Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakulima wa Tanzania wanaozalisha mazao ya chakula na kuyauza kwa Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula Nchini (NFRA) wamelipwa bilioni 347 katika miezi minane iliyopita — kuanzia mwezi Julai 2024 hadi mwezi huu.
Akitoa taarifa hapa juu ya ununuzi wa mazao katika msimu uliopita, uimarishaji wa wakala kuelekea kujitegemea na matazamio katika msimu wa ununuzi wa mazao ujao, Mkurugenzi Mkuu wa NAFRA, Dkt Andrew Komba, alisema malipo yote yamekamilika na kwamba hakuna mkulima ambaye anaendelea kuidai NFRA.
“Endapo kuna mtu atasema kuwa bado anatudai hela basi atakua hajafuatilia taarifa za malipo katika akaunti yake au kuna baadhi ya taarifa zake hakuzihakiki vyema. Lakini kwa upande wetu tumelipa madeni yote na kwa sasa tunaenda kuanza msimu mpya wa manunuzi tukiwa hatuna deni kutoka kwa wakulima,” alisema Dkt Komba.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002516560-1024x682.jpg)
Dkt Komba alieleza kuwa jukumu la NFRA ni kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kuhakikisha taifa lina shehena ya mazao yakutosha hata kama nchi inapitia changamoto za njaa au majanga ya muda mrefu.
Alisema katika kutekeleza jukumu hilo, NFRA imekua ikinunua kidijitali mazao ya nayozalishwa na Watanzania na kuyahifadhi katika maghara yake.
“Miongoni mwa mazao ambayo tumekua tukinunua kutoka kwa wakulima ni pamoja na mahindi, mtama, mchele,dengu pamoja na mbaazi,” alifafanua na kuongeza kwamba NFRA ina madaraka ya kuuza mazao nje. Amesema mpaka sasa NAFRA imeuza takribani tani 600,000 katika masoko ya kimataifa katika nchi za China, India, Congo DRC, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Msumbiji.
Amefafanua kuwa kwa mauzo hayo ya nje NFRA imekusanya takribani bilioni 540 na fedha hiyo imetumika kulipa mikopo benki, kukarabati maghala na barabara na pia kuwalipa wakulima kwa mazao.
Amesema NFRA imevunja rekodi kwa kukusanya tani za mazao ambazo hazikupata kukusanywa. Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 NFRA ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi takribani tani 351,000. Lakini sasa NFRA inahifadhi tani 776,000 katika maghala yake.
“Ili kuhakikisha nchi inakuwa na hifadhi ya kutosha Rais Dkt Samia aliiwekea NFRA lengo la kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 3,000,000 ifikapo mwaka 2030. Hivo jitihada za kulifikia lengo hilo zimekuwa zikiongozwa na Rais Samia mwenyewe pamoja na Waziri wa Wizara ya Kilimo Hussein Bashe. Na sisi wanafanyakazi wa NAFRA tumekuwa tukishirikiana ili tulifikie lengo hilo,”alisema Dkt Komba.
Alifafanua kuwa tani 300,000 zitabakishwa katika maghala kwa ajili ya usalama wa chakula nchini. Kwa maana ya kwamba ikitokea uzalishaji wa chakula ukapungua basi NFRA itakuwa na uwezo wa kulilisha taifa kwa mwaka mzima.
Aidha,ili NFRA iweze kujiendesha yenyewe kama taasisi ilianza kufanya biashara ya kuuza shehena ya mazao katika masoko ya kimataifa yakiwemo China, India, Congo DRC, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Msumbiji pamoja na Malawi.
“Njia hii ya kuuza mazao imekua ni biashara yenye tija kwa Wakala kwani tumeweza kuuza mazao yenye thamani ya bilioni 540 ambapo katika pesa bilioni 347 zimetumika kuwalipa wakulima na kufanya ukarabati wa miundombinu ya majengo na barabara,” alisema Dkt Komba
Amesisitiza kuwa kati ya tani 7760,000 ni tani 400,000 tu zitauzwa katika masoko ya ndani na nje na tani 300,000 hazitouzwa ili kulinda usalama wa chakula nchini.
Ikumbukwe kuwa kuna wakati NFRA ililalamikiwa kwa kutowalipa wakulima kwa wakati, lakini Dkt Komba amesema hadi Desemba mwaka jana NAFRA ilikwisha walipa wakulima wote.