yao kabla ya kulima ili kuongeza tija na kudumisha rutuba ya udongo. Alionya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mbolea yanaweza kuharibu udongo na kuathiri mazingira kwa muda mrefu.
“Kuna maeneo mengi nchini ambako udongo umechoka kabisa kwa sababu wakulima hawajui mbolea sahihi za kutumia au njia bora za kuhifadhi udongo,” alisema Dkt. Mwango.
Wakulima waliohudhuria maadhimisho hayo waliiomba serikali na wadau wa kilimo kuhakikisha huduma za upimaji wa udongo zinapatikana kwa gharama nafuu.
“Ni muhimu elimu ya upimaji udongo ifike kwa wakulima wa vijijini, ambao ndio walengwa wakuu wa kampeni hii,” alisema mmoja wa wakulima.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), udongo wenye afya si tu unachangia uzalishaji bora wa mazao bali pia husaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudumisha maisha ya viumbe hai ardhini.