Na Rahma Khamis, JamhuriMedia, MAELEZO

Wajasiriamali wa kilimo cha mboga mboga mboga na matunda wametakiwa kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwelewa wakulima wa viungo mboga mboga na matunda kuhusiana na usawa wa jinsia huko Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Afisa Muwezeshaji Wanawake Kiuchumi TAMWA Nairat Abdalla Ali, amesema katika Sekta ya kilimo wanawake bado wapo nyuma kimaendeleo hivyo kuwapatia mafunzo hayo itawasaidia kuweka usawa katika sekta hiyo.

Amefahamisha kuwa wanawake wengi ni wakulima lakini hawamiliki ardhi wanategemea kutoka kwa wanaume jambo ambalo linapelekea kupoteza muda na nguvu bila ya mafanikio hivyo mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kujiamini na kuweza miliki ardhi kwa ajili ya kilimo.

Akiwasilisha mada ya usawa wa jinsia Mkufunzi, Lulu Mzee Mohammed amesema miradi mingi ya kimaendeleo hushiriki wanaume pekee kutokana na mfumo dume kuwa kazi za nyumbani ni mwanamke tu jambo ambalo sio sahihi kwani wote wana haki kwa mujibu wa sheria.

Alifahamisha kuwa usawa wa kijinsia ni hali ya kupata haki sawa kwa wote ikiwemo elimu, afya na mambo yote ambayo huleta manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Aidha ameeleza kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii ni jambo la msingi kwani kipindi kirefu walikuwa wako nyuma kimaendeleo lakini kwa sasa jitihada mbalimbali zinachukuliwa kuwainua hasa katika kilimo ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi Nchini.

“Kila mwanadamu ana haki ya kiusawa mbele ya sheria hasa katika matumizi ya technolojia za kilimo kwani dira ya kilimo 2050 inalengo la kuwaweka wanawake katika usawa wa jinsia”, alieleza Bi Lulu

Nae Afisa Biashara na Masoko Mradi wa Viungo Zulfa Rashid amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa vjana na wanawake kwani wao ndio wahusika wakuu ambao wanakumbana na changamoto nyingi za kijinsia katika jamii.

Amesisitiza kuwepo upendo katika jamii kwani familia nyingi zimekuwa hazina mashirikiano kwa kisingizio cha ukali wa maisha hali inayopelekea kukithiri kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

“Tatizo lililopo katika jamii wanaume kukosa kuwasikiliza wanawake na kujiona wao ndio wao jambo ambalo linarejesha nyuma upendo wa mama kwa waume zao na kuwaachia ulezi akina mama pekee,”aliasema Afisa .

Nao wakulima wa mradi huo wameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo na kwani walikuwa wanayahitaji fursa hiyo kwa muda mrefu ili kujiendeleza zaidi katika kilimo chao.

Wamewaomba wanaume wasiwabane wanawake endapo wataamua kushiriki katika miradi ya maendeleo ili wapate kufanikisha maamazio na mafanikio waliyojiwekea katika harakati zao za kujiletea maendeleo.

Aidha wamewaasa wanawake wenzao,Vijana na jamii kwa jumla kujitokeza na kushiriki katika kilimo cha biashara ili kujiinua kiuchumi na taifa kwa ujumla.

Mradi wa viungo Zanzibar unatekelezwa kwa mashirikiano kati ya TAMWA,PDF na Comunity Forest Pemba (CFP) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia Mradi wa Agri -Connect.

Mwasilishaji mada Lulu Mzee Mohammed akizungumza na wakulima wa mbogamboga,matunda na viungo wakati alipokua akiwasilisha mada ya USAWA WA KIJINSIA kwa wakulima hao,hafla iliyofanyika ukumbi wa Studio Raha leo Mjini Unguja.Juni 26,2023.
Biashara na Masoko wa Mradi wa Viungo Zanzibar, Zulfa Bashiri Mbwana akizungumza na wakulima wa mradi huo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwelewa wakulima hao juu ya Usawa wa Kijnsia yaliofanyika Ukumbi wa Studio Raha leo Mjini Unguja.Juni 26,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Mkulima wa mbogamboga Shehia ya Mkataleni Wahida Haji Simai akichangia mada wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wa usawa wa kijinsia wakulima wa mbogo mboga,viungo na matunda walio chini ya mradi wa viungo unaofadhiwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa kwa mashirikiano kati ya TAMWA Zanzibar , PDF pamoja na Community forest Pemba (CFP) kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo,hafla iliyofanyika Ukumbi wa Studio Raha leo Mjini Unguja.Juni 26,2023
Afisa Mwezeshaji Wanawake kiuchumi TAMWA Zanzibar Nairat Abdalla Ali akiwasaidia mawazo wakulima wa mbogamboga wakati walipokua wakijadiliana katika vikundi kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa wakulima hao yaliohusiana na usawa wa kijinsia huko ukumbi wa Studio Raha leo Mjini Unguja.Juni 26,2023.