Viongozi wa vyama vya ushirika mkoani Ruvuma, wanatumia hesabu za kisayansi kuwaibia wakulima mabilioni ya shilingi, hali iliyozaa mtafaruku mkubwa. Chama Kikuu cha Ushirika Songea, Namtumbo (SONAMCU) kimesambaratishwa baada ya viongozi kufukuzwa uongozi katika vyama vya msingi kwa tuhuma ya kuwaibia fedha wakulima wa tumbaku.
Meneja wa SONAMCU, Salum Mbuyu, amethibitisha hilo na kusema wanasubiri mwongozo wa Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini, kwani yeye hana la kusema kwa kuwa naye yupo kwenye chumba mahututi.
“Mwenyekiti wa SONAMCU, Awami Kuyevereka, alijiuzulu, akaingia January Komba akajiuzulu, naye Omary Abeid wa Chama cha Msingi Litepeka akakaa kujaribu bahati yake sasa amejiuzulu. Sasa hapo SONAMCU si ipo chumba mahututi?” anahoji Mbuyu.
Ameimbia JAMHURI kwamba suala la wao kuongeza makisio hawahusiki na wala hawalijui, bali anachokifahamu ni kuwa kampuni za ununuzi wa tumbaku ndizo zinazohusika na suala hilo kwa sababu makisio ya mabwana shamba wao ndiyo yanayotumika.
Amesema kampuni zina mabwana shamba kwenye vijiji ambao kabla ya wakulima kutengeneza makisio yao, wao wanapeleka kwa viongozi wao wa juu taarifa za kiasi cha tumbaku kinachotarajiwa kuzalishwa kwa mwaka husika kwa ajili ya maandalizi ya ununuzi.
Alipohojiwa, Mwenyekiti wa SONAMCU aliyejiuzulu, Awami Kuyevereka, amesema agizo la Waziri Mkuu Pinda limezua balaa kubwa katika vyama vya msingi, kwani uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Namtumbo umetumia agizo hilo kuisambaratisha SONAMCU.
Kuhusu kuongeza makisio na kuwa tofauti na yale yaliyotoka katika vyama vya msingi, amesema hawezi kueleza hili atakalolisema eti kwa sababu amejiuzulu, bali anakiri kuwapo kwa tatizo hilo kwa kuwa hata alipokuwa madarakani alilishuhudia hilo likitendeka.
“Hiki ni kipindi cha Ramadhani [Jumatano Agosti 7), ukweli makisio yanaongezwa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa kupitisha makisio hayo, ambapo maafisa ushirika wa wilaya na mkoa wanashiriki na kubariki kwa kuwa kunakuwa na kiasi chao katika mgawo,” anasema Kuyevereka.
Amedai kuwa wakati mwingine maafisa ushirika wanadai wapewe chao kabisa, ndipo waruhusi makisio hayo yaliyoongezwa yapitishwe na kupelekwa benki baada ya kufuta makisio halisi yaliyoandikwa na vyama vya msingi.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma, Watson Nganiwa, ameiambia JAMHURI kwamba yeye hajabariki kuongeza makisio hata siku moja na kwamba anayesema hivyo ajitokeze athibitishe jambo hilo.
Kampuni za ununuzi wa Tumbaku nchini ziitwazo TLTC na Alliance One, zimesema zenyewe hazihusiki na makisio ya vyama vya msingi bali zinahusika na ununuzi tu.
Afisa mmoja ameiambia JAMHURI kuwa makisio yanatengenezwa na vyama vya msingi na kupelekwa SONAMCU, ambako yanatengenezwa ya Mkoa mzima wa Ruvuma kisha wanaitisha Mkutano Mkuu Maalum ambao Mrajisi Msaidizi wa Mkoa na maafisa ushirika wa wilaya wanashiriki, baadaye takwimu za makisio zinapelekwa benki na wao wakiridhika wanaandikisha mkataba wa mkopo na msambazaji wa pembejeo.
Mchezo wa Benki
Katika sakata hilo, benki za CRDB na NMB Songea, zinadaiwa kuhusika na mchezo wa kuwaumiza wakulima kutokana na kupokea nyaraka za makisio ya mikopo ya vyama vya msingi kupitia SONAMCU, ambazo zimefutwafutwa kienyeji na kuongezwa makisio.
Kiasi cha fedha kilichoongezwa kwenye makisio hayo huwa kinalipwa na wakulima wa tumbaku waliopo kwenye vyama vya msingi, ambao hali zao zimekuwa duni huku wakilia kwa kuwa kiasi wanachopata baada ya kukatwa madeni ya mkopo kinawafanya washindwe kumudu gharama za maisha.
Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, Meneja wa CRDB Songea, Enock Lugenge, alisema yeye si msemaji wa kampuni, na mhusika na hilo yupo makao makuu Dar es Salaam, lakini pia kwa sheria za kibenki haruhusiwi kutoa siri za mteja wake.
“Hivi kwa nini usiende kuchukua taarifa hizo SONAMCU ambao nadhani ndiyo wahusika wakuu wa kutoa taarifa kama hizo?” aliuliza meneja huyo.
Kwa upande wake Meneja wa NMB, Rehema Kiputiputi, ilipofika saa 10:44 jioni, Agosti 8, mwaka huu, alimpigia simu mwandishi wa habari hizi akimtaka asitoe habari hizo kwanza, huku akimpa polisi kwa kutojibu maswali ya gazeti hili aliyoandikiwa siku saba zilizopita.
Tarehe hiyo hiyo saa 1:45:36 usiku, Kiputiputi alimtumia mwandishi ujumbe mfupi usemao; “Za mida, nakutumia kahela kidogo uweze kuwasiliana naye pindi mambo yatakavyokuwa sawa. Tulitegemea angefika jana ili muongee ila naomba uwe mvumilivu kidogo sender: +255784310081.”
Ilipofika saa 1:53:20 usiku ikiwa ni dakika nane tangu Meneja atume ujumbe huo hapo juu Agosti 8, mwaka huu, mwandishi alipokea ujumbe kutoka kwa mfanyakazi wa NMB, uliosema: “M-PESA T54G0596 imethibitishwa umepokea Tsh. 30,000 kutoka kwa ALPHONCE GASPERY tarehe 8/8/13 saa 7:52 PM Salio lako la M-PESA ni Tsh.30,490.”
Vita Kawawa apasua jipu
Mchongo huu umebainika baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa, kupasua bomu kwa Waziri Mkuu Pinda jinsi wakulima wa tumbaku wanavyoibiwa fedha kiufundi.
“Ndugu wananchi wa Namtumbo niseme nisiseme?” alihoji Kawawa kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wakaitikia; “Semaaaaa.” Akaendelea; “Nifichue nisifichue?” Wananchi wakaitikia; “Fichuaaaaa.” Ndipo Kawawa akasema: “Wakulima mnaibiwa na viongozi wenu wa vyama vya msingi na SONAMCU kwa kuwaongezea madeni kupitia makisio yenu.”
Waziri Mkuu aliposikia hilo pale pale aliuagiza uongozi wa Serikali ya Mkoa kulishughulikia suala hilo na apelekewe majibu ya utekelezaji haraka, agizo ambalo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu, alisema amelibeba na atalishughulikia.
Pinda alielezwa taarifa hiyo kwenye mkutano wa hadhara Julai 17 mwaka huu wilayani Namtumbo alipofanya ziara ya kikazi ya siku 8 mkoani Ruvuma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Kawawa, amefafanua kuwa alianza kutambua kuwa kuna tatizo kwa wakulima wa tumbaku nchini kote mwaka 2006, ambapo uzalishaji ulishuka kutoka tani 9,000 hadi tani 897.
Yeye akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku nchini, aliamua kufanya uchunguzi na kubaini kuwa tatizo ni kuwa wakulima walikatishwa tamaa kutokana na kipato duni wakati wa malipo, kulikosababishwa na kukatwa riba mara mbili yaani ya benki na ya kampuni ya ununuzi wa tumbaku.
Hivyo waliamua kubadilisha na kutengeneza mfumo utakaomwezesha mkulima wa tumbaku kumudu gharama za pembejeo kama vile kukopa mbolea na dawa moja kwa moja kupitia benki.
Kwa kutumia mfumo huo mpya, vyama vyao vya ushirika vya msingi vilipata faida mwaka 2007/2008, 2008/2009 na msimu wa 2009/2010, jambo ambalo limeonekana kuwakera baadhi ya watu wachache waliokosa kunufaika kupitia mgongo wa wakulima.
Kawawa alisema msimu wa 2011/2012 viongozi wa chombo cha juu kinachoshughulikia zao la tumbaku waliwarubuni viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na kufanikiwa kuwa vyama vikuu ndivyo vipokee makisio na kupeleka benki kwa niaba ya vyama vya msingi vya ushirika.
Alisema mabadiliko hayo yamezua utata mkubwa unaoashiria kuwapo kwa wizi wa kumwibia mkulima kupitia makisio ya mikopo yao inayopelekwa benki.
Akitolea mfano hai, alisema kwamba katika Jimbo lake la Namtumbo kuna chama cha msingi SULUTI, ambacho makisio halisi ya mkopo ni dola za Kimarekani 104,000 lakini kilichoonekana kupelekwa benki ni dola za Kimarekani 188,000 maana yake dola 84,000 ziliongezwa na deni hilo kulipwa na mkulima.
Hivyo amesema yeye akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku hatakubaliana wala kuwaunga mkono watakaobainika kuwaibia wakulima wa tumbaku, kwani hatimaye anayelaumiwa ni Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku.
Uchunguzi umebaini kuwa baada ya agizo hilo la Pinda, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Abdula S. Lutavi, ndiye aliyekuwa chanzo cha mgogoro huo baada ya kuwakataza viongozi wa vyama vya msingi kutumia dola za Kimarekani katika kutengeneza makisio yao ya mkopo benki.
Pia mkuu huyo wa wilaya aliwataka viongozi wa vyama vya msingi kutengeneza makisio yao na kuyapeleka katika Benki ya NMB Namtumbo na si benki za NMB na CRDB zilizopo Songea.
“Kuanzia sasa acheni kufanya biashara ya tumbaku kwa malipo ya dola kwa kuwa shilingi yetu ni dhaifu na kinacholipwa ni kile kile kilichopo kwenye makisio wala hakiongezeki hata kama dola itakuwa imepanda,” alisema DC Lutavi.
Kutokana na msimamo huo wa mkuu wa wilaya, viongozi wa vyama vya msingi walianzisha mgogoro dhidi ya DC huyo kuwa ana lengo la kutaka kuvuruga biashara ya tumbaku kwa manufaa yake. Baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi walipita kueneza taarifa au uvumi wakidai kuwa DC Lutavi anataka kutumia Benki ya NMB Namtumbo kujinufaisha kwa kuahidiwa kupewa mkopo mkubwa endapo jambo hilo litafanikiwa.
Alipoulizwa ofisini kwake wilayani Namtumbo Julai 30, Mwaka huu, Lutavi alikanusha habari hizo na kusema ushirika ukifanya vizuri una manufaa makubwa kwa wakulima wa tumbaku, wananchi kwa ujumla na serikali.
Alisema wilaya yake ilikuwa inazalisha hadi kilo milioni tano (5,000,000) lakini hivi sasa inazalisha kilo 2,900,000.
Baada ya kuangalia takwimu, alizungumza na viongozi wa vyama vya msingi zaidi ya mara tatu akiwataka wakawaeleze wanachama wao juu ya kutotumia dola, lakini wao hawakufanya hivyo hadi alipopita kueleza upungufu huo kwenye mikutano ya hadhara.
Walipochunguza makisio waligundua yalikuwa hayapitishwi kwa Afisa Ushirika wa Wilaya ya Namtumbo, bali yalipitia kwa Afisa wa Wilaya ya Songea na kupata baraka za Afisa Ushirika wa Mkoa kisha kupelekwa kwenye chama chao kikuu cha SONAMCU kilichoingia mkataba na benki kwa niaba ya vyama vya msingi.
Akitolea mfano wa kuongeza kiwango, alisema msimu wa kilimo 2011/2012 kuna chama kimoja cha msingi makisio yao yalikuwa dola 175,000 lakini hadi nyaraka hizo zinafika benki kiwango kilibadilishwa kwa kufutwa na wino wa kufutia (correction fluid) na kuandikwa dola 220,000 kwa maana hiyo dola 45,000 ziliongezwa.
Aliutaja mfano mwingine hai kuwa Chama cha Msingi Mtonya makisio halisi ni dola 80,000, ukomo wa kukopa benki kwa chama cha msingi ni dola 300,000 lakini makisio yaliyopelekwa benki na SONAMCU ni dola 200,000 hivyo dola 120,000 ziliongezwa kwa manufaa ya wajanja wachache.
Mkuu wa wilaya alisema kibaya zaidi ni pale chama hicho cha msingi kilipokopeshwa mali ambayo walikwishailipia msimu uliopita stock yao ambayo hawakupaswa kuilipia tena. Msimu wa kilimo 2013/2014 Lutavi alisema makisio yaliyopelekwa benki za NMB na CRDB Songea yana thamani ya dola 4,529,138.49, jambo linaloshangaza msimu uliopita 2012/2013 kulikuwa na stock ya mbolea waliyokatwa wakulima yenye thamani ya dola 1,140,000. Hapa napo kuna kuzidisha kiasi.
Alisema kimahesabu makisio kwa msimu wa kilimo 2013/2014 yalitakiwa yaoneshe dola 3,389,138.49 kwa kuwa haoni sababu ya mkulima wa tumbaku kuombewa mkopo kwa kitu alichokilipia.
“Ni ujinga kuchukua fedha nje ya wilaya nyingine kwa kuwa ukikifanya kitendo hicho kiuchumi unaitwa uzuzu,” alisema DC akihoji kwa nini mikopo isichukuliwe katika benki ya NMB na CRDB Songea wakati hapo hapo Namtumbo kuna tawi la NMB.
Aliongeza kuwa endapo NMB Namtumbo itatumika kupitisha makisio ya mikopo ya wakulima wa tumbaku kwa msimu wa 2013/2014, benki itakuwa na uwezo wa kuzungusha kiasi cha Sh bilioni 14 kwa mwaka mmoja.
Kimahesabu, msimu wa 2011/2012 wakulima wa tumbaku Wilaya ya Namtumbo pekee waliibiwa zaidi ya Sh bilioni 1 na kama msimu wa 2013/2014 isingeshtukiwa basi wangelizwa zaidi Sh bilioni 1.7. Kwa wastani huo kila msimu wakulima walilipa deni hewa zaidi ya Sh bilioni moja.
RC Ruvuma alonga
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, kwa upande wake ameithibitishia JAMHURI kuwa ni kweli mgogoro huo upo, lakini kwa sasa hawezi kusema moja kwa moja kwamba kuna wizi, bali atatamka rasmi pale atakapopelekewa taarifa ya uchunguzi wa kimahesabu kutoka kwa wataalamu.
Mwambungu alieleza kwamba wataalamu hao wa ukaguzi wa mahesabu yaani (auditors) wangeanza kazi hiyo ya uchunguzi Agosti 5, mwaka huu na wakikamilisha atatoa taarifa rasmi.